MAMBO SITA YA KUTAFAKARI SIKUKUU YA KRIMASI
Mambo hayo ni pamoja na kupinga mgawanyiko na kujali usawa wa makundi katika jamii, kuhimiza maadili ya viongozi na jamii, kuepuka utamaduni wa kutofanya kazi, kujali usalama wa raia, kutazama aina ya siasa zinazofanyika nchini, amani na kuunga mkono juhudi za Rais John Magufuli.
Mambo hayo ndiyo ambayo wachambuzi hao wanatazamia yawe ajenda kuu za viongozi wa dini na mjadala katika maadhimisho ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo leo.
“Kipindi hiki tujadili jinsi gani tutakuwa na Taifa lisilo na mpasuko wa kidini, kusiwe na dini inayojiona ni bora kuliko dini nyingine,” alisema mwenyekiti wa Mtandao wa Wanawake na Katiba Tanzania, Profesa Ruth Meena alipoulizwa na Mwananchi kuhusu matarajio yake kwa viongozi wa dini leo.
“Kusiwe na ukandamizaji na kupokonya haki za wengine. Tujadili uhuru wa mawazo tunaoutaka, jinsi ya kuweka misingi ya haki za binadamu, tunajadili wote na dini zote, hata asiyesherehekea.”
Pamoja na kuungana na Profesa Meena, Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es Salaam (Duce), Dk Luka Mkonongwa alizungumzia umuhimu wa kujenga utamaduni wa kufanya kazi kwa bidii ili kuepuka athari za kubana matumizi zilizotokea mwaka huu.
Mapema mwaka huu, Rais Magufuli alianzisha utaratibu wa kubana matumizi unaolalamikiwa kuwa umesababisha fedha kupotea mifukoni na katika mzunguko, huku Serikali ikisisitiza kuwa hizo ni athari za muda mfupi.
Dk Mkonongwa alisema Krismasi ni siku muhimu ya Watanzania kutafakari na kusahau tofauti zao na uwezekano wa kutokea migogoro ya kisiasa.
Lakini Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Lilian Liundi alisema tofauti baina ya makundi ya kijamii, hasa za kijinsia, zimeongezeka na hivyo jamii inatakiwa kutafakari namna ya kuiepuka.
Liundi, huku akiomba jamii iongeze nguvu katika vita ya ukatili dhidi ya mwanamke, alipendekeza uwepo mjadala wa kitaifa kuhusu hali ya ukatili na usawa wa kushiriki katika nafasi za uongozi.
Mwanaharakati huyo aliungana na Dk Mkonongwa kuwa Watanzania wanatakiwa kujadili utamaduni wa kufanya kazi ili kuepuka athari za ukali wa maisha unaotokana na kubana matumizi.
“Tusigombanie fito, tutafakari na kujenga nchi yenye uchumi imara,” alisema Mkonongwa.
Msomi huyo, aliyepongeza juhudi za Rais Magufuli kusafisha Serikali kwa mtindo wa utumbuaji, alisema ni vyema Watanzania wakamuunga mkono na kutafakari jinsi gani wanaweza kushiriki katika safari yake ya kurejesha maadili na kuondoa urasimu kwa viongozi wa umma.
Suala hilo la maadili kwa viongozi wa umma lilichukua nafasi kwenye mjadala wa wachambuzi hao, hasa kwa jinsi Rais Magufuli alivyorekebisha nidhamu ya watumishi na viongozi kwa kuwasimamisha au kuwatimua zaidi watumishi 100.
Ili kulinda uhusiano katika jamii, Rais wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Tarcisius Ngalalekumtwa alisema Watanzania wanatakiwa kuwa wakweli.
“Ujumbe wangu kwa Watanzania wote ni kwamba, tuwe wakweli, tutende haki na tuwe na huruma kwa wenzetu kama ambavyo Mungu amekuwa na huruma katika maisha yetu,” alisema askofu huyo wa Jimbo Katoliki la Iringa.
MWANANCHI

No comments: