Header Ads

Blogger Tips and TricksLatest Tips And TricksBlogger Tricks

DK TULIA AJIANGALIE NA MAMBO MATANO

 
Dk Tulia Ackson amechaguliwa kuwa naibu spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Hiyo ni baada ya kumshinda mpinzani wake kutoka chama cha CUF, Magdalena Sakaya.
Hata hivyo, licha ya kupata ushindi huo, kuna mambo matano ambayo Dk Tulia anapaswa kujirekebisha na hasa atakapokuwa akiliongoza Bunge hilo.
Kwanza, anatakiwa kujiamini. Jana wakati akiomba kura kwa wabunge, Dk Tulia alionekana kutojiamini kiasi kwamba hata hotuba yake ya dakika tatu tu alizopewa alikuwa akiisoma. Unapopata dakika chache kama hizo unatakiwa kuonyesha umahiri wako, hasa ikizingatiwa kuwa alijua mapema kwamba angekwenda kuomba kura kwa wabunge.
Lakini pia, wakati akijibu maswali alionekana kutojiamini zaidi kwa sababu badala ya kujibu maswali, alitaka kutoa maelezo marefu jambo ambalo lilifanya ashindwe kujibu maswali mawili na kuruhusiwa kuondoka kutokana na kelele za wabunge wa upinzani.
Pili, awe mtulivu zaidi kama jina lake. Unapokuwa na nafasi kama ya naibu spika unatakiwa kuwa mtulivu. Lakini wakati akiomba kura na wakati wa maswali kutoka kwa wabunge, Dk Tulia hakuwa ametulia na alionekana kama hakujiandaa. Atakapokuwa analiongoza Bunge anatakiwa kutulia zaidi na asikubali kuyumbishwa.
Tatu, asipende mapambano. Unapokuwa naibu spika unatakiwa kusikiliza pande zote mbili, wapinzani na chama tawala. Kosa kubwa ambalo hufanywa na viongozi wetu ni kujaribu kupambana. Wakati akijieleza na wakati wa maswali, wabunge wa upinzani walikuwa wakimchokoza, ndipo Dk Tulia alipotaka kupambana kwa kutaka kujibizana nao na kama si busara za Spika Job Ndugai kuingilia kati na kumruhusu aondoke, huenda angesababisha mabishano makubwa.
Unapokuwa sehemu kama hiyo unatakiwa kuwashawishi wabunge wakusikilize na si kupambana nao.
Nne, awe na maelezo mafupi. Kwa mazingira ya sasa ya Bunge letu ambalo limejaa ushabiki zaidi wa kivyama, Dk Tulia anapaswa kujua kuwa maelezo marefu yanaweza kusababisha kutoka nje ya mstari na kuibua maswali kwa upande mmojawapo. Ni vizuri kujikita katika majibu ya moja kwa moja kuliko kutoa maelezo ambayo pengine hayawezi kusaidia sana.
Tano, asidhani anaowaongoza ni mbumbumbu. Kwa kiwango chake cha elimu na nafasi alizowahi kushika, hapana shaka kuwa Dk Tulia ni mjuzi na mbobezi. Hata hivyo, ajue kuwa aliowashinda pia wamebobea katika masuala ya kanuni za Bunge na sheria za nchi ila yeye amepata fursa. Nilipokuwa nikifuatilia majibu ya Dk Tulia kutokana na maswali ya wabunge, niligundua alikuwa akitaka kujionyesha kuwa yeye si mtu wa mchezo.
Alidhani maswali anayoulizwa ni ya mtego, hivyo akataka kuonyesha umahiri kwa kutoa maelezo yasiyohitajika. Katika nafasi ya uongozi kuna majaribu mengi, hizo ni changamoto za kawaida, lakini akijaribu kudhani anaowaongoza hawajui atajiweka katika matatizo wakati wote katika Bunge lenye mihemko ya kisiasa. Kwa ujumla, hakuna mtu ambaye anaweza kujisifu kuwa anaweza kuliko mtu mwingine. Dk Tulia amepata fursa kuonyesha uwezo wake na jambo la muhimu apewe muda tu. Namtakia kila la kheri katika majukumu yake mapya
MWANANCHI

No comments: