SUMAYE, WARIOBA WAKOLEZA MOTO MAKINIKIA
Mawaziri wakuu wawili wa zamani, Jaji Joseph Warioba na Frederick Sumaye wamejitosa katika sakata la mchanga wa madini, wakiwa na maoni tofauti.
Wakati Jaji Warioba akitaka nchi iachane na kufikiria kuwachukulia hatua waliohusika na badala yake kurekebisha sheria na mikataba, Sumaye amesema kama hakutakuwa na ushahidi wa tuhuma kwamba Acacia inaiba, mazungumzo baina ya kampuni hiyo na Serikali hayatakuwa na manufaa.
Wawili hao walizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti kuhusu sakata hilo baada ya kamati mbili zilizoundwa na Rais John Magufuli kuchunguza kiwango cha madini kilichomo katika makontena 277 yaliyozuiwa bandarini na athari za kiuchumi, kuibuka na majibu yanayoonyesha Acacia ilitoa taarifa za uongo, haijasajiliwa nchini na hailipi kodi ipasavyo.
Ripoti ya kamati ya kwanza iliyoongozwa na Profesa Abdulkarim Mruma ilibaini kuwa kiwango cha madini kilichomo katika mchanga huo ni mara kumi zaidi ya kile kilichotangazwa na Acacia.
Kamati ya pili iliyoongozwa na Profesa Nehemia Osoro ilibaini Tanzania kupata hasara ya zaidi ya Sh108 trilioni katika kipindi cha takriban miaka 20 ambayo Acacia imekuwa ikisafirisha mchanga nje.
Acacia haijakubaliana na taarifa zote mbili na inataka uchunguzi huru.
Taarifa hizo zimewafanya wananchi wapaze sauti wakitaka wote waliohusika, bila kujali nyadhifa zao, wawajibishwe.
Lakini, Jaji Warioba aliiambia Mwananchi jana kuwa kuendelea kujadili waliohusika ni kupoteza muda na ametaka wananchi waanze kujadili mambo yatakayolivusha Taifa kutoka pale ilipokwama.
“Hawa si malaika, ni watu na kuna maeneo walikosea sasa isiwe sababu ya kuanza kunyoosheana vidole kwa kushabikia mapungufu yao,” alisema Jaji Warioba.
“Hebu tuangalie njia bora zaidi ya kusahihisha makosa yao kwa kuweka mipango itakayotupeleka mbele.”
Jaji Warioba, ambaye alikuwa waziri mkuu wakati wa utawala wa Rais wa Awamu ya Pili, alisema haoni sababu za msingi za watu kujadili majina badala ya kuelekeza nguvu katika kutafuta suluhisho na kubuni mikakati itakayosaidia Taifa, hasa wakati huu linapoanzisha majadiliano na wawekezaji wa kigeni kuhusu rasilimali.
Alisema wakati mwingine mjadala huo unakolezwa na vyombo vya habari vinavyotumia muda mwingi kuweka picha za watu.
Bila kuwataja watu hao, mbobezi huyo wa sheria alisema kinachopaswa sasa ni kuanza kujenga hoja zitakazosaidia kutungwa sera na sheria mpya ambazo zitalinda rasilimali zote za Taifa na si kuanza kuhoji nani alifanya nini na alikosea wapi.
Alisema hata kama ikatokea watu wote wakafungwa, bado haitasaidia lolote na kwamba cha msingi ni kutambua kuwa sakata la makinikia limesaidia kuibua mapungufu yaliyokuwepo katika sekta ya madini.
“Mimi naona tunapaswa kuanza kujadili njia bora zaidi za kufanya. Sheria na kanuni zetu zinatoa usawa kwa pande zote yaani wawekezaji na Taifa,” alisema.
Alisema kama viongozi, kuna mambo walikosea na mengine walifanya vizuri, hivyo kama Taifa linapaswa kujifunza katika yale yaliyokosewa ili kusonga mbele.
Alisema hata kama hoja ni kutaka kuwawajibisha viongozi hao, lazima ionyeshe wazi ni wapi walikosea na walikoseaje na si kushabikia mambo ambayo hayawezi kuendeleza rasilimali za Taifa.
“Nadhani sasa mjadala ujikite kuangalia vipi sera zetu zilivyo, sheria nayo imekaaje, kanuni zetu zinasemaje ili hatimaye tuje na mawazo ya kuziboresha,” alisema.
Alisema binafsi amefurahishwa na majadiliano yanayotegemewa kuanza kati ya Serikali na kampuni ya Barrick, ambayo inamiliki asilimia 64 ya hisa za Acacia, akisema yatasaidia kuweka daraja litakalonufaisha pande zote.
“Kwa vile wamekubali kuanza kujadiliana, tuwaache na tuwaamini kwamba mwisho wa majadiliano yao jambo jema litazaliwa. Kwa sasa tusubiri kwanza,” alisema.
Kamati ya pili ilipendekeza wote waliohusika na sheria na mikataba hiyo wawajibishwe, wakiwemo mawaziri, wanasheria wakuu na watendaji wengine.
Ripoti ya kamati ya kwanza ilisababisha Rais Magufuli amtimue aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ambaye mkuu huyo wa nchi aliwahi kuwaeleza wananchi kuwa ni mchapakazi.
Profesa Muhongo alivuliwa uwaziri kutokana na kutowajibika ipasavyo. Rais Magufuli alitoa agizo la kwanza la kuzuia mchanga kusafirishwa nje mwaka jana, lakini ukaendelea hadi alipotangaza tena Machi mwaka huu na kuunda kamati hizo mbili.
Rais pia alimsimamisha kazi ofisa mtendaji mkuu wa Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) na kuvunja bodi ya taasisi hiyo, huku akitaka wafanyakazi wa Wizara ya Madini na Mamlaka ya Mapato wachunguzwe.
Sumaye alonga
Wakati Warioba akisisitiza kutojadiliwa kwa majina katika sakata hilo, Sumaye amesema kamati mbili zilizochunguza sakata la mchanga wa madini ni tofauti na nyingine zote zilizoundwa hapo kabla, ikiwemo aliyoiunda mwaka 2004.
Lakini akasema katika kutafuta njia za kuzuia wizi wa kampuni za madini, aliwahi kuomba ushauri kwa Rais wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki ambaye alimwambia ni kazi ngumu.
“Ni ngumu kuwazuia watu hawa wasiibe ila mnaweza kupunguza wizi huo,” alisema akinunuu ushauri aliopewa na Mbeki.
Sumaye, ambaye ni waziri mkuu pekee hadi sasa aliyefanya kazi hiyo kwa miaka kumi mfululizo, aliunda kamati iliyoongozwa na Dk Jonas Kipokora mwaka huo ikiwa ni ya pili katika mfululizo wa zilizoundwa kuchunguza sekta ya madini.
Ilitanguliwa na kamati iliyoongozwa na Jenerali Robert Mboma iliyoundwa na Rais wa Serikali ya Awamu ya tatu, Benjamin Mkapa mwaka 2002.
Alisema kabla hajaunda kamati hiyo alilazimika kuomba ushauri kwa Mbeki, ambaye alisema kwake alikuwa ni mtu sahihi kwa ushauri kutokana na Afrika Kusini ilivyopiga hatua katika uchimbaji madini.
“Wekeni wakaguzi kupunguza wizi,” alisema Sumaye akikariri ushauri wa Mbeki.
“Hatukuwa na uzoefu. Mpaka muda huo tulikuwa tunachimba almasi zaidi. Tulihitaji kufahamu mengi zaidi.”
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ya Chadema alisema kutokana na muda kutoruhusu hakuifanyia kazi ripoti hiyo, aliimkabidhi kwa mrithi wake.
Sumaye alikuwa Waziri Mkuu kuanzia mwaka 1995 hadi 2005 na alifuatiwa na Edward Lowassa aliyeshika wadhifa huo kwa takriban miaka miwili kabla ya kujiuzulu kutokana na sakata la mkataba wa Richmond.
Akizungumzia mazungumzo yanayosubiriwa kati ya Serikali na uongozi wa kampuni ya Barrick ya Canada, Sumaye alisema kama hakutakuwa na ushahidi wa kutosha kuthibitisha kwamba wawekezaji hao wameiibia Tanzania, hakuna cha maana kitakachopatikana kwa wawekezaji hao hufuata sheria na mkataba.
“Kwa hiyo, mazungumzo hayo yatalenga kuboresha maslahi ya mkataba uliopo,” alisema Sumaye.
MWANANCHI

No comments: