ESTER BULAYA ALIZWA NA MDOGO WAKE!
Ester Bulaya.
KILIO! Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya hivi karibuni alijikuta akimwaga machozi baada ya kuelezwa habari za mdogo wake, Deus Amos Bulaya aliyekuwa ametopea kwenye matumizi ya madawa ya kulevya.
Bulaya aliangua kilio hicho baada ya Risasi Mchanganyiko kumueleza kwamba, mdogo wake kwa sasa anaishi na muuza nyago wa video za Kibongo, Zena Abdallah ‘Jike Shupa’ na kwamba ameshaachana na madawa ya kulevya kwa takriban mwaka mmoja na nusu hivyo anamuomba amsaidie.
“Namuomba dada yangu Ester anisaidie na anisamehe kwani kwa sasa nimebadilika, nimeachana na madawa ya kulevya, siyo Deus yule tena naapa kwa jamii sitarudia maana dunia imeshanifunza
vya kutosha, namuomba dada yangu anisaidie kwa kuwa natamani kuwa na maisha yangu kama watu wengine ila naomba nikakae kwake hata kwa miezi kadhaa,” alisema Deus.
Akizungumza na Risasi Mchanganyiko kwa njia ya simu baada ya kuelezwa maombi aliyotoa mdogo wake huyo anayeendelea na matibabu ya kuacha madawa ya kulevya katika Hospitali ya Mwananyamala, ndipo Ester alipojikuta akitokwa machozi.
Deus Amos Bulaya.
Akiizungumzia ishu hiyo, Ester alisema ni muda mrefu na ameshawahi kuzungumza bungeni kuhusiana na ndugu yake huyo kuathirika na madawa ya kulevya ambapo yeye ndiye aliyemchukua na kumpeleka Mwananyamala kwenye kitengo cha dawa za kutibu waathirika wa madawa ya kulevya (methadone).
“Mimi ndiye niliyemuunganisha na daktari hapo Mwananyamala na kuanza dozi lakini amekuwa wakati mwingine anaacha na kurudia, ukimpa tu hela anaenda kununua unga, nilimnunulia kila kitu yaani nilikuwa namsaidia kwa kila kitu lakini akianza hayo madawa anauza kila kitu.
“Kuhusu kumsaidia, tupo kwenye mipango hiyo kama familia tuangalie ni jinsi gani tunafanya na hata juzi nilizungumza naye kwenye simu,” alieleza Ester huku sauti ya kilio ya mikwaruzo ikisikika kwenye simu.
NA GPL
No comments: