UTEUZI,PICHA NA WASIFU WA WAZIRI MKUU ....KASIM MAJALIWA..

Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania leoa limempitisha Mbunge wa Jimbo la Ruangwa, Mhe. Kassim Majaliwa kuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tano baada ya jina lake kupelekwa Bungeni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
Mhe. Majaliwa amepitishwa kwa kura 258 sawa na asilimia 73.5% ya kura zote za ndiyo.
Idadi ya wabunge ilikuwa ni 394, waliosajiliwa 369, na waliohudhuria Bunge ni 351. Apigiwa kura 258. Zilizoharibika ni 2, na kura za hapana zilikuwa 91.
Majaliwa (CCM) jina lake lilitajwa katika ukumbi wa Bunge - Dodoma na Spika wa bunge hilo, Job Ndugai aliyeahirisha kikao cha bunge kwa dakika 45 kwa ajili ya kuandaa utaratibu wa Bunge kuthibitisha jina hilo kwa kulipigia kura.
Bahasha iliyobeba jina la Waziri Mkuu iliwasilishwa na mpambe wa Rais katika ukumbi wa Bunge huku ikiwa imefungwa kwa bahasha tatu tofauti na ikiwa imeandikwa kwa mkono na Rais mwenyewe, hali inayoonesha usiri mkubwa wa kuzuia kuvuja kwa jina la mteuliwa kabla ya kutajwa bungeni.
Kassim Majaliwa alizaliwa Desemba 22, mwaka 1960 na kupata elimu katika Shule ya Msingi Mnacho kati ya mwaka 1970-1976 kabla ya kujiunga na shule ya sekondari ya Kigonsera kati ya mwaka 1977- 1980.
Mwaka 1991-1993 alijiunga na Chuo Cha Ualimu Mtwara (Mtwara TTC). Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1994 na kuhitimu mwaka 1998 kabla ya kujiunga na Chuo Kikuu cha Stockholm nchini Sweden kwa masomo ya juu.
Amehudumu katika nafasi mbalimbali tangu mwaka 1984 alipojiunga na utumishi wa umma kama mwalimu mkoani Lindi, Katibu wa Chama cha Waalimu Wilaya, Katibu chama waalimu Mkoa na Mkuu wa Wilaya.
Mwaka 2010 alichaguliwa kuwa mbunge wa jimbo la Ruangwa mkoani Lindi kabla ya Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete kumteua mwaka 2012 kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali ya Mitaa (TAMISEMI) anayeshughulikia elimu.
Kiongozi huyu pia mbali na kufanya kazi katika nafasi mbalimbali serikalini, alipitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika kambi ya Makutopora.
Waziri Mkuu Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Majaliwa Kassim Majaliwa, akitoka kwenye ukumbi wa bunge mjini dodoma jana mara baada ya kuthibitishwa uteuzi wake na bunge. (Picha: Francis Dande)
Waziri Mukuu Mteule, Majaliwa Kassim Majaliwa, akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuteuliwa na kuthibitishwa na bunge mjini Dodoma jana, ambapo anatarajiwa kuapishwa leo Ikulu ya Chamwino.
Waziri Mkuu Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Majaliwa Kassim Majaliwa, akitoka kwenye ukumbi wa bunge mjini dodoma jana mara baada ya kuthibitishwa uteuzi wake na bunge.
Waziri Mkuu Mteule akiwashukuru wabunge mara baada ya kumthibitisha.
No comments: