Header Ads

Blogger Tips and TricksLatest Tips And TricksBlogger Tricks

WAPINZANI WASIJIFARIJI KUWA WANAOHAMA WANANUNULIWA, INABIDI WAJITAFAKARI





Siasa Jamii (Community Politics) ni mtindo bora wa kisiasa ambao naamini ukitumiwa na chama chochote hauwezi kukiangusha, zaidi hurahisisha matokeo kwenye kata, majimbo na wilaya, kisha kuikuza taasisi ndani ya maisha ya watu na kwa urafiki mkubwa.


Asili ya Siasa Jamii ni baada ya Uchaguzi Mkuu wa Uingereza mwaka 1987, pale vyama washirika vya Social Democratic Party (SDP) na Liberal Party (LP) vilipoamua kuachana na mfumo wa kushirikiana kwenye uchaguzi ili kuunda chama kimoja.


Kuanzia mwaka 1981, SDP ambacho kilikuwa chama kilichoanzishwa na watu waliojitenga na Chama cha Labour, kilianzisha ushirikiano na LP wa kushiriki uchaguzi kama timu moja. Umoja wao uliitwa SDP-Liberal Alliance na utambulisho wao ulikuwa ni siasa za mrengo wa kati.


Mwaka 1988, SDP-Liberal Alliance walivunja vyama vyao na kuunda chama kimoja cha Liberal Democracy ambacho kilianza kujijengea umaarufu kwa mtindo wa Siasa Jamii. Siasa shirikishi zenye kukifanya chama kishiriki moja kwa moja kwenye maisha ya watu na jamii zao.


Ni mtindo huo wa Siasa Jamii ambao ulikiwezesha Liberal Democracy kujiongezea umaarufu na kukubalika katikati ya vyama vikubwa na vikongwe, Labour na Conservative. Mtindo huo ukakifanya Liberal Democracy kuongeza idadi ya wabunge kutoka uchaguzi mmoja kwenda mwingine.


Kutoka kushinda majimbo 20 kwenye Uchaguzi Mkuu 1992 mpaka kufikisha viti 62 vya ubunge katika Uchaguzi Mkuu 2005. Hii inaonyesha mantiki ya kuvifanya vyama vya siasa viishi na maisha ya watu. Jamii katika maisha yao ya kila siku, ivione vyama vinaishi navyo na si kusubiri nyakati za uchaguzi kuomba kura.




Siasa Jamii ni nini?


Ni siasa shirikishi, kwamba badala ya kutoa maagizo au kuyasemea matatizo, chama kinaziona changamoto kwenye maisha ya watu na kushirikiana na wanajamii kuzitatua. Chama hakisemi mitaro ya kupitisha maji machafu imeziba, bali kinachukua hatua za kushirikiana na wanajamii kuizibua.


Chama hakisemi jamii fulani watu hawana maji safi na salama, badala yake kinaangalia mbinu mahsusi za kuiwezesha jamii husika kupata maji. Chama hakipazi sauti kuwa hospitalini hakuna damu, kinyume chake kinahamasisha utoaji wa damu, huku viongozi wakionyesha mfano wa kujitolea damu.


Mtindo huo husababisha jamii zikione chama cha siasa kikiwa kwenye milangoni yao. Kinakuwepo kutunza mazingira, kinashiriki kutatua matatizo ya watoto ili kukihakikishia kizazi kipya elimu bora. Kinahamasisha uchumi kwa kuwaweka watu kwenye vikundi na kuwakutanisha na taasisi za kifedha ili kuwezesha upatikanaji wa mikopo.


Mfano mmojawapo wa Siasa Jamii ni Desemba 9, 2015, Rais John Magufuli alipoagiza siku hiyo kutumika kufanya usafi ili kuadhimisha Uhuru wa Tanganyika kwa kuiweka nchi ikiwa safi. Viongozi mbalimbali walijitokeza kushirikiana na jamii zao kusafisha maeneo wanayoishi. Rais Magufuli alijumuika na wavuvi wa Magogoni kufanya usafi. Hizo ndizo Siasa Jamii.


Kinyume cha Siasa Jamii ni Siasa Maelekezo au unaweza kuziita Siasa za Rimoti (non-community politics). Chama cha upinzani kinasema vitu bila kupiga hatua japo moja ya kuonyesha njia ya kushiriki kutatua. Jambo la kuhamasisha wananchi au kushirikiana bao kutatua, mbunge analalamika bungeni.


Tatizo ambalo linahitaji diwani kukaa vizuri na wananchi wa kata yake na kushirikiana nao kijamii kulipatia ufumbuzi, anakwenda kulalamika kwenye vikao vya halmashauri ili zitengwe fedha. Hizo ndizo siasa za rimoti au siasa za kupiga domo na kulalamika.


Mathalan, watu wanatupa takataka kwenye mitaro mpaka inafurika uchafu, suluhu si halmashauri kutenga fedha na kuajiri watu wa kusafisha, bali ni kuzielimisha jamii husika kisha kushirikiana nazo kufanya usafi, baada ya hapo watakuwa mabalozi wa kuonyana na kusimamiana wasichafue mitaro.


Vyama vidogo vina nafasi kubwa ya kuchomoza kisiasa na kuingia kwenye mioyo ya watu. Liberal Democracy kilifanikiwa Uingereza katikati ya vyama vikubwa na vikongwe, Labour na Conservative. Hata ACT-Wazalendo, Chaumma, ADC na vingine vinaweza kupata matokeo mbele ya CCM, Chadema na CUF.




Siasa Jamii ndani ya vyama


Maisha ya wanachama ndani ya chama ni aina nyingine ya Siasa Jamii. Viongozi wanavyoishi na mazungumzo yao. Namna kila mwanachama anavyoshirikishwa kujenga chama au jinsi baadhi ya watu wanavyoonekana kuwa bora na kujenga matabaka ndani ya taasisi.


Je, viongozi wa juu wanawashirikisha ipasavyo wanachama wa vyama wanavyoviongoza? Kauli ya kiongozi inafanana kweli na tamko la chama au ni mawazo yake binafsi? Chama ambacho kiongozi wake anatoa uamuzi unaopingwa au kunung’unikiwa na wanachama wengi, maana yake hakiishi katika msingi wa kijamii.


Chama cha siasa hutoka Taifa palipo na makao makuu mpaka kwenye matawi. Muundo huo kwamba chama kinakuwa na shina mpaka matawi, msingi wake ni lazima kiishi kijamii. Ni dhambi kubwa kuwa na uamuzi ngazi ya Taifa ambao matawi hayakubaliani nao.


Kusherehesha hili, Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, anaweza kunisaidia vizuri sana, kupitia andiko lake la Tujisahihishe, aliloandika Mei 1962, alipokuwa Rais wa chama cha Tanganyika African National Union (Tanu). Aliandika kuwa umoja wa watu unavyofanya kazi ni sawa na umoja wa viungo vya binadamu.


Mwalimu Nyerere alisema kuwa binadamu hawezi kuwa sawa kama kiungo kimoja au viungo kadhaa havipo sawa. Kwamba ili mwili wa binadamu uwe sawa na kutii kanuni za kimwili, lazima kila kiungo kiwe katika ukamilifu wake. Alikusudia kufikisha ujumbe kuwa Tanu kama umoja wa watu ni lazima kila mtu atii kanuni ya umoja.


Ndani ya Tujisahihishe, Mwalimu Nyerere alitaja mambo kadhaa ambayo husababisha anguko la umoja wowote. Nikiyaeleza hayo kwa lugha sahihi kulingana na wakati uliopo, jambo la kwanza alisema ni ubinafsi. Watu wakiwa wabinafsi umoja hautadumu kwa mafanikio. Lingine ni unafiki.


Tafsiri ya unafiki ni pana; upendeleo, woga, kutoambiana ukweli na kuangaliana usoni. Mwalimu Nyerere aliifafanua tabia hii: “Wengine hugawa watu kwa mafungu. ‘Fulani’ japo akifanya kosa kubwa sana halisemwi. Lakini ‘fulani’ wa pili, japo akifanya kosa dogo sana hukuzwa likawa kama Mlima Kilimanjaro.”


Mwalimu Nyerere aliandika kuwa watu hutafuta sababu za kumtetea ‘fulani’ aliyekosea kosa kubwa au kumlaumu ‘fulani’ aliyefanya kosa dogo kwa hoja za uongo. Aliendelea kusema ‘fulani’ wa kwanza akisema 2+2 ni 5 anasifiwa, ‘fulani’ wa pili akisema 2+2 ni 4, anaonekana mbaya.


Lingine ambalo Mwalimu Nyerere alilizungumzia ni “kutojielimisha”, kwamba tatizo linatokea lakini mnakimbilia kusingizia watu fulani badala ya kufanya uchunguzi ili kujua ukweli halisi. Wakati huo watu walikimbilia kusingizia wakoloni, Wazungu au vibaraka. Vilevile aligusia mtindo wa viongozi kujidanganya kuwa mawazo yao ndiyo ya wanachama wote.




Sasa tunaweza kutafakari


Hivi sasa vyama vya upinzani, hasa Chadema, ACT-Wazalendo na CUF vinakumbwa na wimbi la wanachama wake kuhamia CCM. Hoja ambayo inatoka kwa wanaohama ni kuwa wanaunga mkono juhudi za Rais John Magufuli kwa sababu anafanya kazi vizuri sana.


Hoja upande wa wapinzani ambao wanakimbiwa na wanachama ni kwamba wanaohama wananunuliwa. Bila shaka hii ni hoja ya kujifariji, mithili ya wakati wa Tanu kusingizia Wazungu, wakoloni au vibaraka. Mwalimu Nyerere alisema, hata kama huo ndiyo ukweli, usemwe baada ya uchunguzi.


Mbunge anatangaza kuhama chama na kujivua ubunge, badala ya viongozi kushituka na kuhoji kulikoni, wanakimbilia kujifariji kuwa ‘amenunuliwa’. Hata kama hoja ya kununuliwa ina ukweli, inapaswa kutolewa baada ya utafiti ambao utawezesha kujenga hoja zenye kuudhihirisha ukweli.


Chama cha siasa kinapaswa kutambua kuwa hoja ya kwamba wabunge au wanachama wake viongozi wanaohama wamenunuliwa si njema kwao. Chama kinakuwaje na viongozi wanaonunulika? Chama kinapitishaje jina la mtu kugombea ubunge mpaka kumsimamia ashinde bila kumpima na kuona hanunuliki?


Chama kinapoondokewa na wanachama, hakipaswi kujikita kwenye maneno mepesi ya kujifariji, bali kijitafakari chenyewe kama kinaishi kijamii. Je, kila mtu kwenye chama anajiona chama ni chake au kuna ambao wanajiona ni wanachama kuliko wengine?


Mathalan Chadema, kuna wabunge ambao wamekuwa wakijiweka kwenye orodha ya kuwa wanachama kuliko wengine, kiasi cha kunyooshea vidole wenzao kuwa wapo kwenye mipango ya kununuliwa. Mpaka hapo hitilafu haionekani kwenye chama? Chama ni kile ambacho kila mwanachama anajiona ana haki sawa na wengine, si zaidi wala pungufu.


Chama kama hakiishi kijamii, hakina utaratibu wa kupitia na kuratibu wanachama wake kwenye shina hadi matawi, hakitajua kwa nini wanachama wake wanahama. Na kitaendelea kushitukizwa kwa taarifa za kuhama kwa sababu chama hakina misingi ya umoja. Ile misingi aliyoieleza Mwalimu Nyerere.


Kwa faida ya vyama vya upinzani vinavyoathirika na wanachama wake kuhamia CCM. Ujumbe ni kuwa chama kisipokuwa na misingi imara na kuruhusu watu kujiunga nacho bila kuvutwa na itikadi au falsafa zake, kitakuwa kimbilio la wasaka fursa za uongozi na kimaisha.


Mtu ambaye hajashiba misingi ya chama na anakuwepo kwa ajili ya fursa, hata akishaipata, siku ikitokeza fursa kubwa zaidi ataondoka bila kujali chochote. Vilevile mtu akiwa anakwazwa na jinsi chama kinaendeshwa, siku akivutwa na malisho mema, atavutika tu.


Chama hakipaswi kuwa na wanachama wanaovumilia na wengine wanafurahia. Chama hakitakiwi kiwe na watu ambao wapo kwa sababu hawana pa kwenda, wanaona aibu kuondoka, hawajashawishiwa au hawawezi kuacha ugali wao. Aina hiyo ya wanachama ni bomu. Vyama vijitafakari.

MWANANCHI

No comments: