Kesi ya Mobeto dhidi ya Diamond yafutwa
Jalada la kesi ya madai ya matunzo ya mtoto, Prince Abdul lililofunguliwa na mwanamitindo Hamisa Mobeto dhidi ya msanii Nasseb Abdul maarufu Diamond Platnumz limefungwa rasmi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu upande wa watoto.
Leo Februari 13, 2018 baada ya kutoka mahakamani hapo, Diamond amesema walifika kwa ajili ya kuweka kumbukumbu sawa upande wa ustawi wa jamii na mahakama.
Amesema wanategemea mtoto wao kuwa kiongozi huku akiwashauri wazazi kuweka majivuno pembeni wanapokuwa na migogoro na wasimuingize mtoto.
"Nalazimika kuweka majivuno pembeni ya matatizo yetu binafsi kwa kuwa mtoto ndiyo anaumia, ni lazima muangalie ni namna gani mnatengeneza mazingira mazuri ya kuweza kumlea na kumsaidia mtoto,” amesema Diamond.
Naye wakili wa Mobeto, Walter Godluck amesema ustawi wa jamii unasaidia katika usuluhishi wa kesi za watoto zinazohusu malezi ambapo baba na mama hukubaliana ni jinsi gani wanaweza kulea mtoto.
“Malalamiko waliyoyaleta kuhusu malezi ya mtoto upande wa pili wameridhia na wameona kuna haja ya kuyafanyia kazi. Kiasi cha fedha wamekubaliana ila wamekiweka kifamilia,” amesema Godluck.
Soma: VIDEO: Kiatu cha Diamond chakatika mahakamani
“Wazazi wamekubali kushughulikia malezi ya mtoto. Diamond yupo tayari kumlea mtoto na yupo tayari kulifanya hilo kwa kadri inavyowezekana.”
Hamisa Mobeto amesema amefurahia maamuzi hayo kwa kuwa pande zote mbili walikaa na wakakubaliana.
Mobeto alifungua kesi hiyo mahakamani hapo, pamoja na mambo mengine alikuwa anaomba matunzo ya mtoto waliozaa na msanii Diamond.
Aliiomba mahakama imwamuru Diamond kutoa matunzo ya mtoto huyo kila mwezi. Alifungua kesi hiyo kupitia mawakili wake Abdullah Lyana na Godluck kutoka kampuni ya uwakili ya Century Attorneys.
Kupitia hati hiyo ya madai, Mobeto anaomba Diamond amuombe msamaha kwa kumsababishia madhara yaliyoishtua familia yake.
Diamond aliwasilisha hati ya majibu kinzani akipinga maombi hayo ya Mobeto akidai gharama anazodai kulipwa kwa mwezi ya Sh 5 milioni kwa ajili ya matunzo ya mtoto ni kubwa hawezi kuzimudu.
No comments: