NDEGE YA NIT YAAGUKA NA KUUWA MARUBANI
Marubani wawili wamefariki Dunia katika ajali ya ndege wakati wa kurusha ndege baada ya matengezo katika Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume Mjini Zanzibar.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo lililotekea majira ya saa saba Mchana Uwanjani hapo, Muhandisi Mkuu kutoka Kampuni ya Tropical Air, David Kisusi amesema ndege hiyo imeanguka na kuungua na kusababisha vifo kwa marubani hao ambao walikuwa ndani ya ndege hiyo.
Dominic Bomani enzi za uhai wake.
Amesema ndege hiyo yenye usajili wa 5H-TDF yenye uwezo wa kubeba abiria wanne ni mali ya Chuo cha Usafirishaji cha Dar-es-Salam (NIT) ambayo ilikuwepo Zanzibar kwa ajili ya matengenezo.
Amesema takriban miezi sita ndege hiyo ipo hapa Zanzibar kwa ajili ya kufanyiwa matengenezo ili iweze kutumika katika chuo cha Usafirishaji .
Daktari Bingwa wa Uchunguzi katika Hospital ya Kuu ya Mnazi mmoja, Msafiri Marijani amethibitisha kutokea kwa vifo hivyo na amesema vifo hivyo vimesababishwa na kukosa hewa safi wakati wa ajali hiyo pamoja na kathirika na moto uliotokea wakati wa kuanguka ndege hiyo.
Amesema uchunguzi ulifanywa katika miili ya maiti hao mnamo majira ya saa 12:45 jioni pia ulitokana na kukosa msaada wa kwa muda mrefu tangu ndege hiyo ianguke na kulipuka.
Wakati huohuo Mkuu wa Chuo cha Usafirishaji wa Anga kutoka Dar es Salaam, Dkt. Bwire Rufunjo alifika Zanzibar kwa ajili ya kufuatilia taarifa za ajali hiyo na amesema wamepokea taarifa hiyo kwa mshtuko mkubwa kutokana na vifo vya wafanyakazi hao muhimu katika sekta ya anga.
Aliwataja marehemu kuwa ni Injinia Edger Alfred Mecha mwenye Umri wa miaka 26 na mwengine ni Dominic Bomani mwenye umri wa miaka 64 ambao walikuwa wanafanya kazi katika chuo hicho kwa ufanisi mkubwa.
Injinia Edger Alfred Mecha enzi za uhai wake akiwa na Waziri wa uchukuzi, Prof. Mbarawa.
Aidha amewataka wanafamilia wa Marehemu hao kuwa wavumilivu katika kipindi hichi kigumu kufuatia msiba huo pamoja na kutoa wito kwa wanafunzi wa chuo hicho kutokata tamaa wakati wa masomo.
Akizungumzia sababu ya kuanguka kwa ndege hiyo ndogo, amesema uchunguzi bado unaendelea lakini katika uchunguzi wa awali wamebaini kuwa ni hitilafu ya mfumo wa umeme ambao umesababishwa na moto ulilipuka kutokana na ndege kuwa na Mafuta mengi.
Ndege hiyo imenunuliwa kutoka kampuni ya Tropical Air ya Zanzibar kwa ajili ya kufundishia Urubani katika Chuo cha Usafirishaji lakini kutokana na kutokuwa na hali Nzuri ililazimika kufanyiwa matengenezo na kampuni hiyo kabla kuchukuliwa na chuo.
No comments: