Header Ads

Blogger Tips and TricksLatest Tips And TricksBlogger Tricks

MAMBO 7 YALIYOMNG’OA ZARI KWA DIAMOND

 Mwanamama mfanyabiashara maarufu Afrika Mashariki, Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’ juzi Jumatano usiku, alitangaza kuachana jumla na supastaa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ na kusababisha gumzo kubwa mitandaoni, Risasi Jumamosi lina mambo saba yanayoaminika kuwa sababu ya kuvunjika kwa penzi hilo.

Zari alitangaza uamuzi wake huo kupitia ukurasa wake wa Mtandao wa Kijamii wa Instagram, ikiwa ni siku chache tangu Diamond aonekane akiwa kimahaba na aliyekuwa mpenzi wake wa zamani, Wema Isaac Sepetu kwenye ‘event’ ya kumtambulisha msanii mpya kwenye Lebo ya Diamond ya Wasafi Classic Baby (WCB), Maromboso au Mbosso iliyofanyika katika Ukumbi wa Hoteli ya Hyatt Regency Dar es Salaam, The Kilimanjaro, Posta jijini Dar.

UJUMBE WENYEWE
Katika ujumbe huo aliouandika kwa lugha ya Kingereza, Zari alisema amekuwa akisikia mambo mengi mabaya kwenye vyombo vya habari kuhusu Diamond ambayo baadhi yake yana ushahidi kuhusu usaliti wa mzazi mwenzake huyo hivyo ameamua kuachana rasmi na msanii huyo aliyezaa naye watoto wawili, Latifa Nasibu ‘Tiffah’ na Prince Nillan.
Licha ya kuwa Zari hakuainisha moja kwa moja sababu za kuachana, uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwepo kwa mambo saba ambayo yanatajwa kuwa sababu ya wawili hao kumwagana.

JAMBO LA KWANZA
Risasi Jumamosi lilibaini kwamba, jambo la kwanza lililosababisha Zari na Diamond kuachana ni kukosa ushauri mzuri wa wazazi ukizingatia Zari ambaye mama yake mzazi amefariki dunia huku akiwa hayupo karibu na baba yake.
“Angeweza kuwa na msaada mzuri wa kimawazo kama mama yake angekuwepo. Alikuwa akimsihi sana asiachane na Diamond licha ya kusikia mambo mengi mabaya ya Diamond sasa kwa upande wa pili yani wazazi wa Diamond, si rahisi sana kupata ushauri wao,” alisema Juma Sheki, mkazi wa Sinza, Dar.

JAMBO LA PILI
Jambo la pili ambalo uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa kama sababu ya wawili hao kuachana ni maisha ya wawili hao kuendeshwa na mitandao ya kijamii.
“Unajua mitandao hii imekuwa ikimpa sana presha Zari. Kuna mambo mengi alikuwa anapewa kupitia mitandao hiyo ambayo kimsingi haikuwa na ukweli wowote, lakini presha ilikuwa kubwa kiasi cha kushindwa kuhimili,” alisema John wa Mwenge.

JAMBO LA TATU
Suala la uongo nalo limetajwa kuwa sababu ya Zari na Diamond kuachana huku suala hilo likitajwa zaidi kwa msanii huyo kuliko mrembo huyo.
“Diamond alikuwa wakati mwingi sana hamuelezi ukweli mwenzake. Zari yule ameishi katika mazingira kama ya Kizungu fulani hivi hivyo hakuna kitu kinachomuudhi kama akigundua amedanganywa au kufichwa kitu fulani.

“Kama unakumbuka, mara kadhaa Diamond alikuwa akibanwa kuhusu warembo kama (Hamisa) Mobeto na Tunda (Sebastian), lakini alikuwa akikataa, lakini mwisho wa siku inakuja kubainika ukweli.
“Alificha sana kwa Mobeto, lakini baadaye ukweli ulikuja ukabainika kwamba ni kweli amempa mimba na hadi kumzalisha. Hivyo vitu ambavyo kwa wenzetu wenye kuishi katika tamaduni za Kizunguzungu huwa hawawezi kuvivulia,” alichangia Abdallahman Akida, aliyejitambulisha kuwa anaishi Tandale, Dar.

JAMBO LA NNE
Uchunguzi huo ulizidi kubaini kwamba, jambo lingine lililosababisha wawili hao wamwagane ni kutokana na Zari kuhifadhi matukio mengi maovu ya Diamond ambayo yalifikia levo fulani ya kushindwa kuvumilika.
“Zari alihifadhi matukio mengi sana ya Dai (Diamond). Alijitahidi sana kutetea penzi lake, lakini mwisho wa siku maji yalimfika shingoni, akaamua bora ajiweke pembeni,” alisema Amina Shekiondi wa Kigogo, Dar.

JAMBO LA TANO
Naye John Sekion, mkazi wa Mbagala, Dar, alisema kuwa, jambo lingine lililosababisha Diamond na Zari waachane ni hadhi na jina la Zari kwani inafahamika mrembo huyo anamiliki shule na vyuo hivyo hakupenda kuonekana yupo na mtu ambaye kila uchwao anaonekana na wanawake tofauti.

JAMBO LA SITA
Jambo la sita lililopatikana kwenye uchunguzi wa gazeti hili ambalo kimsingi limetajwa kuchangia kuachana kwa Diamond na Zari ni mrembo huyo kukosa kile alichokuwa anakihitaji kwa mwanaume, upendo wa dhati.
“Zari alikuwa ana fedha, ana kila kitu kinachomwezesha kuishi katika levo ya maisha ya kitajiri, lakini alikuwa anakosa penzi la dhati ambalo kwa mtazamo wangu amelikosa kwa Diamond na ndiyo maana akaamua kubwaga manyanga,” alisema Meckion Mtamba wa Chanika, Dar.

JAMBO LA SABA
Jambo la saba ambalo Risasi Jumamosi lilibaini katika uchunguzi wake ni jeuri ya fedha ya Zari ambapo inaonesha alikuwa akitaka kumpanda kichwani Diamond ambaye alikuwa amemzidi kiumri na hata kifedha.
“Unajua Zari ana fedha na miradi mikubwa ambayo kimsingi alikuwa anamzidi Diamond. Sasa hii wakati mwingine huwa inamfanya mtu awe na jeuri fulani na kutaka kumfanya mwanaume anavyotaka,” alisema mkazi wa Kijitonyama, aliyejitambulisha kwa jina moja la Penny.

DIAMOND ANASEMAJE?
Risasi Jumamosi lilimtafuta Diamond ili kumsikia anazungumziaje suala hilo la kuachana alilolitangaza Zari ambapo alipopatikana, alisema hana jambo la kuzungumza kwa sasa kwani na yeye ameona kwenye Mtandao wa Instagram.
“Kwa sasa sina la kuzungumza kwa sababu na mimi nimeona tu hivyo siwezi kuzungumza kwa sasa,” alisema Diamond.

BABA DIAMOND ATIA NENO
Gazeti hili lilizungumza na baba wa msanii huyo, mzee Abdul Jumaa ili kumsikia anamshaurije mwanaye baada ya kusikia Zari kamwaga manyanga ambapo alifunguka:
“Huu ni uhusiano wao na nisingependa kuingilia sana kama mzazi licha ya kwamba tayari amenipa wajukuu ila kama watashindwana, basi amuoe Mobeto ambaye pia ninamuona ni mwanamke mzuri na ana moyo mzuri.”

MAMA MOBETO VIPI?
Baada ya kumtafuta bila mafanikio Mobeto, gazeti hili lilifanikiwa kumpata hewani mama yake mzazi ambaye aliposikia mwandishi amejitambulisha tu, alikata simu kabla hata hajaelezwa dhumuni la kupigiwa simu.

MAMA DIAMOND
Baada ya kumalizana na mama Mobeto, Risasi Jumamosi lilimtafuta mama mzazi wa Diamond, Sanura Kassim ‘Sandra’ na mzungumzo yake na mwanahabari wetu yalikuwa hivi:
Risasi Jumamosi: Mama vipi za siku? Tumekumisi kweli upo?
Mama Diamond: Asante, ninashukuru. Leta maneno.
Risasi Jumamosi: Aaah jamani ata husemi umetumisi na sisi? Kweli? Usitufanyie hivyo mama D.
Mama Diamond: Wewe sema bwana ulichonipigia…
Risasi Jumamosi: Vipi habari za wapi? Madale au?
Mama Diamond: Madale wapi, wewe mimi nipo Kontena.

Risasi Jumamosi: Oooh kumbe siku hizi unaishi Kontena, ipo wapi hiyo?
Mama Diamond: Wewe sema bwana ulichonipigia…
Risasi Jumamosi: Tulikuwa tunataka huu ubuyu mpya wa Zari unauzungumziaje?
Mama Diamond: Wewe bwana sema ulichonipigia.
Risasi Jumamosi: Ndicho hicho, tumeona waraka wa Zari kwamba ameamua kuachana mazima na mwanao, unazungumziaje?
Mama Diamond alikata simu na hata alipopigiwa tena hakupokea.

TUJIKUMBUSHE
Kabla ya kukutana na Diamond, Zari aliwahi kuolewa na aliyekuwa mfanyabiashara maarufu, raia wa Uganda, marehemu Ivan Ssemwanga ‘Don Ivan’ ambaye aliachana naye akiwa amezaa naye watoto watatu hivyo hadi sasa mwanamama huyo ana jumla ya watoto watano, ukiongeza na wawili aliozaa na Diamond.

Kwa upande wake Diamond, kabla ya kukutana na Zari kwenye ndege wakiwa safarini na kuanzisha uhusiano wa kimapenzi, kwa nyakati tofauti aliwahi kubanjuka penzini na warembo tofauti wenye majina Bongo akiwemo mtangazaji, Penniel Mungilwa ‘Penny’, Irene Uwoya (muigizaji), Wema Sepetu (muigizaji) na Jokate Mwegelo (muigizaji) kisha kuachana nao.

NA GPL

No comments: