Header Ads

Blogger Tips and TricksLatest Tips And TricksBlogger Tricks

FAMILIA YA LISSU YALIA NA BUNGE




Kaka wa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, Alute Mughwai amehoji kitendo cha Bunge kushindwa kutoa stahiki za ndugu yake tangu aliposhambuliwa kwa risasi, Septemba 7 mwaka jana.


Wakati Mughwai akieleza hayo, Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai amesema Bunge linaendelea na mazungumzo na familia ya mbunge huyo kuhusu kumlipa stahiki hizo.


Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Arusha, Mughwai alisema licha ya kumwandika barua Kagaigai, chombo hicho cha Dola kimeendelea kuwa kimya kuhusu matibabu ya Lissu ambaye pia ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).


Lissu alishambuliwa kwa risasi zaidi ya 30, Septemba 7 mwaka jana na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma na siku hiyohiyo alihamishiwa Hospitali ya Nairobi ambako alilazwa hadi Januari 6 alipohamishiwa Ubelgiji katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven, anakoendelea na matibabu.


Mughwai alisema ingawa Lissu anaendelea vizuri na matibabu ya viungo, “bado hatujapata fedha zake za kujikimu na matibabu kama ambavyo sheria za Bunge zinaeleza.”


Alisema Januari 10, alipokea barua ya Kagaigai ikieleza kuwa ameunda jopo la madaktari watatu kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ambalo lilikwenda Nairobi kuchunguza afya ya Lissu, kushauri Bunge juu ya malipo yake kulingana na taratibu za matibabu nje ya nchi. “Sasa hawa walijua kabisa kuwa tangu Januari 6 Lissu amepekwa Ubelgiji wao wanaunda timu ya madaktari Januari 10 kwenda Nairobi kufuatilia afya yake ili kumshauri Katibu wa Bunge. Hatudhani kuwa ni sahihi,” alisema.


Alisema gharama za matibabu za Mwanasheria Mkuu huyo wa Chadema sasa ni kubwa kwani mkewe anayemuuguza amelazimika kutafuta sehemu ya kuishi nje ya hospitali hiyo.


“Tunaomba Bunge kutimiza wajibu wake. Kumpatia Lissu stahiki zake kwani sasa gharama ni kubwa zaidi na kutokana na kauli za Bunge kuwa litagharamia matibabu watu wengine wamepunguza michango yao.”


Alisema kama wanafamilia wataendelea kudai stahiki zote za Lissu kwa madai kuwa wanadhani hakuna nia njema juu ya tatizo lililomkuta mbunge huyo. “Hawa waheshimiwa wanataka Lissu awe kilema kabla hawajawa tayari kutoa matibabu na posho ya kujikimu, sasa hivi anaishije nchini Ubelgiji,” alihoji.


Alipoulizwa kuhusu stahiki za mbunge huyo, Kigaigai alisema, “Bunge tutaendelea na mazungumzo na familia kuwezesha taratibu za stahiki za Lissu. Kuhusu madaktari ni kweli tuliomba timu ya madaktari ikasaidie Nairobi lakini inaonekana Lissu aliondoka kabla ya timu ya madaktari kufika.”


Katika hatua nyingine, Mughwai alisema hadi Lissu anaondoka kwenda Ubelgiji, Jeshi la Polisi halijamuhoji dereva wa mbunge huyo aliyekuwa naye siku aliposhambuliwa kwa risasi.


Licha ya msemaji wa polisi, Barnabas Mwakalukwa kutopatikana kuzungumzia madai hayo kutokana na simu yake kuita bila majibu, mara kadhaa jeshi hilo limekuwa likisema linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.


Katika ufafanuzi wake Mughwai alisema Desemba 4 mwaka jana, polisi iliahidi kutuma makachero wake Nairobi lakini hawakwenda.


“Nilikwenda Nairobi kuwasubiri na nilikaa siku tatu hawajatokea. Wito wetu, ni vyema wakaitwa wachunguzi wa kimataifa katika suala hili,” alisema.




“Haitakuwa mara ya kwanza kuombwa wachunguzi wa nje, tukio la kuuwa padri Zanzibar, Serikali iliruhusu wapelelezi kutoka Marekani ambao walifanyakazi nzuri na kutoa taarifa,” alisema.

No comments: