Header Ads

Blogger Tips and TricksLatest Tips And TricksBlogger Tricks

WAZIRI WA JK AFICHUA SIRI YA UPIGAJI MOGODI


Aliyekuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini katika serikali ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete StephenMasele,amefichua kuwa udhaifu katika eneo la utafiti ni sababu mojawapo iliyofanikisha upigaji uliogharibu taifa mabilioni ya shilingi kupitia mikataba mibovu ya madini

Masele alifichua ukweli huo juzi mjini Dodoma katika mahojiano maalumu ikiwa muda mfupi baada ya kupitishwa kwa kishindo miswada mitatu inayohusiana na rasilimali za nchi kwa manufaa ya taifa.

Aidha, Masele ambaye ni Mbunge wa Shinyanga Mjini CCM), alisema kupitishwa kwa miswada hiyo kutaiwezesha serikali kudhibiti kwa karibu zaidi sekta ya madini na kuzuia upotevu wa mapato, hasa katika hatua ya utafiti ambayo ndiyo chimbuko la hasara iliyopatikana kwa taifa.

Miswada iliyopitishwa na Bunge kwa dharura ni Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Nchi Kuhusiana na Umiliki wa Maliasili, Muswada wa Sheria ya Mapitio na Majadiliano Kuhusu Masharti Hasi katika Mikataba ya Maliasili za nchi na Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali, ikiwamo Sheria ya Madini.

Akieleza zaidi, Masele alisema kuna mauzo mengi ya leseni za utafiti yamefanyika bila serikali kuwa na taarifa kamili wala mapato kutokana na uuzaji huo.

“Kwenye leseni hizo serikali haikuweza kupata taarifa kamili za nani kamuuzia nani; kwa kiasi gani cha fedha na serikali imepata nini,” alisema Masele ambaye alikuwa Naibu Waziri wa Nishati na Madini na baadaye nafasi hiyo hiyo Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira).Alitumikia nafasi hizo kati ya Mei, 2012 na Oktoba, 2015.

Alibainisha kutokana na marekebisho hayo, serikali sasa itaanza kudhibiti kwa ukaribu zaidi hasa hatua ya utafiti kwa kuwa kumekuwa na mwanya mkubwa wa upotevu wa mapato kwenye eneo hilo.

“Kuna watu wengi wanadhani madini unaanza kuweka usimamizi mkubwa wakati wa kuchimba. Wakati wa utafiti pia ni eneo ambalo sheria ilikuwa ipo kimya na kuacha wawekezaji kuweza kuuza leseni," alisema Mbunge huyo ambaye alikuwa naibu waziri katika awamu ya Rais wa nne, Jakaya 'JK' Kikwete.

“Mtu anamiliki leseni ya utafiti, anachimba mashimo mawili matatu ya utafiti baadaye anaiuza kwa mtu mwingine.

"Mauzo yale, zile fedha serikali haipati chochote, haina umiliki wa hisa yoyote, lakini hata usimamizi wake unakuwa sio mkubwa sana.”

Mbunge huyo alisema kwa marekebisho yaliyofanyika sasa bungeni umiliki wa serikali unaanzia kwenye utafiti.

“Kwa hiyo serikali itaanza kujua kila kinachoendelea lakini pia kwenye gharama za utafiti unaweza kudhibiti kwa sababu kwenye mtindo wa kampuni, unapojaribu kutafuta unafuu, wanaweza kuongeza gharama za utafiti ambazo zinaweza kuwa na madhara kwenye ulipaji wa kodi baadaye.

“Kwa sheria hii sasa utaweza kujua gharama halisi (kwa sababu) mtu hawezi kudanganya kwenye gharama ambazo ametumia.

"Ni eneo muhimu kwa serikali ambapo mabadiliko haya yameweka usimamizi mkubwa.”

Aidha, Masele alisema marekebisho yaliyofanyika kwenye miswada hiyo yanalenga kuziba mianya ambayo huko nyuma iliachwa na ukosefu wa nguvu ya kisheria.

“Kwa mfano sheria ya mwaka 2010 ilikuwa inaruhusu serikali kumiliki shughuli za uchimbaji, lakini marekebisho haya sasa unaona kabisa kwamba imeelekeza serikali ianze kuwa na hisa katika makampuni ya asilimia 16 kama kiwango cha chini na inaweza kuendelea kuongezwa hadi hisa asilimia 50.

“Hivyo mabadiliko haya yameeleza kabisa tunaanzia hapo, lakini ile ya mwanzo ilikuwa ipo kimya... ilikuwa inasubiri majadiliano kati ya serikali na mwekezaji.”

Kuhusu umiliki wa leseni, Masele alisema muswada huo uliopitisha sasa leseni ambazo zimeshindwa kutimiziwa masharti yake na watu wanaozimiliki wakiwamo wawekezaji wa ndani au wa nje zitarudi zote serikalini na zitamilikiwa na serikali.

“Hivyo mwekezaji yeyote mpya awe wa ndani au wa kigeni akitaka kumiliki eneo hilo itabidi awe na ubia na serikali kwa maana ya kwamba serikali itamiliki leseni kwa pamoja na yeye,” alisema Mbunge huyo.

YA MWISHO
Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi alisema mikataba iliyopo ya madini haitavunjwa licha ya mabadiliko ya kisheria yaliyopitishwa na Bunge mjini hapa.

Badala yake, alisema Waziri Prof. Kabudi, mikataba hiyo iliyopo ni ya mwisho kwani kuanzia sasa wawekezaji wataokuja katika sekta hiyo watatumia leseni.

Akihitimisha hoja ya mjadala wa Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Sheria Mbalimbali ya mwaka 2017 Jumatano, Waziri Kabudi alisema sheria hiyo mpya ikisainiwa na Rais John Magufuli itabadilisha mfumo uliopo kutoka mikataba kwenda leseni.

Aidha, alisema waziri huyo, Serikali itafanya marejeo ya mikataba hiyo iliyopo na kwamba taarifa ya mapitio hayo itatolewa kwa Bunge.

Rais Magufuli alimwagiza Waziri Kabudi katikati ya mwezi uliopita kupeleka muswada wa marekebisho ya sheria zote za madini kwa hati ya dharura.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo baada ya kamati maalumu ya kuchunguza masuala ya kisheria na kiuchumi kuhusiana na makinikia yanayosafirishwa nje ya nchi na kampuni ya Acacia kuwasilisha ripoti yake Ikulu jijini Dar es Salaam.

Kamati hiyo ya watu nane iliyokuwa chini ya Profesa Nehemiah Osoro ilisema nchi inaweza kuwa imepoteza mpaka Sh. trilioni 489 katika kodi na mali (madini) kwa miaka 19 iliyopita kwenye biashara hiyo ya madini inayofanywa na Acacia.

Kati ya fedha hizo, kiwango cha kodi kilitajwa kuwa Sh. trilioni 108.

Aidha, kamati ya Prof. Osoro ilitoa mapendekezo 21, ikiwamo kutaka mabadiliko ya sheria ili kuiwezesha nchi kupata mapato na kuacha kuibiwa kama ilivyo sasa.

Rais alisema ni vyema hata Bunge lililokuwa likiendelea la Bajeti likaongeza muda wake ili kujadili sheria hizo, ikiwamo mikataba kupitiwa upya na kumwagiza waziri kubaini sheria mbovu ili zifanyiwe marekebisho.

Bunge liliongeza muda wake kwa siku tatu kabla ya kuahirishwa Jumatano.

NIPASHE

No comments: