RC KILANGO AANZA NA WATENDAJI WA USHETU
Kilango ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wakuu wa idara na madiwani wa halmashauri hiyo wakati wa ziara yake.
Mkuu huyo wa mkoa amesema hakuna sababu za msingi za ofisi za halmashauri hiyo kuendelea kuwa mjini Kahama wakati watendaji wanapaswa kutekeleza shughuli zao za kuwahudumia wananchi katika makao hayo ya Nyamilangano.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo, Isabela Chilumba amewatupia mzigo madiwani kuwa ndiyo waliokwamisha jitihada za kuhamia Nyamilangano.
Chilumba amesema licha ya eneo hilo kutokuwa na usalama wa kutosha wakihofu vifaa vya ofisi kuibiwa, pia madiwani wamekuwa kikwazo kwa halmashauri hiyo kuhama mapema.
“Mimi na wakuu wangu wa idara mbalimbali tulikubali kuhamia siku nyingi, hata tukiishi katika nyumba za kulala wageni ilimradi tuweze kuwatumikia wananchi wa Ushetu ila kuna changamoto mbalimbali,” amesema Chilumba.
Licha ya utetezi huo, Kilango amewahimiza madiwani na watumishi wa halmashauri hiyo kutekeleza agizo lake hilo kwa muda huo ili pia kupunguza kutumia gharama kubwa kwa kila siku kwenda mjini Kahama na kurudi kwenye makazi yao.
Kilango amesema halmashauri hiyo haiwezi kupiga hatua kama watendaji wake watakuwa wanaishi mbali na eneo lao la kazi.
Amewataka kukabiliana na changamoto za maendeleo katika eneo lao la kazi, huku wakiishi katika sehemu hiyo na kwamba, Watanzania wana kiu kubwa ya maendeleo ambayo yanatakiwa kusukumwa na watendaji walio karibu nao.
Akizungumza kwa sharti la kutotajwa jina lake, mmoja wa madiwani wa halmashauri hiyo amesema kauli ya mkurugenzi wao inalenga kuwachonganisha na mkuu wa mkoa kwa kuwa wako tayari kuhamia, lakini miundombinu inapaswa kuboreshwa zikiwamo ofisi, maji na sehemu za kufanyia vikao.
MWANANCHI

No comments: