PENGO ASEMA MUHIMBILI INATOSHA
Askofu Mkuu Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Kardinali Polycarp Pengo, aliyelazwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), amekataa kwenda nje ya nchi kwa matibabu akisema kuwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) inatosha.
Pengo amelazwa kwenye taasisi hiyo tangu Januari Mosi mwaka huu, na hali yake imeelezwa kuwa inaendelea vizuri na anaweza kuruhisiwa wakati wowote kuanzia sasa.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Watoto na Wazee, Ummi Mwalimu, ambaye alimtembelea Askofu Pengo hospitalini hapo, alisema alimsikia Askofu Pengo akisema kuwa watakuwa na kazi ya ziada kumshawishi kupelekwa nje kwa matibabu.
Mwalimu alisema amefurahishwa na kauli hiyo kwani imemtia moyo kwamba juhudi za serikali za kuwezesha huduma mbalimbali za afya zinapatikana Tanzania zimezaa matunda na viongozi mashuhuri kama yeye wameanza kufurahia huduma hizo.
Mkurugenzi wa taasisi ya JKCI, Profesa Mohammed Janabi alisema hali ya Askofu Pengo imeimarika na wanatarajia kumruhusu kwenda nyumbani wakati wowote kuanzia leo na kuongeza kuwa Askofu huyo hapendelei kwenda kutibiwa nje ya nchi.
Mwalimu aliwatoa hofu Watanzania na kuwaeleza kuwa, afya ya Askofu Pengo imeimarika na ameambiwa kuwa anaweza kuruhusiwa wakati wowote.
Waziri alisema huduma inayotolewa na taasisi hiyo tangu mwaka jana imeiwezesha serikali kuokoa Sh. Bilioni tatu zilizokuwa zitumike kwa wagonjwa wanaopelekwa nje ya nchi.
Aidha, alisema wako wagonjwa 300 ambao wanasubiri kufanyiwa upasuaji huku taasisi hiyo ikiiomba serikali isaidie angalau kuwalipia wagonjwa 50.
Waziri alisema kutokana na kauli iliyotolewa na Askofu Pengo kuhusu huduma nzuri zinazotolewa na taasisi hiyo, serikali itaangalia wezekano huo na itaendelea kuiwezesha ili iendelee kufanya vizuri.
Alisema kwa sasa madaktari bingwa katika taasisi hiyo wanafanya upasuaji ambao awali ulikuwa ngumu kufanyika nchini.
Kulingana na viwango vya kimataifa vya upasuaji vya asilimia 6, taasisi hiyo imefikia asilimia nne, hatua ambayo ni nzuri, alisema waziri.
CHANZO: NIPASHE

No comments: