SHINYANGA::MWILI WA MAREHEMU WAFUKULIWA NA KUZIKWA TENA,TUMBO KUTOBOLEWA
Wakazi wa mtaa wa Matanda kata ya Chamaguha wakifukua kaburi la Ashura Shabani baada ya ndugu wa marehemu kumzika ndugu yao wakiwa na hofu ya kuwa huenda viungo vya mwili wake viliibiwa
Zoezi la kufukua mwili wa marehemu likiendelea
Mjomba wa marehemu Sued Mussa akizungumzia namna kifo cha mpwa wake Ashura Shabani
Wananchi wa Mtaa wa Matanda kata ya Chamaguha manispaa ya Shinyanga wakiwa katika ofisi ya mtaa huo kwa ajili ya kusubiri maelekezo ya kwenda kuufukua mwili wa marehemu Ashura Shabani
Akina mama wakiwa eneo la tukio
Wananchi wakiwa katika eneo la ofisi ya mtaa wa Matanda
Wananchi wa mtaa wa Matanda kata ya Chamaguha manispaa ya Shinyanga wakiwa katika ofisi za mtaa huo
***
Taharuki ya aina yake imetokea baada ya mwili wa marehemu Ashura Shabani (35-40) mkazi wa mtaa wa Matanda Kata ya Chamaguha katika manispaa ya Shinyanga kufukuliwa kisha kuzikwa kwa mara ya pili katika makaburi ya Chamaguha baada ya kuwepo na mashaka kuwa alitobolewa tumbo na madaktari wa hospitali ya rufaa Bugando Jijini Mwanza na kuondolewa baadhi ya viungo vyake vya ndani.
Mwili wa Ashura uliozikwa Februari 18,2018 umefukuliwa leo Jumatano Februari 21,2018 baada ya kutokea uvumi kuwa mwili huo ulikuwa na tundu pembeni mwa tumbo hivyo huenda kuna baadhi ya viungo vyake vimenyofolewa.
Ashura anadaiwa kufariki dunia Februari 17,2018 mwaka huu katika hospitali binafsi za madaktari wa hospitali ya rufaa Bugando Jijini Mwanza akifanyiwa upasuaji kwa ugonjwa wa shingo 'goita' na hakuwa na malazi ya tumbo.
Inaelezwa kuwa awali alikuwa amelazwa katika hospitali ya rufaa Bugando na kupelekwa kwenye hospitali binafsi kufanyiwa upasuaji wa shingo na alipofariki dunia mwili ulirudishwa tena Bugando kwenye chumba cha kuhifadhia maiti.
Mjomba wa marehemu Sued Mussa, alisema marehemu alikuwa anaumwa Goita Shingoni na alikuwa akitibiwa katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Shinyanga na kupewa Rufaa kwenda Bugando Jijini Mwanza na hatimaye mauti kumfika na kwenda kuuchukua mwili wake kwa ajili ya mazishi.
“Wakati akina mama walipokuwa wakiuosha mwili wa marehemu waliona pembeni ya tumbo kuna tundu, na wakati marehemu alikuwa na tatizo shingoni lakini hawakusema hadi tunamzika juzi Februari 18,2018 ndipo wakaanza minong’ono kuwa wamekuta tundu hilo hivyo huenda viungo vya mwili wa marehemu vimenyofolewa”alieleza.
Alisema baada ya taarifa hiyo ndipo wakaenda kutoa taarifa polisi wakitaka mwili wa ndugu yao ufukuliwe ili uweze kufanyiwa uchunguzi (Postmoterm) kujiridhisha kama kweli ametobolewa tumbo na kupewa taarifa kwanini alifanyiwa hivyo na wakati tatizo lake lilikuwa ni la Shingo.
Zoezi la kufukua mwili huo limesimamiwa na mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai wa Jeshi la Polisi mkoa Mwanza John Mwaulemi, ambaye alifika mkoani Shinyanga na kubainika kuwa
marehemu hakutobolewa tumbo bali alichanwa paja kwa ajili ya kuwekwa dawa ili asiharibike.
Mjomba wa marehemu Sued Mussa, ambaye ni miongoni mwa walioufanyia uchunguzi mwili huo wa mpwa wake amesema baada ya kufanya uchunguzi wa kina hawakukuta tundu lolote tumboni kama ilivyodaiwa awali na akina mama ambao waliuosha mwili huo.
Amesema mara baada ya kubaini kuwa hakufanyiwa unyama wowote wameuchukua mwili wa marehemu na kuuzika tena kwa mara ya pili huku akitoa lawama kwa madaktari wa Bugando kwa kumtoa kwenye hospitali hiyo na kumpeleka kwenye hospitali zao binafsi na kufia huko.
No comments: