HOTUBA YA MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, MWENYEKITI WA CHAMA CHA MAPINDUZI, WAKATI WA MKUTANO MKUU WA CCM DODOMA, 23 JULAI 2016
Mheshimiwa Dr. John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Dr. Ali Mohammed Shein, Makamu Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Zanzibar;
Mheshimiwa Philip Mangula, Makamu Mwenyekiti wa CCM – Bara;
Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania;
Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idd, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi, Rais na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM;
Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, Rais na Mwenyekiti Mstaafu wa CCM;
Mheshimiwa Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM;
Waheshimiwa Makamu Mwenyeviti Wastaafu wa CCM;
Waheshimiwa Makatibu Wakuu Wastaafu wa CCM;
Waheshimiwa Mawaziri Wakuu Wastaafu;
Waheshimiwa Wajumbe wa Kamati Kuu;
Waheshimiwa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa;
Waheshimiwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Taifa;
Wageni wetu waalikwa; Mabibi na Mabwana,
Kama ilivyoada naomba tuanze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujaalia uzima na kutusafirisha salama kutoka makwetu hadi hapa Dodoma. Nawapa pole ya safari na karibuni Dodoma na kwenye Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa Chama cha Mapinduzi. Kwa niaba yenu napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi nyingi kwa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa, chini ya uongozi makini wa Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana kwa maandalizi mazuri ya mkutano huu. Pongezi maalum tunazitoa kwa Kamati mbalimbali zilizoongozwa na kuratibiwa na Naibu Katibu Mkuu Bara Ndugu Rajab Luhwavi kwa kazi kubwa na nzuri waliyofanya mpaka mambo yamekuwa mazuri kiasi hiki kama sote tunavyoshuhudia. Ni matumaini yangu kuwa tutamaliza salama.
Kwa niaba yenu pia napenda kuwashukuru wenyeji wetu wa Mkoa wa Dodoma, wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa, Ndugu Adam Kimbisa na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Ndugu Jordan Rugimbana kwa kutupokea vizuri na kutuwekea mazingira mazuri ya kuishi na kufanya mkutano wetu. Nimeambiwa kuwa hali ya usalama ni nzuri na ya uhakika.
Karibuni Wageni waalikwa
Ndugu Wajumbe,
Katika mkutano huu tumealika wageni mbalimbali. Wapo wazee wa Chama na marafiki wa CCM. Pia wapo watu mashuhuri, Mabalozi wa nchi za nje na wawakilishi wa mashirika ya kimataifa waliopo hapa nchini. Hali kadhalika kuna wawakilishi wa vyama vya siasa. Wote hawa tunawashukuru sana kwa kukubali mwaliko wetu na kuja kujumuika nasi kwenye siku hii muhimu katika historia ya Chama cha Mapinduzi. Kuja kwao ni jambo la heshima na faraja kubwa kwa viongozi na wanachama wa CCM. Ahsanteni sana, tunaomba muendelee na moyo huo wa ushirikiano.
Ndugu Wajumbe,
Kama tujuavyo tumekutana hapa siku ya leo kwa ajili ya kubadilisha uongozi wa juu wa Chama cha Mapinduzi. Hii itakuwa ni mara ya nne katika miaka 39 ya historia ya uhai wa chama chetu. Mara ya Kwanza ilikuwa Agosti, 1990 wakati Mwenyekiti wa Kwanza na muasisi wa CCM, Mwalimu Julius Nyerere alipong’atuka na Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi aliyekuwa Rais wa pili wa Jamhuri ya Muungano alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa pili. Mara ya pili ilikuwa Juni, 1996 wakati Mheshimiwa Benjamin William Mkapa alipochaguliwa kuwa Mwenyekiti wa tatu wa CCM kuchukua nafasi ya Mwenyekiti wa pili Mheshimiwa Ali Hassan Mwinyi alipostaafu. Mara ya tatu ilikuwa tarehe 25 Juni 2006 wakati Mwenyekiti wa tatu Mheshimiwa Benjamin Wiliam Mkapa alipong’atuka na mimi kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa nne. Leo imefikia zamu yangu kustaafu na kukabidhi hatamu za uongozi wa juu kabisa wa Chama chetu kwa Rais wa Tano Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli kuwa Mwenyekiti wa tano wa Chama cha Mapinduzi. Raha ilioje ndugu zangu. Nani kama CCM.
Ndugu Wajumbe,
Niruhusuni kwa niaba yenu na kwa niaba yangu binafsi nitoe pongezi nyingi kwa Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli kwa kukubali kubeba dhamana ya kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi. Najua haikuwa Rais kwake kukubali na ilibidi tufanye kazi ya ziada kumshawishi mpaka akakubali. Nakumbuka mara ya kwanza mwezi February 2016 nilipomuambia kuhusu jambo hili alikataa hata kulizungumzia. Akaniambia kuwa yeye hana haraka kwani ana mambo ya kufanya Serikalini na ndiyo kwanza anaendelea kupanga mambo yake. Jitihada na ufundi wangu wote haukufanikiwa kumshawishi akubali. Nadhani kwa nia ya kutaka niachane na mazungumzo yale alinikaribisha chakula. Nikamkubalia tukala tukaagana.
Baadae nikamsimulia Makamu Mwenyekiti wa CCM Mzee Philip Mangula, matokeo ya mazungumzo yangu na Rais na kumuomba nae akajaribu. Waswahili wamesema mzee dawa. Mwezi mmoja na nusu baadae Mzee Mangula akarudisha jibu kuwa Rais amesema sawa, tuamue na kupanga siku. Ndipo nikarudi tena kwake na mapendekezo ya tarehe mbili tatu aangalie kwenye ratiba yake ipi ingemfaa. Baada ya muda si mrefu tukapata jibu la tarehe ya 23/7/2016 kuwa ingefaa. Ndiyo maana ya kupanga na kukutana siku ya leo.
Ndugu Wajumbe,
Majibu yale ya Rais wetu hayakunishangaza kwani hata mimi na Mheshimiwa Benjamin Mkapa ilikuwa hivyo hivyo. Aliponipa wazo la kuniachia Uenyekiti kwa mara ya kwanza February 2006 nilimkatalia na hoja zangu ni kama hizo hizo alizoniambia Mwenyekiti wetu mtarajiwa. Baada ya mazungumzo zaidi nilikubali na ndipo Mkutano Mkuu Maalum ukafanyika June 25, 2006 na nikachaguliwa kuwa Mwneyekiti wa Nne wa CCM. Tofauti ya wakati ule na sasa ni kwamba hapakuwepo na vyombo vya habari na watu waongo, wazushi, wachonganishi na wafitini waliodai kuwa Mzee Mkapa anang’ang’ania kama ilivyokuwa kwangu kudaiwa ati sitaki kukabidhi Uenyekiti. Tena wakaongeza ati wapo watu wanaozunguka kushawishi zoezi zima lisifanyike. Sijui baada ya leo watasema nini au watazua uongo upi mpya! Najua hawataacha maana inaelekea kuna mitambo mahsusi ya kutunga uongo na kila siku wanazalisha bidhaa mpya. Lengo lao ni kuchochea mfarakano ndani ya CCM na wanasikitika kwamba jitihada zao hazifanikiwi. Ndugu zangu tuendelee kuwa makini.
Ndugu Wajumbe,
Kama kweli ningekuwa sitaki kuachia ngazi baada ya Rais kuniambia hana haraka nisingekwenda kumtafuta Mzee Mangula akazungumze nae tena. Nilifanya vile kwa dhamira ya kudumisha mila na desturi nzuri ya kuunganisha kofia ya Urais wa Jamhuri ya Muungano na Uenyekiti wa Chama cha Mapinduzi. Pili ni kutokana na kutambua kuwa kofia hizi mbili kuvaliwa na mtu mmoja ni jambo lenye maslahi mapana kwa Chama chetu, Serikali yetu na nchi yetu. Ni jambo muhimu sana kwa utulivu na ustawi wa Chama Cha Mapinduzi, Serikali na Tanzania. Wazee waliona mbali walipoamua iwe hivyo. Nisingependa “mguu wangu uote tende kwa kutosikia la mkuu”. Bahati nzuri kwangu wakati inaamuliwa kutenganisha kofia kwa Wakuu na Makatibu wa Mikoa na Wilaya na kubakisha kwa Rais na Mwenyekiti ngazi ya Taifa nilikuwepo na nilishiriki kufanya uamuzi. Naelewa vyema sababu, hekima, busara na mantiki ya uamuzi ule. Sijaiona sababu ya kwenda kinyume na uamuzi huo.
Shukrani Binafsi
Ndugu Wajumbe,
Kwangu mimi, leo ni siku nyingine muhimu na ya aina yake katika historia ya maisha yangu. Ni siku ambayo safari yangu ya utumishi na uongozi katika Chama inafikia ukomo. Safari yangu hiyo niliianza tarehe 2 April 1975, nilipowasili Singida kuanza kazi ya Katibu Msaidizi wa TANU Mkoa wa Singida. Mwaka mmoja baadae nikapelekwa Jeshini na baada ya kuunganisha ASP na TANU na kuzaliwa Chama Cha Mapinduzi nilihamishiwa Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui, Zanzibar. Pamoja na kuwa na jukumu la kumsaidia Naibu Katibu Mtendaji Mkuu wa CCM Col Ayoub Simba na baadae Capt. Allan Heri nilipewa dhamana kubwa ya kutengeneza mfumo mpya wa utawala na uendeshaji wa shughuli za Chama Zanzibar. Hususani tulifanya kazi ya kuhaulisha mfumo uliokuwa unatumika na ASP na kuwa ule wa CCM kuanzia Afisi Kuu Kisiwandui mpaka Ofisi za Mikoa, Wilaya na Matawi. Pia nilihusika na kuandaa mchakato wa uteuzi wa Makatibu Watendaji wa Wilaya na Mikoa, Makatibu Wasaidizi na watumishi wengine wa Chama.
Mwaka 1980 nilihamishiwa Ofisi Ndogo ya Makao Makuu ya CCM, Dar es salaam ambapo nilikuwa Mkuu wa Utawala, Mkuu wa Idara ya Ulinzi na Usalama na Msaidizi Mahususi wa Katibu Mtendaji Mkuu wa CCM wakati ule Mzee Pius Msekwa na baadae Mzee Daudi Mwakawago. Mwaka 1981 nikateuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa CCM Mkoa wa Tabora. Mwaka 1983 nikarejeshwa jeshini na miaka mitatu baadae (1986) nikateuliwa kuwa Katibu wa CCM Wilaya ya Nachingwea na baadae mwanzoni mwa mwaka 1988 nikahamishiwa Wilaya ya Masasi. Mwezi Novemba 1988 nilimalizia utumishi wangu baada ya kuteuliwa kuwa Mbunge na Naibu Waziri wa Nishati na Madini.
Kwa upande wa uongozi ndani ya Chama nilianza mwaka 1982 nilipochaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa kupitia kundi la Vijana. Niliendelea kuchaguliwa kwa nafasi hiyo kwa chaguzi za miaka ya 1987, 1992, 1997 na 2002 kupitia Kundi la 20 Bara. Mwaka 1997 na 2002 nilibahatika kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa, na mwaka 2006 nikapata heshima kubwa ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi na kuchaguliwa tena mwaka 2007 na 2012 hadi hii leo.
Ndugu Wajumbe,
Leo ninapostaafu Uenyekiti wa CCM nitakuwa nimetumikia Chama kwa takribani miaka 41 mfululizo kwa maana ya utumishi na uongozi. Na nikijumuisha muda niliotumia katika uongozi wa Umoja wa Vijana, nimekitumikia Chama hiki kwa miaka mingi zaidi ya hiyo. Hata nilipokuwa Jeshini nilikuwa najishughulisha na mambo ya siasa na Chama. Kwa kweli baada ya kipindi kirefu kiasi hicho kwanza kwangu mimi sasa kustaafu ni jambo ninalolistahili kabisa. Nitaendelea kuwa mwanachama wa kawaida na kutoa mchango wangu kwa uongozi wa Chama pale nitakapohitajika na kupitia Baraza la Wazee Wastaafu.
Ndugu Wajumbe,
Mtakubaliana nami kuwa ninayo kila sababu ya kutoa neno la shukrani. Orodha yangu ni ndefu kidogo hivyo naomba mnivumilie maana sijui kama nitapata fursa nyingine nzuri kuliko hii. Kwanza kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wetu na mwenye kutoa neema ndogo ndogo na neema kubwa kubwa. Namshukuru kwa kunijalia uzima na baraka zake zilizoniwezesha kufika hapa nilipofika maishani. Bila ya yeye nisingefika hapa. Namuomba aendelee kunilinda na kuniongoza nipate hatma njema. Pili nawashukuru wazazi wangu Mzee Halfan Mrisho Kikwete na Bi Asha Bint Jakaya Kalungwana kwa kunizaa, kunilea, kunisomesha na kwa ushauri na maelekezo yao yaliyonisaidia kupata mafanikio niliyoyapata maishani.
Namshukuru Mzee John Aaron Mhaville aliyekuwa Katibu Mtendaji Mkuu wa TANU kwa kuniona ninafaa kuajiriwa kuwa mtumishi wa Chama. Yeye ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Jopo lililonifanyia usaili nilipoonesha nia ya kupenda kutumikia Chama wakati nilipokuwa Chuo Kikuu cha Dar es salaam. Namshukuru Mzee Pius Msekwa aliyekuwa Katibu Mtendaji Mkuu wa kwanza wa CCM kwa mambo mengi. Namshukuru kwa kuniamini na kuniteua kwenda kufanya kazi Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui na kunipa dhamana kubwa nikiwa na umri mdogo wa miaka 26. Wakati ule nilikuwa nimekitumikia Chama kwa mwaka mmoja tu. Lakini yeye na waliokuwa Manaibu wa Katibu Mtendaji Mkuu wakati ule yaani Dr Salimin Amour Juma kwa Tanzania Bara na Col. Ayoub Simba kwa Zanzibar waliona wanijaribu. Bahati nzuri kwa malezi na uongozi wao na majaliwa ya Mwenyezi Mungu sikuwaangusha. Nikafanikisha vyema kama walivyonitarajia.
Uteuzi ule ulinipa fursa ya kushiriki vikao vyote vya Kamati za Kudumu za Chama, Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa nikiwa mmoja wa waandishi wa kumbukumbu za mikutano. Kwa sababu hiyo basi tangu mwaka 1977 mpaka sasa nimebahatika kuhudhuria vikao vyote vya Halmashauri Kuu ya Taifa CCM isipokuwa ule mwaka mmoja nilipohamishiwa Tabora kabla ya kuchaguliwa kuwa Mjumbe wa NEC mwaka 1982. Nimeyaona na kuyasikia mengi jambo ambalo limenijengea msingi nzuri wa uongozi katika Chama. Kama kuna kitu nakifahamu vizuri maishani ni kazi ya Chama.
SHUKRANI KWA MARAIS WASTAAFU
Ndugu Wajumbe,
Napenda pia, kuwashukuru Mwenyekiti wa Kwanza wa CCM Mwalimu Julius Nyerere na Katibu Mkuu na Makamu Mwenyekiti wa CCM Mzee Rashid Mfaume Kawawa kwa kuwa wazazi na walezi wangu wazuri wa kisiasa. Nawashukuru kwa kutambua vipaji vyangu na kazi waliyofanya ya kunilea, kuniendeleza na kuniongoza. Waliniamini na kunipa fursa iliyonijengea msingi mzuri ambao naamini ndiyo ulionisadia kufika hapa ninapomalizia leo.
Natoa shukrani maalum kwa viongozi wangu wawili muhimu sana katika maisha yangu ya kisiasa. Wa kwanza ni Mzee Ali Hassan Mwinyi, Rais wa Awamu ya Pili na Mwenyekiti wa Pili wa CCM. Namshukuru kwa kuniamini na kunifanya nijulikane kwa Watanzania. Mimi sikuwa Mbunge, nilikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa na Katibu wa CCM Wilaya ya Masasi. Uamuzi wake wa kuniteua kuwa Mbunge na Naibu Waziri wa Nishati na Madini Novemba, 1988 na baadae Waziri wa Maji, Nishati na Madini mwaka (1990) na Waziri wa Fedha (1994) ndivyo vilivyonifanya nijulikane kwa Watanzania.
Wa pili ni Mzee Benjamin Wiliam Mkapa Rais wa Awamu ya Tatu na Mwenyekiti wa Tatu wa CCM. Namshukuru kwa kuniamini na kunipa dhamana nzito ya kuongoza diplomasia ya Tanzania kama Waziri wake wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa miaka 10 mfululizo. Hii ilinipa fursa ya kuijua dunia na watu duniani kunijua. Niliweza kujifunza mambo mazuri na yenye manufaa kwa nchi yetu na kuwajua viongozi na watu duniani walioweza kuwa wa msaada na manufaa kwa nchi yetu. Mambo hayo yalikuja kunisaidia sana katika kuliongoza Taifa letu. Pia namshukuru kwa kunipa fursa ya kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM katika kipindi chote cha miaka 10 ya uongozi wake wa Chama chetu. Na jambo jingine muhimu namshukuru kwa kunilinda kwani kama asingefanya hivyo huenda nisingekuwa hapa leo. Mzee Mkapa sitakusahau maishani.
Mzee Mwinyi na Mzee Mkapa sina kitu wala namna ya kuwalipa kwa ihisani kubwa mliyonifanyia maishani. Nasema ahsanteni na tena ahsanteni sana. Inshaallah Mwenyezi Mungu atawalipa kwa wema wenu. Mimi nitaendelea kuwaombea maisha marefu yenye afya njema, furaha na faraja tele.
SHUKRANI MAKAMU WA MWENYEKITI
Ndugu Wajumbe,
Katika kipindi cha miaka 10 ya kuwa Mwenyekiti wa Chama nilifanya kazi na Makamu wa Mwenyekiti wa CCM watano. Kwa upande wa Zanzibar ambako nako tumekubaliana kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi anakuwa Makamu Mwenyekiti nilianza na kaka yangu na swahiba yangu Dr. Amani Abeid Karume. Ninamalizia uongozi wangu na Dr. Ali Mohamed Shein, Rais wa sasa wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Wamekuwa wasaidizi makini wa shughuli za Chama Zanzibar na bila ya wao sijui mambo yangekuwaje.
Kwa upande wa Tanzania Bara nilianza na Mzee John Samuel Malecela ambae pia ni Makamu wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu. Pamoja na kunisaidia kwa mengi yeye alikuwa mpambanaji wa mstari wa mbele kutetea na kupigania maslahi ya Chama. Nani asiyejua kazi ya Mzee Malecela kwenye chaguzi ndogo. Wa pili alikuwa Mzee Pius Msekwa, Spika Mstaafu. Yeye alikuwa kama kamusi na hazina inayotembea ya kumbukumbu za historia ya Chama na taifa. Alinisaidia sana kwa masuala ya Katiba ya Chama na nchi na Kanuni mbalimbali za Chama. Wa tatu na wa mwisho ni Mzee Philip Mangula Makamu Mwenyekiti aliyopo sasa. Yeye amesaidia sana kwa masuala ya maadili, nidhamu na udhibiti katika Chama. Amekuwa maarufu kama Mzee wa Mafaili.
Ndugu Wajumbe,
Kwa jumla Makamu Mwenyekiti wote wamenisaidia sana kuifanya kazi yangu ya Uenyekiti wa Chama kuwa rahisi hasa wakati nilipokuwa Rais wa nchi yetu ambapo nafasi ya kujishughulisha na masuala ya Chama kwa kila siku ilikuwa ndogo. Bila ya msaada wao mambo yangekuwa magumu sana. Hivyo basi napenda kukutoa hofu Rais wetu kwamba ukiwa na Makamu wa Mwenyekiti wazuri na Katibu Mkuu mzuri na ukiwapa fursa ya kufanya kazi zao na wewe ukasaidia kwa upande wa uwezeshaji utafanya kazi zako zote mbili vizuri. Hakuna jambo litakalo haribika upande wowote.
Shukrani Makatibu Wakuu na Watumishi wa CCM
Ndugu Wajumbe,
Vile vile nimefanya kazi na Makatibu Wakuu watatu. Wa kwanza alikuwa Lt. Yusufu Rajabu Makamba. Alikuwa mtu wa watu, aliyeweza kuchanganyika na watu wa makundi yote, rika zote na dini zote. Alikuwa rasilimali kubwa kwani kwa uwezo wa kujenga hoja alitusogezea watu wengi kuwa karibu na Chama. Wa pili alikuwa Ndugu Wilson Mukama, msomi, mwanafalsafa na bingwa wa masuala ya uchambuzi wa masuala ya kisiasa na kijamii. Alitusaidia sana katika mchakato wa kufanya mageuzi ndani ya Chama na kubuni na kupanga mikakati iliyosaidia katika kuimarisha na ujenzi wa Chama.
Ndugu Wajumbe,
Wa tatu na ambae ndiye Katibu Mkuu aliyepo sasa ni Ndugu Col. Abdulrahman Omar Kinana. Jembe la kazi. Jembe la Nguvu. Amefanya kazi kubwa na nzuri isiyokuwa na mfano wake. Amefanya kazi adhimu iliyoleta uhai na mtazamo mpya na chanya kwa Chama cha Mapinduzi. Juhudi zake zimeleta matumaini mapya ya Watanzania na wanachama kwa Chama cha Mapinduzi. Ni mtu wa mikakati, mbunifu wa hali ya juu na wa mipango yenye tija na maslahi kwa CCM. Katika miaka yake mitatu ya uongozi ametembelea Mikoa yote, Wilaya zote na Majimbo yote ya uchaguzi. Amekutana na kuzungumza na wanachama wa CCM na wananchi. Amefanya kazi ya kulima na ujenzi na kusikiliza shida za wananchi Kwa ajili hiyo aliwafanya viongozi na wanachama wa CCM wajiamini. Aidha aliwafanya wananchi waendelee kuwa na imani na CCM hivyo kupeperusha matumaini kidogo waliyokuwanayo jamaa zetu wa upande wa pili. Kwa kweli unapozungumzia utulivu wa CCM baada ya mchakato wa uteuzi wa mgombea Urais mwaka jana uliokuwa na majaribu mengi na mitihani isiyo na kifani, na unapozungumzia ushindi murua tulioupata katika Uchaguzi Mkuu, huwezi kushindwa kuona na kutambua mchango mahsusi wa Katibu Mkuu Ndugu. Abdulrahman Kinana. Ni jembe kweli kweli! Naomba tumpigie makofi ya nguvu kuelezea pongezi na shukrani zetu kwake.
Ndugu Wajumbe,
Nawashukuru kwa dhati Wanachama, Wenyeviti na Makatibu wa Mikoa, Wilaya, Majimbo, Kata na Matawi pamoja na Wajumbe wa Vikao vya Chama vya ngazi hizo kwa ushirikiano na msaada mlionipa katika kipindi chote nilichokuwa Mwenyekiti wa Chama chetu. Ushirikiano na msaada wenu ndivyo vilivyofanya kazi yangu kuwa nyepesi na tukapata mafanikio tuliyoyapata. Maombi yangu kwenu ni kuendelea kukijenga na kukipigania Chama cha Mapinduzi kwa ari, nguvu na kasi kubwa zaidi ya mlivyofanya wakati wangu. Pili naomba mumpe Mwenyekiti mpya ushirikiano na msaada maradufu zaidi kuliko mlivyofanya kwangu. Umoja na mshikamano ndiyo siri ya mafanikio na ushindi wa CCM. Umoja ni Ushindi.
Ndugu Wajumbe,
Nawashukuru kwa namna ya kipekee watumishi wa Chama cha Mapinduzi kwa moyo wao wa kujitolea, uzalendo na upendo kwa Chama chao. Nayasema haya kwa dhati kwani nafahamu kuwa watumishi wa Chama wanalipwa ujira mdogo sana na hawana marupurupu mengi. Kutokana na hali ngumu ya kifedha inayokikabili Chama chetu hata viposho vilivyokuwa vinasaidia kuleta nafuu havipo. Pamoja na hayo wamekuwa wanachapa kazi usiku na mchana kujenga na kukipigania Chama cha Mapinduzi. Moyo wao wa kujitolea unastahili kutambuliwa na kupongezwa. Siku ile ya tarehe 25 Juni, 2006 nilipochaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa Mwenyekiti wa Chama chetu niliahidi kuboresha maslahi ya wafanyakazi wa CCM. Nilitimiza ahadi yangu. Hata hivyo kwa vile tumeshindwa kuendelea kuboresha mishahara kila wakati Serikali ilipoongeza kima cha chini cha mishahara kwa wafanyakazi nchini hali ya watumishi wa Chama imeendelea kuwa ngumu.
Sipendi kumsemea Mwenyekiti mpya na wala kumtaka atoe kauli ya matumaini siku ya leo. Lakini, ni jambo muhimu ambalo halina budi kutazamwa mapema iwezekanavyo. Ilikuwa dhamira yangu kabla ya kuondoka tutoe nyongeza ya mishahara lakini mipango haikwenda kama tulivyotarajia.
Shukrani kwa Wajumbe wa Mkutano Mkuu
Ndugu Wajumbe,
Niruhusuni nitoe neno la shukrani kwenu, kwa imani kubwa mliyoionyesha kwangu. Mara zote tatu yaani 2006, 2007, na 2012 jina langu lilipoletwa mbele yenu kunipigia kura ya kuwa Mwenyekiti mlinipa kura nyingi mno. Wingi ule wa kura ndiyo ulionidhihirishia upendo wenu na imani yenu kwangu. Mambo hayo ndiyo yaliyonitia moyo na kunipa nguvu ya kukitumikia Chama kwa nguvu zangu zote na kwa kutumia vipaji vyangu vyote nilivyojaaliwa na Mwenyezi Mungu. Ombi langu kwenu leo tufanye zaidi ya vile mlivyofanya kwangu kwa ndugu yetu , Rais wetu mpendwa Mheshimiwa John Pombe Magufuli. Tumpigie kura zote za Ndiyo. Isipotee hata kura moja. Je tutafanya hivyo wajumbe wenzangu? Hebu nithibitishieni! Tumekubaliana. Atakayefanya kinyume ni Mchawi? na wachawi hawapo!
Kuimarisha Chama
Ndugu Wajumbe,
Mtakumbuka kuwa katika hotuba yangu ya kushukuru baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Nne wa Chama cha Mapinduzi tarehe 25 Juni, 2006 nilizungumzia kwa kirefu umuhimu wa kuendelea kufanya kazi ya uimarishaji wa Chama. Nilikimithilisha Chama chetu na mwili wa mwanadamu kuwa na viungo. Kama ilivyo mwanadamu kama kiungo kimoja wapo kikikosekana huitwa mlemavu na kikipata maradhi huitwa mgojwa. Nilisisitiza umuhimu wa viungo vya Chama kutimia na kufanya kazi vizuri.
Ndugu Wajumbe,
Nilivitaja viungo vya CCM kuwa sita yaani Wanachama, Viongozi, Vikao, Watendaji, Rasilimali na Jumuiya. Nilifafanua kwa kina na upana mambo ya kufanya katika azma yetu ya kuimarisha Chama. Chini ya uongozi mahiri na makini wa Katibu Mkuu wa CCM Lt. Yusuph Makamba ulitengenezwa Mradi wa Kuimarisha Chama Awamu ya Tatu uliozinduliwa Oktoba 2006. Katika historia ya Chama hii ilikuwa mara ya tatu kuwa na Mradi wa namna hiyo. Mradi wa Kwanza ilikuwa mwaka 1961, Mwalimu alipojiuzulu Uwaziri Mkuu na kufanya kazi ya kuimarisha Chama. Wa pili ilikuwa mwaka 1987 Mwalimu Julius Nyerere Mwenyekiti wa Kwanza wa CCM, aliobuni na kutekeleza chini ya uongozi wake baada ya kustaafu Urais.
Ndugu Wajumbe,
Leo miaka kumi baadae ninaponga’atuka napenda kutoa taarifa fupi ya hatua tuliyofikia katika uimarishaji wa Chama.Kufanya hivyo kutamsaidia Mwenyekiti mpya kujua mahali tulipo na hasa pale pa yeye kuanzia katika kazi hii mama na ya msingi kwa uhai na ustawi wa Chama chetu. Kazi ya kuimarisha Chama ni ya kudumu na ni ya kila siku kwa Viongozi na Wanachama. Ni kazi endelevu. Tunapoifanya kwa ufanisi mambo yote yanakuwa mazuri na taswira ya CCM katika jamii inakuwa nzuri. Imani iliyoonyeshwa na Watanzania kwa Chama chetu katika uchaguzi uliopita ilitokana na Watanzania kuona mafanikio tunayoendelea kuyapata katika dhamira yetu ya kurekebisha baadhi ya mambo waliyokuwa hawayapendi kuhusu Chama chetu.
Wanachama
Ndugu Wajumbe,
Kwa upande wa wanachama tumepata mafanikio makubwa. Watanzania wengi wamejiunga na Chama cha Mapinduzi kuthibitisha kukubalika na kuaminika kwa Chama chetu. Hivi sasa CCM ina wanachama 8,782,833 ukilinganisha na 5,433,325 waliokuwepo mwaka 2006. Hili ni ongezeko kubwa sana. Jambo la kutia faraja kuhusu wanachama wa CCM ni moyo wao wa kukipenda Chama chao na kukipigania kwa nguvu zao zote. Wamedhihirisha hivi katika chaguzi zote. Wanachama wa CCM ni rasilimali na mtaji mkubwa katika uchaguzi. Wanachama wetu ni kura nyingi za kuanzia. Wanachama wetu wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kuomba kura kwa wananchi wengine. Hivyo basi, kazi ya kuingiza wanachama wapya haina budi kuendelea na kuendelezwa kwa bidii na maarifa zaidi.
Ndugu Wajumbe,
Kuna mambo mawili ambayo wanachama wetu wanatakiwa kujirekebisha kwa maslahi ya Chama cha Mapinduzi sasa na mbele tuendako. Jambo la kwanza linahusu ushiriki wao katika vikao kutokuwa wa kiwango cha kuridhisha. Kwa sababu hiyo wanachama wanakosa au kujinyima fursa ya kuzungumzia mambo yenye maslahi kwa Chama chao na nchi. Lazima wana-CCM watambue kuwa uhai na vuguvugu la Chama linakuwepo pale wanachama wanapokutana kuzungumza na kukubaliana jambo na mambo ya kufanya. Wasipokutana inakuwa kila mtu na lwake na wengine kutokushughulika kabisa. Hii haikubaliki na isiachwe kuendelea.
Pia kwamba, kwa vile Serikali ni ya CCM wanachama wanao wajibu wa kiuongozi katika maeneo yao wanayoishi. Wanapokutana kwenye vikao vya Chama wanao wajibu wa kuzungumza mambo ya Chama, utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi na masuala yanayohusu maendeleo na matatizo ya wananchi katika eneo lao. Kwa vile wao ndiyo Chama tawala ni rahisi kuwasiliana na mamlaka husika za Serikali kutoa taarifa, kuuliza maswali na kupata majibu. Wakifanya hivyo na hatua zikachukuliwa au kuwapatia wananchi majibu na ufumbuzi wa matatizo yao, wanajenga imani kwa CCM na Serikali yake. Kwa ajili hiyo, inaifanya kazi ya CCM kuwa nyepesi wakati wa uchaguzi.
Ndugu Wajumbe,
Jambo la pili ni wanachama kutokulipa ada na michango ya kuimarisha Chama. Kutokufanya hivyo kunakipunguzia Chama chetu uwezo wa kutekeleza ipasavyo majukumu yake. Kwa idadi hii ya wanachama CCM haingestahili kuwa na matatizo ya fedha wakati wote. Ada ya uanachama peke yake ingeipatia CCM zaidi ya shilingi bilioni 10.5 kwa mwaka. Zingetuwezesha kufanya mambo mengi sana. Lakini wanachama wengi hawalipi ada. Kwa mfano, katika bajeti ya Chama iliyopita ilikadiriwa kupata shilingi 800 milioni kutokana na ada lakini zilizopatikana ni milioni 500 tu. Hili ni jambo baya ambalo halikubaliki hata kidogo na hatuwezi kuliacha kuendelea.
Mheshimiwa Mwenyekiti unaesubiri kuthibitishwa, nakuachia kazi hii. Tumia maarifa na ujuzi wako kupata ufumbuzi wa matatizo ya wanachama kushiriki vikao vya Chama vinavyowahusu, walipe ada zao na kutoa michango ya kuimarisha Chama.
Viongozi
Ndugu Wajumbe,
Kwa upande wa viongozi nafurahi kwamba namaliza ngwe yangu safu ya uongozi ikiwa imekamilika katika ngazi zote isipokuwa pale ambapo kuna mapengo yaliyotokana na vifo hivi karibuni. Nafurahi pia, kwamba mapengo yaliyotokana na baadhi ya viongozi kufariki, kuachishwa uongozi au kuhama Chama na kujiuzulu siku za nyuma yamekwishazibwa. Viongozi wa Chama wanastahili pongezi maalum kwa uongozi wao nzuri. Mwaka jana walithibitisha uhodari na ushupavu wao katika kuhakikisha CCM imeibuka kidedea kutokana na jinsi walivyowaongoza wanachama na wananchi.
Pamoja na hayo kuna mambo mawili kuhusu viongozi wa CCM ambayo ningependa kuyasemea. Kwanza, kwamba viongozi wetu wamekuwa wazito kutoka na kwenda kwa wanachama na wananchi. Kwa sababu hiyo kazi ya Chama ndani ya Chama na kazi ya Chama nje ya Chama ndani ya Umma hazifanyiki ipasavyo. Siasa ni kufikisha ujumbe kwa watu wakuunge mkono. Hivi usipotoka watu wakakuona na kukusikia wanakuungaje mkono? Lazima tujirekebishe.
Ndugu Wajumbe,
Siku za nyuma viongozi walilalamikia kukosa magari mazuri, tumewaletea Toyota Land Cruiser Hardtop kila Mkoa na kila Wilaya. Tena zenye uwezo wa kubeba viongozi wengi kwa wakati mmoja. Pia tumesambaza pikipiki na baiskeli nyingi. Lakini, bado viongozi hawatoki na wengine wamediriki hata kudai hawana hela ya mafuta au hata ya kununulia matairi na kulipia bima ya magari. Kwa kweli inaudhi na kukatisha tamaa. Hivi ndugu zangu mnataka Makao Makuu waliowanunulia hizo gari ndiyo waje kuwapatia na hela za mafuta, bima, kubadili matairi na matengenezo ya kawaida. Waswahili wana msemo “ukibebwa shikilia” baadhi yenu mmejilegeza mno kiasi cha kufanya tuwe tunaulizana swali la kulikoni bila ya majibu sahihi. Je ni kutokujua wajibu, woga, uzembe au kutokuwa na mapenzi ya dhati na CCM?
Ndugu Wajumbe,
Jambo baya na la kusikitisha ni kwamba, wakati viongozi wetu wa CCM hawaendi kwa wanachama na wananchi, wenzetu wa vyama vya watani zetu wanatoka. Matokeo yake ni kuwapa fursa ya kujijenga kwa kupotosha wananchi na kuifanya kazi ya uchaguzi kuwa nzito bila ya sababu. Tunalazimika kutumia nguvu kubwa kutafuta ushindi isivyokuwa lazima. Kwa huko mbele tuendako lazima viongozi wa CCM wabadilike. Tusipobadilika na kufanya kazi na wanachama wetu na miongoni mwa wananchi mambo yanaweza kutuharibikia, balaa ambalo hatutaki litokee.
Ndugu Rais na Mwenyekiti mtarajiwa,
Nakuomba uitambue hali hii wakati unapopokea kijiti cha kukiongoza Chama chetu. Tusiiache ikaendelea. Naomba uchune bongo na kama hapana budi kufanya kazi ya ziada kuipatia ufumbuzi thabiti. Kwa kweli hapa ndipo ninaporudia kumpongeza kwa dhati, Katibu Mkuu Ndg. Abdulrahman Kinana kwa kuonyesha mfano kwa vitendo jinsi viongozi wa Chama wanavyotakiwa kuwa. Kila alipotembelea Wilaya na Mikoa alikutana na kuzungumza na wanachama na wananchi katika maeneo yao. Naambiwa baadhi ya viongozi wa maeneo hayo ilikuwa ndiyo mara yao ya kwanza kufika. Wamekuwa wanashangaa jinsi wanachama na wananchi walivyokuwa wanajitokeza kwa wingi na kufurahia kutembelewa na kusikilizwa. Jambo la kushangaza ni kwamba badala ya kuendeleza utaratibu wanarudia kutotoka na kuomba Katibu Mkuu au Katibu wa Itikadi na Uenezi Ndg Nape Nnauye afanye ziara nyingine.
Vikao.
Ndugu Wajumbe,
Vikao ni kitu muhimu sana katika uhai na ustawi wa Chama cha Mapinduzi. Vikao ndicho chombo kikuu cha uamuzi na uendeshaji wa Chama kwa mujibu wa Katiba ya Chama cha Mapinduzi. Mfumo wa Chama umejengeka juu ya vikao kufanya uamuzi na siyo kiongozi binafsi. Hata Mwenyekiti au Katibu anapotaka jambo lake sharti alifikishe kwenye kikao kwa uamuzi isipokuwa yale ambayo ni utekelezaji wa maamuzi ya vikao vilivyopita au Katiba ya Chama imewapa mamlaka ya kufanya hivyo. Na, kwa vyo vyote vile hayatakuwa mambo yahusuyo kubadili itikadi na sera za msingi za Chama au kubadili masharti ya Katiba ya Chama. Mambo ya namna hiyo huletwa kwenye kikao na wajumbe hupewa fursa na uhuru wa kujadili na kuamua wanavyoona inafaa.
Ndugu Wajumbe,
Kwa sababu ya umuhimu huo wa vikao katika uamuzi na uendeshaji wa Chama kufanyika kwake kwa mujibu wa Katiba ni jambo la msingi sana. Ndiyo maana kila mwaka Chama hutoa ratiba ya vikao vya Chama kwa ngazi zote kama mwongozo kwa wote. Taarifa zinaonesha kuwa hali ya ufanyikaji wa vikao vya kawaida vya Chama ni ya wastani na kwa baadhi ya ngazi ni chini ya wastani. Kuna kujitokeza tabia ya vikao maalumu hasa vile vihusuvyo uteuzi wa wagombea na uchaguzi hufanyika kama inavyotakiwa. Hali hii si nzuri kwa ustawi wa Chama. Unakifanya Chama chetu kiwe hai wakati wa uchaguzi na siyo wakati wote kabla, wakati na baada ya uchaguzi. Hali hii haifai kuachwa kuendelea kwani inakinyima Chama chetu fursa muhimu ya kujijenga na kujiimarisha. Upungufu huu lazima utafutiwe ufumbuzi kwa maslahi mapana ya Chama chetu. Hatuwezi kusubiri mpaka wakati wa mchakato wa uchaguzi. Ipo siku tunaweza kujikuta tumezingirwa kila upande tukashindwa kujinasua au kukosa pa kuchomokea.
Watendaji wa Chama
Ndugu Wajumbe,
Kwa Chama cha Mapinduzi kuwa na watendaji wazuri ni jambo lenye umuhimu wa aina yake kwa ustawi na uhai wa Chama. Inatoa uhakika kwamba kumbukumbu za vikao, fedha na mali za Chama zitaandikwa na kuhifadhiwa vizuri. Pili kwamba mipango na shughuli za kiutawala za Chama zitaendeshwa vizuri. Watendaji wa Chama wanapokosekana au wanapokuwa ni wa kiwango cha chini cha ubora ni hasara kwa Chama. Uwezo wa Chama kutimiza wajibu wake unakuwa umedhoofika sana. Kwa vile CCM ni Chama cha siasa tena katika mfumo wa vyama vingi watendaji wake siyo tu wawe hodari kwa kazi zao bali lazima pia wawe waumini wa dhati wa sera, siasa, imani na madhumuni ya Chama cha Mapinduzi.
Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita tumechukua hatua za maksudi za kuajiri vijana wasomi katika utumishi wa Chama. Msimamo huu ukiendelezwa baada ya muda si mrefu tutakuwa na watumishi wasomi katika kada zote ngazi za Wilaya, Mkoa na Taifa. Jumuiya za Chama nazo zihimizwe kufanya hivyo. Jumuiya ya Vijana iko mbele ya Jumuiya za Wanawake na Wazazi kwa hili. Lazima, zisisitizwe kubadilika kwani huko mbele tuendako elimu ya watendaji na viongozi wetu ni sifa na mtaji muhimu. Pamoja na hayo Chama kiendelee kuelimisha watendaji wake kuhusu namna ya kufanya kazi ya Chama.
Rasilimali za Chama
Ndugu Wajumbe,
Nilipozungumzia rasilimali kama moja ya viungo vikuu vya Chama cha Mapinduzi nilizungumzia Chama kuwa na majengo ya ofisi mazuri yanayolingana na hadhi ya Chama kikubwa kama CCM. Pia nilizungumzia Chama kuwa na fedha za kutosha za kuendesha shughuli zake, vitendea kazi, na miradi ya kiuchumi ya kukipatia fedha. Leo miaka 10 baadae ninapomaliza kipindi changu cha uongozi kwa upande wa Makao Makuu tumekamilisha ujenzi wa ukumbi wa mikutano ambao ndiyo huu. Tumejenga jengo jipya zuri na la kisasa katika Ofisi Ndogo ya Makao Makuu, Dar es salaam na ukarabati mkubwa unaendelea kufanyika Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui pamoja na kuweka samani mpya. Kwa hapa Dodoma kazi ambayo haijakamilika ni ujenzi wa jengo la Ofisi ya Makao Makuu na jengo la kitega uchumi. Kazi hiyo sasa namuachia Mwenyekiti mpya na safu ya uongozi atakayoiunda. Hali kadhalika, majengo mazuri ya Ofisi yamejengwa katika Mikoa, Wilaya, Majimbo, Kata na Matawi kote nchini. Kila Ofisi ya Wilaya na Mikoa imepatiwa gari na pikipiki zipo katika baadhi ya Ofisi za Wilaya, na Kata. Matawi mengi yamepatiwa baiskeli.
Lakini sina budi kusema mbele yenu kuwa tumshukuru na kumpongeza Katibu Mkuu Ndugu Abdulrahman Kinana kwa ubunifu wake. Ni mtu aliyebobea kwa mikakati na mipango. Siyo tu imetuwezesha kujenga huu ukumbi lakini pia imetuwezesha kupata hayo magari, pikipiki, baiskeli na mahitaji mengine muhimu ya kuendesha Chama kabla, wakati na baada ya kampeni za uchaguzi.
Ndugu Wajumbe,
Changamoto yetu kubwa ambayo lazima nikiri sikuweza kuipatia jawabu la kudumu na endelevu ni Chama kukosa vyanzo vya uhakika vya kujipatia rasilimali fedha. Kwa sasa chanzo kikubwa na cha uhakika cha mapato kwa Chama chetu ni ruzuku ya Ubunge na Udiwani. Aghalab fedha hizo zote hutumika kulipia mishahara ya watendaji na watumishi wa Chama. Fedha kwa ajili ya kuendeshea shughuli nyingine muhimu za Chama kama vile vikao au ziara za viongozi kuhamasisha uhai wa Chama na kuimarisha Chama upatikanaji wake si wa uhakika. Mara kadhaa imebidi hata Mwenyekiti uingilie kati kutafuta ndipo baadhi ya shughuli muhimu zifanyike.
Nikuombe Mwenyekiti Mtarajiwa kwamba suala la Chama kuwa na vyanzo vya uhakika vya mapato ulipe kipaumbele cha juu. Hali kadhalika uendelee kuwabana viongozi wa Mikoa na Wilaya kutilia maanani uanzishwaji wa mifuko ya uchaguzi. Utekelezaji wake unasuasua. Napata shaka kwamba viongozi wetu wengi hawaoni umuhimu wa kufanya hivyo. Naona kama vile wamejenga dhana potofu ati kuwa yupo mwenye Chama chake ambae ni Chama ngazi ya Taifa. Wao wanajifanya kana kwamba hawahusiki. Hata maagizo ya kuanzisha shughuli za kiuchumi Chama kijitegemee hayatiliwi maanani. Kama yangelitiliwa maanani CCM isingekuwa katika hali ngumu ya kifedha iliyopo sasa.
Ndugu Wajumbe,
Chama kina rasilimali nyingi ambazo zikitumika zinaweza kuboresha sana hali yake ya kifedha. Mkoani Dar es salaam kwa mfano, Chama kina jumla ya viwanja 279 katika ngazi mbalimbali. Vingeweza kuwa chanzo muhimu cha miradi ya kiuchumi kama wafanyavyo watu wengine binafsi wenye viwanja. Umoja wa Vijana wameonesha mfano mzuri wa kutumia viwanja kujenga majengo makubwa ya kitegauchumi. UWT nao wamefanya hivyo. Naamini wengine nao wangeweza kuiga mifano hiyo mizuri. Jambo lililo muhimu ni kuhakikisha wanakuwa na mikataba mizuri pale wanapoingia ubia. Mimi naamini tukichangamkia uwekezaji na kuitumia vyema rasilimali ya viwanja na ardhi tuliyonayo CCM inaweza kabisa kujiondolea unyonge wa uhaba wa fedha. Zoezi la uhakiki wa viwanja vya Chama linahitaji kupewa msukumo maalum linakwenda pole pole mno. Kukamilika kwake ndiko kutatoa uhakika wa milki ya CCM kwa viwanja hivyo. Isijekuwa watu wameshajimilikisha au kuviuza viwanja hivyo kinyemela.
Jumuiya za Chama
Ndugu Wajumbe,
Kuhusu Jumuiya za Chama nilifafanua, siku ile na mara kadhaa kwamba zina jukumu na wajibu maalum kwa Chama. Nao ni kukitafutia Chama wanachama, marafiki, wapenzi na watu wa kukiunga mkono na kukipigia kura wakati wa uchaguzi kutoka katika jamii pana ya Watanzania. Pamoja na kuwepo kwa changamoto za hapa na pale Jumuiya za Chama zimekuwa zikitimiza vizuri majukumu yake hayo. Hata Jumuiya ya Wazazi ambayo iliamuliwa ifutwe kwa sababu ya kutoridhishwa na kazi zake safari hii imejitahidi. Alhaj Abdallah Bulembo Mwenyekiti wa Wazazi amefanya kazi nzuri sana inayostahili pongezi. Hata hivyo wajue kuwa uamuzi ule haujafutwa, hivyo waendelee kujitengenezea uhalali. Na pengine la haraka zaidi ni lile la Shule za Wazazi ambazo haziendeshwi vizuri. Chama kiliagiza ziuziwe Serikali Kuu au Halmashauri lakini bado kuna uzito wa kufanya hivyo. Inatoa sura na sifa mbaya kwa Jumuiya ya Wazazi na Chama chenye Jumuiya yake.
Ndugu Wajumbe,
Bahati mbaya, Jumuiya bado zimeendelea kuwa tegemezi kwa CCM kulipa mishahara ya watendaji na watumishi wao. Hata pale walipokuwa na miradi ya kuwaingizia mapato kama walivyo UWT na UVCCM kwa majengo na Wazazi kwa shule zake hawakuacha kuomba na kupokea ruzuku kutoka CCM. Pengine wakati umefika kusisitiza Jumuiya za Chama ziendelee kuchukua hatua za kujitegemea na kuanza kuchangia katika mapato ya Chama cha Mapinduzi.
Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu
Ndugu Wajumbe,
Katika kipindi hiki pia tulianzisha Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu. Moja ya sifa ya Chama makini cha siasa kama CCM, kinachohitaji kudumu katika uongozi, ni kutayarisha kada ya viongozi wapya, wenye sifa na maono ya nyakati zinazokuja. Chama chetu kinayo Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM ambao kwa miaka mingi limekuwa tanuru la kupika viongozi wa Chama chetu na taifa letu. Hata hivyo, kwa kuzingatia ongezeko kubwa la wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, na kwa kuzingatia kwamba vyuoni ndiko kumekuwa na harakati kubwa za kisiasa, Ndipo tulipoamua kuanzisha Shirikisho hilo. Hii ilikuwa sehemu ya mageuzi ya ndani ya Chama na madhumuni yake ni kuhakikisha kwamba tunapata wanachama wapya na kuungwa mkono na kundi hili muhimu la wasomi katika nchi yetu. Pia ni fursa ya aina yake ya kutayarisha viongozi wajao wa CCM na Taifa kutoka miongoni mwao.
Ndugu Wajumbe,
Faida za kuwepo kwa Shirikisho hili zimeanza kuonekana. Kwanza kabisa imeondoa dhana potofu iliyokuwepo zamani eti kwamba wasomi wa vyuo vya elimu ya juu wanapenda upinzani zaidi kuliko CCM. Chama chetu kimevuna wanachama wengi zaidi na kina washabiki wengi zaidi kwenye vyuo. Pili katika uchaguzi uliopita Shirikisho limefanya kazi kubwa na nzuri ya kuhamasisha jamii kuiunga mkono CCM. Napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza viongozi wa Shirikisho na Mlezi wake Ndugu January Makamba, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa, kwa kuliwezesha Shirikisho kufika hapo lilipo na kusimama imara. Sisi viongozi wa Chama tuendelee kuchukua hatua ya kuliwezesha Shirikisho hilo liendelee kuwalea vijana hawa wa CCM.
Uwezo wa Chama Kutumia TEHAMA
Ndugu Wajumbe,
Katika mambo yenye tija ambayo tumeyafanya katika mageuzi ya ndani ya CCM ni pamoja na kujenga uwezo wa Chama chetu kuingia katika ulimwengu mpya wa teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA). Pamoja na ukongwe wake, matumizi ya TEHAMA yamefanya Chama chetu kiende na wakati na kiwafikie watu wengi na hasa vijana. Uwekezaji wa miundombinu ya kisasa ya TEHAMA katika Ofisi Ndogo ya Lumumba umewezesha mawasiliano na usambazaji wa taarifa kwa haraka na umekiwezesha Chama chetu kupambana vyema na kuleta uwiano wa nguvu za mapambano ya kimtandao. Nyote mlishuhudia katika uchaguzi mkuu uliopita jinsi nguvu ya CCM ilivyojidhihirisha mitandaoni. Uwezo huo tumeujenga katika kipindi hiki kifupi. Kwa uwezo wetu huu, taarifa za Chama chetu zina uwezo wa kuwafikia watu zaidi ya milioni na kuendelea kwa wakati mmoja, popote walipo. Hii ni zaidi ya watu wanaosoma magazeti na kuangalia TV hapa nchini.
Vyombo vya Habari vya Chama
Ndugu Wajumbe,
Ufanisi wa Chama chochote cha siasa kueneza sera zake, malengo yake, shabaha zake na mafanikio yake kwa jamii unachangiwa kwa kiasi kikubwa na uwezo wake wa kuwasiliana na umma. Pamoja na kutumia TEHAMA, Chama chetu kinavyo vyombo vyake vya habari kwa ajili hiyo. Tuna magazeti mawili ya Uhuru na Mzalendo na Radio mbili yaani, Uhuru fm na Bahari Fm. Vyombo vyetu hivyo vimekuwa vinafanya kazi kubwa na nzuri ya kueneza ujumbe wa CCM kwa umma. Hata hivyo vimekuwa vinakabiliwa na changamoto mbalimbali za uendeshaji zinazovifanya visifikie pale tunapopakusudia. Katika kipindi cha uongozi wangu wa Chama chetu, tumechukua hatua mbalimbali za kuimarisha vyombo vya habari vya CCM.
Ninayo furaha kuwajulisha kwamba tunanunua mtambo mpya wa uchapishaji ambao utaimarisha magazeti yetu na kufanya kazi za watu wengine kibiashara. Radio Uhuru, tumeiongezea uwezo wa vifaa, fedha na rasilimali-watu ili isikike maeneo mengi zaidi hapa nchini. Hata hivyo mipango iko mbioni kuijengea uwezo mkubwa zaidi wa kusikika kwa urahisi zaidi kote nchini. Mwaka jana tumefungua redio mpya inayoitwa Bahari FM kule Zanzibar ambayo nayo tumedhamiria kuiboresha zaidi.
Sambamba na vyombo hivi, tumeendelea na mpango wa kufungua Televisheni ya Chama, ambapo hatua mbalimbali za utangulizi zimekamilika ikiwemo ya kupata leseni ya matangazo. Matayarisho ya kuiwezesha TV yetu irushe matangazo mapema iwezekanavyo yanaendelea. Sina wasiwasi kwamba Mwenyekiti ajae atatoa msukumo mkubwa zaidi.
Mafunzo ya Uongozi, Siasa na Itikadi
Ndugu Wajumbe,
Chama imara ni kile chenye makada, viongozi na watendaji waliopikwa na kufundwa wakaiva vizuri katika elimu ya siasa, itikadi ya Chama, uongozi na mbinu na mikakati ya ushindani wa kisiasa. Katika miaka kumi iliyopita tumeongeza kwa kiasi kikubwa idadi ya makada na viongozi waliopata mafunzo ndani na nje ya nchi. Kwa hapa ndani tumekuwa tunatumia Chuo cha Ihemi na semina na warsha mbalimbali kutoa mafunzo kwa makada wetu. Kupitia ushirikiano wetu na Chama cha Kikomunisti cha China tumepeleka makada wa Chama 80 kwa mafunzo nchini China.
Ndugu Wajumbe,
Niliahidi kwamba nitajitahidi kwa kadri ya uwezo wangu Chama chetu kiwe na Chuo chake pale Ihemi, kutoa mafunzo kwa viongozi na makada wa Chama. Juhudi za kukiimarisha Chuo cha Ihemi zinaendelea. Ninayo furaha kuripoti kwenu pia kwamba tumekamilisha taratibu za kujenga chuo kikubwa cha kimataifa kwa ajili ya kutoa mafunzo kwa makada wa Chama. Chuo hicho kitajengwa Kibaha kwa kushirikiana na vyama rafiki vya ukombozi yaani FRELIMO, MPLA, ZANU PF, SWAPO, na ANC na marafiki zetu wa Chama cha Kikomunisti cha China. Makada wetu na wa vyama hivyo watapatiwa mafunzo katika Chuo hicho ambacho kitakuwa na ubora wa kimataifa.
Hii ni hatua muhimu sana kwani sasa tutajenga kada ya viongozi na watendaji wa Chama walioandaliwa vizuri kisiasa , kiitikadi, uendeshaji wa shughuli za Chama, uchaguzi na kwa mambo mbalimbali ya dunia ya sasa. Kuwepo kwa Chuo hicho kutaimarisha sana viongozi, watendaji na makada wa CCM na vyama rafiki.
Ushindi Katika Chaguzi Mbalimbali
Ndugu Wajumbe,
Katika kipindi cha miaka 10 mliyonipa heshima ya kuwa Mwenyekiti, Chama chetu kimeshiriki Uchaguzi Mkuu mara mbili yaani 2010 na 2015 na marudio ya mwaka 2016 kwa Zanzibar. Katika chaguzi zote hizo tumefanikiwa kutimiza madhumuni ya Ibara 5 (i) kwa kushinda uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi na kupata viti vingi vya Wabunge, Wawakilishi na Madiwani. Kwa ajili hiyo tumeweza kuendelea kukamata dola kwa sehemu zote mbili za Muungano. Katika kipindi hicho pia tulishiriki katika chaguzi mbili za Serikali za Mitaa kwa upande wa Tanzania Bara na kupata ushindi mkubwa sana. Katika uchaguzi wa viongozi wa mitaa, vijiji na vitongoji mwaka 2009 tulipata ushindi wa 91.72% na mwaka 2014 tulipata 80.58%. Nani kama CCM?
Ndugu Wajumbe,
Katika kipindi hiki pia, tulishiriki katika chaguzi ndogo za Ubunge katika Majimbo manane ya Kiteto, Tunduru, Tarime, Busanda, Mbeya Vijijini, Biharamulo Magharibi, Igunga na Arumeru Mashariki. Pamoja na ushindani mkali uliokuwepo tulishinda katika majimbo sita. Pia tulishiriki katika chaguzi ndogo za udiwani katika Kata 31, na tulishinda katika Kata 25 kati ya hizo. Nani kama CCM?
Ndugu Wajumbe,
Ushindi tuliopata katika chaguzi zilizofanyika katika ya kipindi cha miaka 10 ya uongozi wangu ni ishara tosha kwamba CCM imeongoza vizuri nchi yetu na Chama chetu kimeendelea kuaminiwa na kukubalika kwa Watanzania. Pia ni ushahidi wa ubora wa mikakati na mipango yetu ya uchaguzi pamoja na umahiri na umakini wa Viongozi na Wanachama wa CCM katika utekelezaji. Napenda kuchukua fursa hii kurudia kuwapongeza viongozi, wanachama, makada, washabiki na wapenzi wa CCM kote nchini kwa kazi nzuri waliyoifanya katika kukipigania na kukipatia ushindi Chama chetu. Napenda pia kuwashukuru Watanzania kwa kuendelea kuonyesha imani kubwa kwa Chama cha Mapinduzi. Nani kama CCM.
Ndugu Wajumbe,
Kwa kweli, ninaona fahari kwamba, wakati namaliza ngwe yangu ya uongozi, CCM imeendelea kuwa madarakani sehemu zetu zote mbili za Muungano. Malengo na madhumuni ya msingi ya kuundwa kwa CCM ya kushinda chaguzi na kushika dola Tanzania nzima na Zanzibar yametimia. Kazi hii sikuifanya peke yangu. Tumeifanya wote. Ushindi tulioupata chini ya Uenyekiti wangu, haukuwa ushindi wangu binafsi bali ni ushindi wa Chama cha Mapinduzi. Ushindi wa viongozi, wanachama na wapenzi wa CCM. Ni matunda ya kazi nzuri tuliyofanya ya kujenga viongozi, makada, watendaji na wanachama wenye uwezo na uzoefu wa kuendesha chaguzi. Tumejenga mikakati, mbinu na miundombinu ya kutafuta ushindi, ambayo imeweka msingi imara kwa ushindi wa Chama chetu kwa miaka mingi ijayo.
Ilani ya Uchaguzi
Ndugu Wajumbe,
Ni mazoea ya Chama cha Mapinduzi kushindana katika chaguzi za dola kwa hoja. Kwa kawaida hoja za Chama chetu huandikwa na kuchapishwa katika Ilani ya Uchaguzi kwa Uchaguzi Mkuu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, Wabunge, Wawakilishi na Madiwani. Kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa upande wa Tanzania Bara, CCM imekuwa inatoa kijarida kinachoitwa Tamko la CCM kuhusu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Maandiko hayo mawili huelezea nia na makusudio ya Chama cha Mapinduzi kushiriki katika chaguzi hizo. Aidha Chama hufafanua mambo ambayo kinakusudia kuyafanya kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu na watu wake iwapo tutapata ridhaa ya kuongoza. Wagombea wa Chama pamoja na Viongozi, wanachama na wapenzi wa CCM hutumia maandiko hayo katika kuomba kura kwa wananchi.
Baada ya Uchaguzi, na hasa baada ya kushinda CCM huwa makini katika kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi na Tamko la CCM. Katika kufanya hivyo Chama huwataka Viongozi wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa ambao ndiyo wana dhamana ya utekelezaji kutengeneza mkakati na mipango ya utekelezaji na kutoa taarifa ya utekelezaji kwenye vikao vya Chama vya ngazi husika, yaani Wilaya, Mkoa na Taifa. Ni wajibu wa Serikali katika ngazi zote husika kutoa taarifa ya utekelezaji. Huo ni wajibu na wala sio hiyari au ihsani wanayoifanyia CCM. Ni kutokana na wajibu huo ndio maana Rais, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano pamoja na Rais wa Zanzibar na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ni Wajumbe wa Kamati Kuu, Halmshauri Kuu ya Taifa na Mkutano Mkuu wa Taifa wa CCM. Hali kadhalika, Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya ni Wajumbe wa Kamati za Siasa, Halmashauri Kuu za Chama na Mikutano Mikuu ya Chama katika ngazi zao husika. Viongozi hao wakuu wa Serikali ndio makamisaa wa Chama na kiungo kati ya Chama tawala na Serikali katika ngazi zao husika za uongozi.
Ndugu Wajumbe,
Kuwa na ilani nzuri na utekelezaji mzuri wa Ilani na ahadi za viongozi wa Serikali na Chama ndio siri kubwa ya CCM kuendelea kuaminiwa, kukubalika na hivyo kuchaguliwa kuendelea kuongoza nchi yetu. Wosia wangu kwa Mwenyekiti mpya, Makamu Mwenyekiti Zanzibar pamoja Viongozi na Wanachama wenzangu wa CCM ni kudumisha na kuendeleza utaratibu huu nzuri wa Chama kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM unaofanywa na Serikali zake. Ni jambo lenye manufaa na maslahi makubwa kwa Chama chetu.
Ndugu Wajumbe,
Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Mwaka 2015 – 2020 uko mikononi kwa Mheshimiwa Dr John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa mambo ya muungano na Tanzania Bara. Kwa mambo yahusuyo Zanzibar uko mikononi mwa Mheshimiwa Dr Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi ambaye yupo katika kipindi chake cha pili.
Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndiyo kwanza ameanza bahati nzuri ameanza vizuri. Kwa kweli tumembebesha mzigo mkubwa sana kwenye Ilani hii na hivyo ana kazi kubwa ya kutafuta rasilimali. Ninachomshukuru na kumpongeza ni kwamba ameupokea mzigo huo kwa moyo mkunjufu na anatekeleza kwa ari, nguvu na kasi kubwa. Amefanya uamuzi sahihi kabisa kwa kutoa msukumo maalum kwa upande wa kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya Serikali kwani bila ya kufanya hivyo utekelezaji wa Ilani utakuwa mashakani. Wajibu wetu katika Chama ni kuwaunga mkono na kuwasaidia ili wafanye kazi yao vizuri, kwa moyo na ufanisi. Nawaomba Watanzania wenzangu tuwe na moyo wa subira na kumpa nafasi Rais wetu kutekeleza malengo aliyojiwekea kwa manufaa ya nchi yetu na watu wake.
Hitimisho
Ndugu Mwenyekiti Mtarajiwa,
Hiyo kwa muhtasari ndiyo hali ya uhai wa Chama wakati ninapomaliza ngwe yangu ya uongozi na kukabidhi kijiti kwako. Tulipanga kufanya mengi na tumefanikiwa mengi ingawaje bado yapo mambo hatukuweza kuyafanya. Kimsingi, kazi ya ujenzi wa Chama au nchi haifanani na kazi ya ujenzi wa nyumba au daraja ambayo ina mwanzo na ukomo. Kazi hii haiishi. Hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa Rais na Mwenyekiti wetu wa kwanza, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na ndivyo ilivyokuwa kwa Rais na Mwenyekiti wa Pili Ali Hassan Mwinyi. Hali ilikuwa hivyo kwa Rais na Mwenyekiti wa Tatu Benjamin Mkapa aliponiachia. Na ndivyo ilivyokuwa kwangu nilipomwachia Mhe Dkt. John Pombe Magufuli, Urais na sasa ninapomuachia Uenyekiti wa CCM. Na ndivyo itakavyokuwa kwako Mheshimiwa Rais utafanya yako na hutayamaliza yatakayobakia atamwachia Rais na Mwenyekiti atakayemfuatia, mwaka 2025. Jambo linalonipa faraja kama ilivyokuwa kwa viongozi walionitangulia ni kuwa name nimepata fursa ya kutoa mchango wangu kwa ujenzi wa Chama chetu na maendeleo ya nchi yetu na watu wake. Naamini historia itahukumu kwa usahihi kuhusu utumishi wangu kwa nchi yetu na Chama chetu.
Mheshimiwa Rais na Mwenyekiti Mtarajiwa,
Nimezungumzia wewe kumkabidhi mrithi wako mwaka 2025 kwa sababu naamini utapata kipindi cha pili. Maneno ya magazeti ati CCM mwisho wake 2020 yasikusumbue. Hilo halitatokea. Walinitabiria CCM kufia mikononi mwangu. Haikutokea na CCM imeendelea kushinda sana na itaendelea kushinda 2020 na 2025.
Tumuunge Mkono Mwenyekiti Mpya Dkt. Magufuli
Ndugu Wajumbe,
Baada ya maelezo yangu marefu ya utangulizi na ya kuagana, naomba sasa nizungumzie madhumuni makuu ya mkutano wetu huu. Agenda yetu ni moja tu: kuchagua Mwenyekiti Mpya wa kuchukua nafasi yangu. Sisi katika Halmashauri Kuu ya Taifa tumempendekeza Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ashike nafasi hiyo. Wapo wenzetu wawili ambao watakuja kuzungumza kwa niaba yetu kuwashawishi Wajumbe mkubaliane nasi. Nitawaita watu hao wakati wake ukifika, kwa sasa napenda kuchukua fursa fupi nami kusema kidogo.
Nina imani isiyokuwa na hata chembe ya shaka kwamba Mheshimiwa John Pombe Joseph Magufuli kazi hii anaimudu na ataifanya vizuri sana. Mapenzi yake na uaminifu wake kwa CCM hauna shaka. Anaipenda CCM kwa dhati ya moyo wake. Ameitumikia CCM na Serikali zake kwa moyo na uadilifu mkubwa. Anao uzoefu wa kutosha wa uongozi katika Chama. Amekuwa Mbunge na Waziri kwa miaka 20 yaani kumi katika Awamu ya Tatu na kumi katika Awamu ya Nne. Kama Mbunge amekuwa Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya, Halmashauri Kuu ya Wilaya , Mkutano Mkuu wa Wilaya, Halmashauri Kuu ya Mkoa na Mkutano Mkuu wa Mkoa na Mkutano Mkuu wa Taifa kwa miaka yote hiyo ishirini (20). Amekuwa Mjumbe wa Kamati ya Wabunge wa CCM kwa miaka 20. Hoja ya yeye kutokukijua Chama haina msingi wala mashiko. Ni kweli hajafanya kazi ya ukada kama nilivyokuwa mimi. Lakini hata Mzee Mwinyi na Mzee Mkapa hawakuwa Makada wa Chama lakini walikuwa Marais wazuri wa nchi yetu na Wenyeviti wazuri wa CCM.
Ndugu Wajumbe,
Mimi naamini Dr. John Magufuli atakuwa Mwenyekiti nzuri tu wa CCM. Baada ya miezi minane ya kuishikilia Serikali, ni wakati muafaka wa kuunganisha kofia hizi mbili kama ulivyo utamaduni, mila na desturi yetu nzuri. Nawaomba nyote mumuunge mkono kwa kumpa kura zote za Ndiyo na isipotee hata moja ya Hapana. Nawaomba pia kwamba baada ya kuchaguliwa mumpe ushirikiano zaidi ya ule mlionipa mimi katika kutekeleza majukumu yake ya kuongoza Chama chetu. Naondoka nikiwa naamini bila ya shaka yoyote kabisa kwamba chini ya uongozi wa Dr. John Pombe Joseph Chama cha Mapinduzi kiko katika mikono salama na kitapata maendeleo makubwa na haraka.
Mwisho
Ndugu Wajumbe,
Mwanzoni mwa hotuba yangu nilitoa shukrani kwa watu kadhaa lakini sikuwamaliza wote. Nimeacha salamu mahsusi mwishoni kwa familia yangu. Namshukuru kwa namna ya pekee mke wangu mpenzi Bi. Salma. Amekuwa nguzo imara katika familia na maisha yangu ya utumishi wa umma. Ana mchango mkubwa katika mafanikio yangu. Ndiyo chemchem yangu ya utulivu na ustahamilivu.
Shukrani zangu pia nazitoa kwa wanangu na wajukuu zangu kwa kunivumilia pale walipomkosa baba yao na babu yao. Nawapa pole na kuwataka radhi wanangu na familia yangu kwani wakati mwingine baadhi yao wamekuwa wahanga (collateral damage) kwenye mambo yasiyowahusu kwasababu ya maisha yangu ya siasa.
Nirudie tena kuwashukuru wana-CCM wenzangu kwa heshima kubwa mliyonipa ya kuwa kiongozi wa juu kabisa wa Chama chetu. Naondoka nikiwa mtu mwenye furaha tele kwamba Chama cha Mapinduzi kiko salama na kinaendelea kuwa madarakani. Naipenda sana CCM na nitaendelea kuipenda. Nawapenda sana viongozi na wanachama wenzangu wa CCM na nitaendelea kuwapenda hadi siku Mungu atakaponiita mbele ya haki.
Mungu Ibariki CCM
Mungu Ibariki Tanzania
Kidumu Chama Cha Mapinduzi
No comments: