SERIKALI YATENGA BILIONI 131.4 KWA AJILI YA ELIMU BURE KWA MWAKA UJAO
Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 131.4 kwa ajili ya kugharamia uendeshaji wa shule za msingi na sekondari kuanzia mwaka ujao wa masomo ambapo fedha hizo pamoja na mambo mengine zitatumika kama ruzuku ya uendeshaji mashuleni, chakula kwa wanafunzi wa bweni, karo na gharama za mitihani ikiwemo ya kidato cha nne ikiwa ni utekelezaji wa ahadi yake ya kutoa elimu bure ili kila mtoto apate haki hiyo ya msingi.
Waziri wa nchi ofisi ya rais tawala za mikoa na serikali za mitaa Tamisemi Mhe George Simbachawene anatoa taarifa kwa umma kuhusu elimu bure kwa shule za serikali ambapo anasisitiza utekelezaji wake unahitaji ushirikishwaji wa karibu kwa wadau wote wa elimu huku akiwaagiza viongozi wote wakiwemo wakuu wa mikoa na wilaya pamoja na wakurugenzi wa halmashauri na mamlaka za serikali za mitaa kusimamia utekelezaji wake.
Aidha taarifa hiyo pia ikabainisha maeneo ambayo wazazi na walezi wanapaswa kutoa michango ambayo ni pamoja na sare za shule na michezo, vifaa vya kujifunzia, matibabu, nauli kwa wanafunzi wa kutwa na bweni magodoro na mashuka na vifaa vya usafi binafsi kwa wanafunzi wa bweni huku pia jamii ikitakiwa kutoa taarifa kwenye mamlaka za serikali zilizo karibu nao kuhusu mienendo inayokwenda kinyume na elimu bila malipo.
Kufuatia taarifa hiyo ITV inazungumza na baadhi ya wakazi wa mkoa wa Dodoma na wanaonyesha kuipokea kwa furaha huku wengine wakitia shaka juu ya utekelezaji wake ambapo waziri Simbachawene anatolea ufafanuzi.
Wakati huohuo waziri Simbachawene amemuagiza mkurugenzi wa manispaa ya Dodoma kuwasimamisha kazi mara moja kaimu afisa biashara wa manispaa hiyo Elias Kamara na afisa biashara Donatila Vedasto kwa makosa ya urasimu katika utoaji leseni za biashara na rushwa hali iliyochangia upotevu wa zaidi ya shilingi milioni 75 taarifa inayotolewa kwa niaba yake na mkuu wa kitengo cha mawasiliano Tamisemi Rebecca Kwandu.
ITV
No comments: