AJIRA ZINGINE MPYA ZAMWAGWA SERIKALINI
Serikali imetangaza kuajiri walimu 381 wa Sayansi na Hisabati kwa awamu ya pili kwa ajili ya shule za sekondari.
idha, imeonya walimu watakaopokea posho za kujikimu, lakini wasiripoti kuanza kazi katika vituo walivyopangiwa watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza jana na waandishi wa habari mjini hapa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene, alisema awamu hiyo pia inajumuisha mafundi sanifu wa maabara 137 kwa ajili ya shule hizo.
Alifafanua kuwa ajira hizo zimetokana na tangazo la nafasi ya kazi lililotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia miezi mitatu iliyopita.
Simbachawene alisema katika tangazo hilo la Aprili kilitolewa kibali cha kuajiri walimu 4,129, lakini walimu 3,081 ndio walioweza kupatikana kwa awamu ya kwanza.
Alisema bado nchi inahitaji kuajiri walimu 1,048 waliosalia, hivyo baada ya uhakiki wa vyeti katika awamu ya pili kwa wahitimu wa mwaka 2015 kurudi nyuma wamepatikana walimu 381 na mafundi 137.
Aidha, alisema katika kibali hicho bado kuna mahitaji ya walimu 530.
“Walimu hawa wamechaguliwa na hatimaye kupangiwa vituo vya kazi na watatakiwa kuripoti katika Ofisi za wakurugenzi wa halmashauri zilizopo shule walizopangiwa, na wanatakiwa kuripoti kuanzia Julai 17 hadi 31 mwaka huu,” alisema Simbachawene.
“Maombi yaliletwa mengi, lakini katika mchujo huo kutokana na vigezo mbalimbali, ikiwamo wawe ni wahitimu wa mwaka 2015 kurudi nyuma, hawajaajiriwa, kwa tatizo la vyeti na wengine pia umri.”
Alisisitiza vituo vyao vya kazi ni shule za sekondari walizopangiwa walimu hao na si makao makuu ya halmashauri.
Aliwataka wakurugenzi wa halmashauri ambazo walimu hao wataripoti kuwapokea kwa kuzingatia taratibu na kanuni zote za utumishi.
Simbachawene alisema kwa upande wa walimu wa masomo ya sanaa bado kuna ziada ya walimu zaidi ya 7,000 hivyo kwa sasa hawataajiriwa.
Hata hivyo, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, ililiambia Bunge mjini Dodoma Mei 13, mwaka huu kuwa imebaini upungufu wa walimu 182,899 wa shule za msingi na 69,794 wa shule za sekondari.
Kamati ilikuwa ikitoa taarifa yake kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi kwa mwaka wa fedha 2016/17 na makadirio ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka huu wa fedha.
SIKU 10
Kutangazwa kwa ajira hizo kunakuja siku 10 tangu Serikali kusema inatarajia kutoa vibali 3,000 vya ajira katika sekta ya afya, zikihusisha madaktari na wauguzi kwa ajili ya vituo vya afya vya kata ili kuboresha sekta hiyo.
Aidha, serikali ilitangaza kuwa itatoa vibali vya ajira za maofisa hesabu 535 kwa ajili ya vituo vya afya na zahanati nchini ili kushughulikia ipasavyo ukusanyaji wa mapato.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Laurean Ndumbaro, ndiye aliyetangaza neema hiyo kwa wasomi wanaosubiri ajira serikalini Julai 3, wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha waganga wakuu wa mikoa na wilaya kuhusu maadili na uwajibikaji mahali pa kazi.
Aidha, ajira hizo zinakuja baada ya Serikali kuwachukua madaktari 258 ambao walisailiwa kwa ajili ya kwenda kufanya kazi Kenya, lakini mpango huo ukasitishwa na mahakama ya huko.
Katika mwaka huu wa fedha, serikali imeahidi kutoa vibali vya ajira za moja kwa moja 52,436 katika sekta zake mbalimbali.
NIPASHE

No comments: