POLISI WAFUTWA KAZI KIGOMA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Ferdinand Mtui amesema kutokana na utaratibu wa kijeshi, askari hao walichunguzwa na mashitaka yaliendeshwa dhidi yao kwa miezi mitatu kabla ya kuchukua uamuzi huo.
Amewataja askari waliofukuzwa kazi ni Koplo Johnson, PC Justine na WP Mercy ambao pamoja na kufukuzwa kazi, wamepewa nafasi ya kukata rufaa ikiwa hawakubaliani na hukumu waliyopewa.
“Askari huwa wanaajiriwa kwa cheti lakini wanafukuzwa kwa makosa ya utovu wa nidhamu na hili linachukuliwa kwa Askari yeyote bila kujali ukubwa wa cheo chake. Ni vema wakawa makini kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa sheria za kijeshi ili kuepuka hali ya namna hii kutokea,” amesema Mtui.
Licha ya kushindwa kufafanua makosa hayo kuwa yalimlenga Kigogo gani wa Jeshi hilo, lakini habari za uhakika zilizopatikana katika Kituo cha Polisi kati mjini Kigoma zinaweka bayana kwamba askari hao watatu walitoa lugha za kejeli kwenye mitandao ya kijamii wakidai ziara ya Mkuu wa Jeshi hilo, IGP Ernest Mangu haikuwa na tija mkoani Kigoma.
“Hawa wenzetu waliofukuzwa walikuwa wanachati (wanaandika) kwenye mitandao wakijadili kama ujio wa IGP Kigoma unaonekana kuleta tija lakini ikatokea wakubwa wakapata taarifa hiyo na ndipo hatua zimechukuliwa dhidi yao,” amesema askari mmoja aliyekataa jina lake lisitajwe.
Kamanda Mtui ametoa wito kwa askari kuzingatia maadili ya kazi katika muda wote wanapokuwa katika utekelezaji wa majukumu yao na hatua za kinidhamu zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka maadili ya kazi.
Hata hivyo, askari wote watatu waliofukuzwa kazi wanadaiwa kukata rufaa kupinga hukumu waliyopewa.
MWANANCHI

No comments: