WAZIRI MKUU ASEMA UAMUZI KUHAMIA DODOMA SIYO SIASA
“Hapa tulipofika ni hatua ya utekelezaji wa pamoja na hakuna namna nyingine kwa sababu uamuzi umeshatolewa. Nataka niwahakikishie kwamba hii siyo siasa, tunachokamilisha ni eneo dogo tu la kisheria juu ya uhamishaji wa makao makuu kuja Dodoma na katika Bunge la Septemba sheria hii itapitishwa,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo jioni wakati akizungumza na viongozi wa mkoa, Serikali za mitaa, viongozi wa dini, wajasiriamali, wazee wa Dodoma, wasafirishaji, wafanyabiashara, wakuu wa taasisi za elimu, za kifedha na watoa huduma mbalimbali katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Hazina ndogo.
Waziri mkuu ambaye aliitisha kikao cha kazi na wadau hao, ameutaka uongozi wa mkoa huo pamoja na wadau wake wakae na kuandaa mpango kazi wa jinsi ya kupokea na kutekeleza uamuzi wa Serikali kuhamia Dodoma.
Pia ametoa siku 14 kwa uongozi wa mkoa wa Dodoma kukamilisha mpango kazi wao na kumkabidhi mapendekezo yao ili yaweze kuingizwa kwenye mpango mkubwa wa Serikali kuu.
“Uongozi wa Mkoa, ukishirikiana na Ofisi yangu kupitia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Rais Tamisemi usimamie na kuyaratibu majukumu haya. Ndani ya siku 14 nipate proposal ya kwanza namna mtakavyoyatekeleza. Naagiza kiundwe kikosi kazi chini yenu kitakachowajumuisha makundi yote niliyoyataja,” amesema Waziri Mkuu.
MWANANCHI
No comments: