Header Ads

Blogger Tips and TricksLatest Tips And TricksBlogger Tricks

SERIKALI YASHINDWA KUWEKA WAZI POLISI WALIOGUSHI VYETI

SERIKALI  imeshindwa kutoa taarifa ya idadi ya askari wa Jeshi la Polisi ambao wanadaiwa kughushi vyeti tofauti na ilivyoahidi hivi karibuni kuwa itaweka majina hayo hadharani.
 
Awali, Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, aliahidi kutoa orodha ya askari ambao wameghushi vyeti vyao pamoja na ile ya wafanyabiashara wanaojishughulisha na uuzaji wa dawa za kulevya.
 
Gazeti hili liliwahi kumnukuu Waziri Kitwanga akisema kuwa amekabidhiwa majina ya askari ambao amegushi vyeti vya taaluma na kuahidi kuwa hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
 
Lakini licha ya wiki mbili tangu Waziri aahidi hivyo bado na wahusika wanapoulizwa wamekuwa wakirushiana mpira.
 
Nipashe ilizungumza na Waziri Kitwanga kwa njia ya simu ambapo alisema kuwa tayari alishazungumzia suala hilo hivyo hawezi kulizungumzia mara ya pili na kuagiza atafutwe Msemaji wa Jeshi la Polisi Advera Bulimba.
 
"Sio kila jambo azungumze Waziri mtafute huyo msemaji atakujulisha na asipokujulisha niambie," alisema Waziri lakini msemaji huyo alipotafutwa alisema hajui lolote kuhusiana na suala hilo.
 
Msemaji huyo ambaye ni  Mrakibu Mwandamizi wa Polisi,  Bulimba, alisema hana taarifa ya suala hilo na alielekeza atafutwe msemaji wa wizara hiyo.
“Sina taarifa hiyo na kama ningekuwa nayo ningewajulisha mtafuteni Msemaji wa Wizara umuulize huenda akawa nayo,” alisema Bulimba.
 
Alipotafutwa, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Isack Nantanga, alisema kuwa orodha hiyo bado haijafika wizarani.
 
Wiki chache zilizopita, Waziri Kitwanga alisema anayo orodha ya askari wanaotuhumiwa kughushi vyeti na kuahidi kuwa wakithibitika watachukuliwa hatua kali huku akiahidi kuweka hadharani majina yao.
 
 NIPASHE

No comments: