AGNES MASOGANGE NA WENZAKO TUMIENI UJANA WENU VIZURI
KWAKO
Agness Gerald ‘Masogange’ pamoja na wenzako wengi ambao baadhi yao
nitawataja kwa majina hapo chini. Nawasalimu katika jina la Bwana, vipi
mko poa? Mnajionaje na hali? Mishe zenu zinakwenda kama kawaida?
Mkitaka kujua afya yangu, mimi
namshukuru Mungu. Naendelea vizuri. Nazidi kupambana ndani ya huu mjengo
mkubwa wa Magazeti Pendwa Tanzania, Global Publishers Ltd. Kazi yetu ni
ngumu kidogo, kila siku wasomaji wanataka habari mpya. Kuzitafuta si
kazi ya kitoto.
Dhumuni la kukuandikia barua
Masogange na wenzako leo ni moja tu, kutaka kuwakumbusha kwamba kuna
maisha baada ya ujana. Umaarufu mnaoupata kwenye mitandao, hauna maana
kama mnakuwa hamna shughuli ya kufanya.
Watanzania hawafurahishwi na
mnavyoposti picha zenye viashiria vya ngono na kuziweka mtandaoni.
Unajipiga picha ya nusu utupu, unaiweka mtandaoni ili iweje? Umekaa mkao
wa kuhamasisha ngono unataka kutafsirika vipi? Unajiuza? Kama ndiyo
biashara, kwa nini usitafute nyingine?
Mbona biashara zipo nyingi jamani.
Kupitia urembo wenu mbona kuna ishu kibao tu za kutengeneza fedha? Kuna
makampuni yanataka kufanya kazi na nyinyi kwenye matangazo yao, kuna
wasanii wanataka muwapambie video zao, yote hayo hamyaoni? Njia pekee ya
kuishi ni hiyo mliyoichagua?
Wiki iliyopita niliona moja kati ya
habari iliyopamba magazeti ya Global ni ile ya mtindo mpya wa mastaa
kujiuza. Kwamba siku hizi taarifa zinaeleza kwamba wengi wenu mnapoweka
picha kwenye mtandao wa Instagram, mnapata dili nchi za nje.
Hii ni aibu. Kweli warembo wa
Tanzania mmefika hapa? Yaani biashara inafanyika mtandaoni, mnasafiri
kwenda nchi za watu kweli? Sikushtuka sana nilipoona ile habari maana
Masogange wewe na wenzako mmekuwa mkisafiri pasipo kueleweka
kinachowasafirisha.
Utasikia tu Masogange yupo Sauz,
sijui Gigy Money yupo wapi mara sijui Kidoa alikwenda kufanya shopping
Dubai na kurudi, mnakwenda kule kwa kipato gani? Kazi gani
zinazowaingizia kipato hadi muende kule kufanya shopping?
Niliwahi kuzungumza na wewe Masogane
siku moja katika Global TV Online. Nilikubana maswali kuhusu kazi
inayokufanya uishi mjini, hukuwa na jibu la kueleweka. Bado pia ulisema
wasanii hawawalipi vizuri pindi mnapotumika katika video zao.
Hiyo ilitosha kunifanya mimi nikuone
kwamba unahitaji kubadilika. Unahitaji kutafuta kazi ya kufanya kuliko
kuishi kimjinimjini. Mbona unaonekana unaweza hata kuigiza, kwa nini
usiigize? Unafikiri aina ya maisha unayokwenda nayo itadumu hadi lini?
Mimi nakushauri kama kaka yako,
badilika. Wenzako pia wenye kamchezo kama ka kwako nao pia nawaambia
wabadilike ili na wao wafanye kazi, waache kuweka picha za nusu utupu
mitandaoni.
Ni matumaini yangu wewe pamoja na wenzako wote wanaofanya mambo hayo watabadilika mara moja maana si ungwana.

No comments: