MAJALIWA ATAKA VIYOYOZI VITUO VYA MABASI YA DART
Katika ziara hiyo iliyochukua takriban saa tatu, Waziri Majaliwa alipita katika vituo vyote vilivyopo kwenye mradi huo, akitaka kujua ni wapi utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa, Novemba 27, mwaka huu ulipoishia.
“Tena ingekuwa vizuri kama vituo hivi vyote vingefungwa viyoyozi ili kuboresha mandhari pindi wanaposubiri usafiri,” alisema Wazri Mkuu Majaliwa kwenye ziara hiyo.
Akitoa maagizo yake alimwita mhandisi, Frank Mbilinyi kutoka Tanroads akimtaka ahakikishe vigae vilivyokuwepo kwenye kituo hicho vinabadilishwa kabla ya kuzinduliwa kwa mradi huo Januari 10 mwakani.
“Nilipokuja mara ya kwanza nakumbuka tulikubaliana kuwa vigae hivi havina ubora, hivyo naagiza viondolewe mara moja,” alisema.
Aliwataka kujenga uzio kwenye kituo cha Kivukoni kwa lengo la kulinda usalama wa abiria lakini pia miundombinu.
“Hakikisheni kunakuwa na uzio, nafikiri nyote mnakijua kituo cha mabasi cha Msamvu Morogoro, kina geti moja la kuingilia na moja la kutoka. Hivyo nafikiri ni vizuri kuiga mfano wao,” alifafanua.
“Enhe kuna vyoo?” aliuliza wakati akiendelea na ukaguzi huu kabla ya kujibiwa na Asteria Mlambo ofisa mtendaji mkuu wa Darts. Ndiyo vipo upande wa kule alisema huku akionyesha kwa mkono.
Agizo la tatu; aliwataka watendaji wa Halmashauri ya jiji la Dar es Salaam, wao kuhakikisha moshi unaotoka kwenye soko la samaki unadhibitiwa kwa kujengwa majiko ya kisasa kama walivyokubaliana awali.
“Ninyi watu wa jiji, hakikisheni mnafanya moja kati ya haya: kwanza ni kufunga majiko ya kisasa katika soko hilo na pili ni kuhamisha soko hili ili kunusuru afya za abiria na miundombinu ya mradi huu” alizungumza alielekeza hayo mbele ya Sarah Yohana Kaimu Mkurugenzi wa jiji.
Baada ya ukaguzi wa kituo hicho cha Kivukoni, alikwenda eneo la Jangwani kukagua karakana ya mabasi yatakayotumika katika mradi huo.
Karakana ilikuwa ina idadi ya mabasi yapatayo 140, yakijumuisha mabasi madogo na makubwa. Kwa mujibu wa Asteria Mlambo, mabasi makubwa yatakuwa yakitumia njia maalumu zilizojengwa na Darts, ambapo hata utaratibu wake wa ukatishaji tiketi ni tofauti na ule wa yale ya kawaida.
“Mabasi ya kawaida yatakuwa yakichukua abiria kutoka maeneo ya ndani na kuwaleta kwenye vituo vya mabasi yaendayo kasi” “utaratibu wa ukatishaji tiketi kwenye mbasi madogo ni kama huu wa kawaida uliozoeleka,” alisema.
Lakini kwa upande wa yale makubwa, utaratibu wa ukatishaji tiketi utakuwa ni ndani ya gari ambapo abiria atajihudumia mwenyewe. Pia atakuwa na uwezo wa kukata tiketi ya kutumia hata mwaka mzima kulingana na mahitaji yake.
Baada ya kutoka kwenye karakana msafara huo moja kwa moja ulifika Kimara, ambapo alipoingia tu, alipokewa na wakazi wa eneo hilo wakipaza sauti kuhusiana na tatizo la maji linalowakabili.
Hata hivyo Waziri Majaliwa alitoa ahadi kuwa angelitafutia ufumbuzi tatizo hilo, kabla ya kuto agizo la nne kwa watendaji wa Darts kuhakikisha kuwa vituo vyote vya mradi huo vinakamilisha ujenzi wa uzio , lakini pia kunakuwa na milango maalumu yenye uwezo wa kujifunga na kujifungua, ili kurahisisha huduma kwa abiria watakaokuwa wakitumia usafiri huo.
Waziri Mkuu Majaliwa katika agizo lake la tano aliwataka wadau wanaohusika na mfumo wa ukatishaji wa tiketi wahakikishe Serikali inanufaika na mradi huo.
Agizo la sita lilikwenda moja kwa moja wa wanasheria wa Tamisemi, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuhakikisha mikataba yote imekamilika.
“Fanyeni mapitio ya mikataba yote na uendeshaji wake na namna ya mfumo wa utendaji wake utakavyofanya kazi na kwa kuwa mtakutana kama Waziri Simbachawene (George), ni vyema mkahakikisha Serikali inalindwa,” alisisitiza.
Pia Waziri Majaliwa alitoa agizo lake la saba katika ziara yake akiitaka manispaa ya Kinondoni kuhakikisha inajenga eneo la maegesho, wakitafuta eneo hilo kwa gharama yoyote ile ili kuondoa tatizo la msongamano wa magari linalolikabili jiji la Dar es Salaam.
Alisema kuliko kuruhusu magari ishirini yaliyobeba watu ishirini, ni vyema watu hao wakaegesha magari yao kwenye maegesho yatakayojengwa katika eneo maalumu.
MWANANCHI

No comments: