Mtulia atangazwa mbunge wa Kinondoni
Mgombea wa CCM Jimbo la Kinondoni, Maulid Mtulia ameibuka mshindi katika uchaguzi mdogo wa ubunge uliofanyika jana Februari 17,2018.
Msimamizi wa uchaguzi ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni, Aron Kagurumjuli ametangaza matokeo hayo leo Februari 18,2018.
Amesema Mtulia ameshinda kwa kupata kura 30,247 akifuatiwa na Salum Mwalimu wa Chadema aliyepata kura 12,353 na Rajab Salum wa CUF aliyepata kura 1,943.
“Kwa matokeo hayo na kwa mujibu wa mamlaka niliyopewa na sheria ya uchaguzi, namtangaza Maulid Mtulia kuwa Mbunge wa Kinondoni,” amesema msimamizi huyo wa uchaguzi.
Jana jioni Februari 17,2018 Kagurumjuli alisema kazi ya kutangaza matokeo ingekamilika saa sita usiku lakini hilo lilishindikana.
Ulinzi uliimarishwa katika eneo la kujumlisha matokeo la Biafra, ambako Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa; Mkuu wa Mkoa, Paul Makonda na Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi wamekesha katika eneo la kuhesabu kura.
Mgombea wa CCM, Maulid Mtulia naye alikesha eneo hilo akisema hataki kuuchukulia kirahisi uchaguzi huo.
Wawakilishi wa vyama vya upinzani hawakuwepo eneo hilo.
No comments: