Header Ads

Blogger Tips and TricksLatest Tips And TricksBlogger Tricks

SIRI ZA MAUAJI YA KWENYE VIROBA ZAFICHUKA!

Samson Josiah enzi za uhai wake.

DAR ES SALAAM: Siri ya mauaji ya watu na miili yao kukutwa kwenye viroba kando ya bahari na mito imefichuka, Amani limechimba na kuibuka na siri.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba, watu wasiojulikana wanaofanya mauaji hayo, huyafanya ili kuficha ushahidi wa mauaji hayo ya kutisha.

Akizungumza na gazeti hili afisa mmoja wa serikali ambaye aliomba jina lake lihifadhiwe kwa sababu siyo msemaji rasmi alieleza kuwa, wauaji hao wanakuwa wameiweka miili kwenye viroba ili kuficha ushahidi wa kuwatambulisha.


Kauli ya afisa huyo imekuja huku kukiwa bado kuna wingu la mmiliki wa mabasi ya Super Sami, Samson Josiah mkazi wa Magu, Mwanza kuuawa kikatili na watu wasiojulikana na mwili wake kukutwa katika Mto Ndabaka wilayani Bunda mkoani Mara, ukiwa umefungwa kwenye kiroba.
Polisi bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo la kusikitisha na linawashikilia watu wanne, huku gumzo likiwa ni kwa nini mtu auawe halafu afungwe kwenye kiroba na kutupwa mtoni.
Afisa huyo alibainisha kuwa, kwa kuiweka miili hiyo kwenye viroba na kuitupa kwenye bahari au mito, wanakuwa wamepoteza ushahidi wa alama za vidole.


“Wanafanya unyama huo ili kuwahangaisha wapelelezi wanaochunguza miili hiyo, kwa kuwa wanajua kwamba finger print (alama za vidole) za wahalifu hao zitafutika kwa maji baada ya maiti kuitumbukiza mtoni au baharini,” alisema afisa huyo.
Kwa mujibu wa afisa huyo, maiti iliyotupwa kwenye maji na kukaa siku kadhaa, huwa rahisi kuharibika hivyo hata ile dhana kwamba inaweza kuchunguzwa na kuwagundua waliofanya unyama huo huwa ni ndogo.

Pia kuna macho ya mtu aliyeuawa yanaweza kutunza kumbukumbu ya aliyemuua, lakini baada ya miili hiyo kutupwa baharini au mtoni, kumbukumbu hiyo hupotea.
Vilevile sababu nyingine ya wauaji kuwazamisha watu waliouawa baharini au mtoni ni kuficha eneo la tukio, kwani wanajua kwamba maiti kwenye maji husafirishwa kwa kusukumwa na maji umbali mrefu, hivyo ni vigumu kugundua mara moja mtu huyo aliuawa wapi.


“Wauaji wanaweza kuwa eneo A na maiti ikakutwa eneo D, hivyo basi wauaji akili yao ni ileile kuwahangaisha wapelelezi, kusudi wadhani kwamba tukio limetokea eneo D wakati ukweli ni kwamba mtu huyo aliuawa eneo A, hivyo kuwapa kazi ya ziada Makachero wanaochunguza tukio husika,” alisema mtoa habari wetu.
Afisa huyo aliongeza kuwa, nia yao wahalifu hao ipo wazi kwamba maiti waliyoitupa ionekane mbali na sehemu waliyofanyia mauaji kwa kuwa wanajua kwamba maji ya mto au bahari yatasafirisha maiti chini kwa chini kutokana na kuwekewa mawe mazito kwenye viroba walivyofungia miili hiyo.

Mauaji yaliyowahi kutokea Kibiti.

Aliongeza kwamba mara nyingi watu wanaofanya vitendo hivyo huwateka watu wanaowaua na huwa hawawachukui kwa hiari yao, hivyo inawezekana wanawapeleka sehemu kuwatesa ili wawaambie kile wanachokitaka kwao.
“Inawezekana mtu aliyeuawa aliteswa kwanza na wauaji ili aweze kutoa siri wanazozitaka na baada ya kupata wanachokitafuta, huwaua na kuwafunga kwenye viroba pamoja na mawe kisha kuwazamisha mtoni au baharini,” alisema.

MSEMAJI WA POLISI NCHINI
Gazeti hili lilimtafuta Msemaji wa Jeshi la Polisi, ACP Barnabas Mwakalukwa kuhusiana na siri hizo kama polisi wana habari nazo, alisema msemaji wa matukio hayo ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Mwigulu Nchemba.
“Mtafuteni Waziri wa Mambo ya Ndani (Mwigulu), kwakuwa ndiye msemaji wa matukio hayo,” alisema Kamanda Mwakalukwa.
WAZIRI MWIGULU ALIVYONENA
Waziri huyo alipotafutwa kwa njia ya simu hakuweza kupatikana kwa simu zake zote mbili, hata hivyo siku za nyuma aliwahi kufafanua kwamba huenda watu waliokutwa wamekufa na kutupwa kwenye Mto Ruvu na kufungwa kwenye viroba walikuwa ni wahamiaji haramu ambao walikumbwa na mkasa huo toka kwa wasafirishaji wa wahamiaji hao.

Waziri Mwigulu alisema kitendo cha kukutwa kwa wahamiaji zaidi ya 80 wakiwa na majeraha na hawajiwezi mkoani Pwani, kinahusisha kwa namna moja au nyingine na maiti zilizookotwa Mto Ruvu mwaka jana.
Aliongeza kuwa, Tanzania hakuna tishio lolote kuhusu watu kupotea au kuuawa kama inavyoelezwa na baadhi ya watu na kusema kuwa wizara yake inapambana kuhakikisha watu na mali zao wako salama.

Waziri Nchemba alisema kuwa miili ya watu ambayo imekuwa ikiokotwa baharini au mtoni si miili ya Watanzania, kwani kama ingekuwa miili ya Watanzania basi familia zao zingekuwa zinasikika zikipiga kelele kuhusu ndugu zao hao kupotea.
“Mimi kama Waziri wa Mambo ya Ndani nakuhakikishieni Watanzania kwamba wizara inapambana kuhakikisha watu na mali zao wako salama na mpaka sasa hakuna tishio la namna hiyo, kusema kwamba watu wanapotea hovyohovyo au watu wanauawa hakuna kitu cha namna hiyo,” alisema.
Waziri Mwigulu Nchemba akiwa na maofisa wa Jeshi la Polisi.

“Inapotokea miili inaokotwa baharini, bahari ambayo tunachangiana nchi nyingi sana na miili pia inaweza kusafiri kwa upepo kutoka sehemu nyingi sana japokuwa kuna watu wanasema watu wanauawa hovyo, haiwezekani watu wauawe hovyo halafu kukawa shwari tu familia zikawa zimetulia lazima familia zingepiga kelele,” alisema Mwigulu.
Aidha, Waziri Mwigulu alitaka ajenda za watu zisigeuke kuwa siasa na kusema kuwa ajenda za siasa zifanywe kwenye siasa na si maisha ya watu.

Aliongeza kuwa, bado wanaendelea na uchunguzi juu ya matukio hayo ikiwa ni pamoja na operesheni mbalimbali za kutokomeza matukio ya kihalifu pamoja na wahamiaji haramu nchini.
Akaongeza kuwa iwapo kuna watu ambao ndugu zao wamepotea ni vyema wakafika katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa ajili ya vipimo na kufanyika upelelezi.
“Bahari ni kubwa inapita katika nchi nyingi na inachukua kila kitu, haya mambo yanapotokea hata nchi nyingine yanatokea. kwahiyo kimsingi tumeunda timu ya wataalamu ya kupeleleza kuhusu miili hii inayopatikana kwenye fukwe za bahari na mtoni,” alisema.
IGP Sirro.

IGP NAYE ALIWAHI KUNENA
Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Simon Sirro aliwahi kuzungumzia kadhia hiyo na akatoa wito kwa kusema: “Kama kuna mtu ambaye ndugu yake amepotea afike makao makuu ya polisi upande wa DCI tuweze kufanya uchunguzi kuona kama ni ndugu yake.
“Tatizo letu Watanzania ni kwamba moja kwa moja wanaanza kuhisi, sijui kwa nini tunakuwa tunaishi kwa hisia na hizi. Hisia si nzuri tuseme kitu tukiwa na uhakika. Ikitokea jambo utasema ni Sirro, utasema ni nani, hii si nzuri na niwaambie tumwogope Mungu pia,” alisema IGP Sirro.

No comments: