NI KIWEWE.. VIGOGO KORTINI
Chanzo kimoja kilicho karibu na mamlaka za kiuchunguzi na pia mahakama, kimeiambia Nipashe kuwa kuanzia kesho Jumatatu, upo uwezekano mkubwa wa kuwapo kwa msururu wa vigogo wanaokabiliwa na tuhuma mbalimbali kufikishwa kortini.
Inadaiwa kuwa hali hiyo inatokana na kile kinachoelezwa kuwa wengi wao, tayari majalada yao yalishafanyiwa kazi na mamlaka za uchunguzi na kisheria hivyo, kilichobaki ni kwa wote kufikishwa mahakamani ili sheria itwae mkondo wake.
Ofisi za Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) na pia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), zinatajwa kuwa zimekamilisha kazi zao kuhusiana na uchunguzi wa baadhi ya tuhuma na sasa, hatua inayofuata ni kuwafikisha wahusika mahakamani.
Katika siku takribani 10 zilizopita, Takukuru iliwafikisha kortini vigogo kadhaa kutokana na tuhuma za makosa mbalimbali, baadhi yao wakiwa viongozi wa juu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu (TFF), viongozi wa klabu ya soka ya Simba na wafanyabiashara wakubwa wawili, Harbinder Singh Sethi na James Rugemalira. Watu wote hao kwa sasa wako katika mahabusu kwenye gereza la Keko, Dar es Salaam.
“Kuna uchunguzi wa masuala kadhaa ambao ulishakamilika …DCI, Takukuru na DPP wameshamaliza kila kitu kuhusiana na majalada yanayohusiana na mashtaka na hivyo kilichobaki ni kuwafikisha wahusika kortini,” chanzo kiliiambia Nipashe, bila kutaja majina ya watuhumiwa ingawa kilisisitiza kuwa ni kesi zinazohusisha upotevu wa fedha nyingi za umma.
“Kwa kawaida, uchunguzi ukikamilika majalada hufikishwa kwa DPP…sasa kwa baadhi ya watuhumiwa kila kitu kimefanyika, yaani hata DPP ameyapitia na kuridhia kuwa mchakato wa kuwafikisha mahakamani uendelee. Na hili ndilo linalowatia kiwewe baadhi ya watu kwa sababu hizi siyo kesi ndogo,” chanzo kiliongeza.
Hadi kufikia jana jioni, Nipashe haikuweza kupata taarifa rasmi kuhusiana na suala hilo kutoka ofisi ya DPP wala DCI. Hata hivyo, Msemaji na Ofisa Uhusiano wa Takukuru, Mussa Misalaba, aliwahi kuiambia Nipashe katikati ya wiki kuwa wao wanaendelea na kazi yao ya uchunguzi na kila mara wanapokamilisha taratibu zao, huwafikisha watuhumiwa kortini pale inapobidi.
Tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani Novemba 5, 2017, vita dhidi ya vitendo vya rushwa na ufisadi imeendelea kushika kasi hasa baada ya Rais John Magufuli, kutangaza wazi kuwa kamwe hatakuwa na simile dhidi ya watu wanaojihusisha na vitendo hivyo, lengo likiwa ni kuona kuwa fedha za umma zinawafikia moja kwa moja wananchi kwa kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo na pia kufanikisha malengo kadhaa yakiwamo ya utoaji wa elimu bure, ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge), miradi ya ujenzi wa barabara za juu (fly-overs); ununuzi wa ndege; ujenzi wa barabara na pia uimarishwaji wa huduma za afya
NIPASHE

No comments: