ASKOFU CHENGULA: CHAGUENI VIONGOZI WASIO NA UBINAFSI
ALIKUWA AKIONGOZA IBADA YA IJUMAA KUU ILIYOFANYIKA KITAIFA MBEYA |
Kauli hiyo imetolewa leo Machi 30 na Mhashamu Askofu Evarist Chengula alipokuwa akiongoza ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika kitaifa katika kanisa Katoliki la Bikira Maria wa Fatma lililopo Mwanjelwa mjini Mbeya.
Akihutubia katika ibada hiyo Mhashamu Chengula amesema ujumbe uliotolewa na maaskofu siku kadhaa zilizopita ulikuwa haumlengi mtu fulani bali uliwalenga wanafiki wanaodai ni Wakristo lakini hawana imani ya Kikristo ili waweze kubadilika na kuwa watu wema.
VIDEO-Mkuu wa KKKT: hatutakubali kunyamazishwa
“Ujumbe wa mwaka huu tunasema hakuna maana kusikiliza kila kitu tu, badala yake tufikiri kabla ya kutenda.
“Imekuwa kawaida kila baada ya kumalizika uchaguzi mkuu tunaanza kulaumiana, Wakristo wote katika jumuiya zenu ndogo ndogo nchi nzima muanze kujipanga mnataka mtu wa aina gani, angalieni ana tabia gani na si anatoka chama fulani,” amesema Mhashamu Chengula. Amewataka wanaparokia kukaa na maaskofu na kujadili.
“Msipofanya hivyo mtarudi kule kule kwa kulaumiana. Chagueni kwa kuzingatia kila mmoja atendewe haki, apate haki na amani.” Amesema na kuongeza;
“Kila baada ya uchaguzi wanakimbizana kama sungura na mbwa maana hatuchagui anayetusaidia sisi, tunachagua chama fulani kituongoze na kitutetee badala ya kufikiri kuchagua atakayetuongoza kwa amani.”
Ameongoza: “Haina maana kutuchagulia watu fulani ambao tukiwachagua wanatuongoza kwa woga, hawa hawajajiweka wenyewe ni mimi na wewe tumewaweka, tusichague watu wenye roho ya ubinafsi.”
Amesema ujumbe huo ni kwa wote, ili waanze kujiandaa kwa sababu unafika uchaguzi wa mwaka 2019 wachague kwa kuangalia hali halisi.
“Kila mmoja akasimulie hili anapokwenda kwa sababu ni vita ya wote, kila mmoja awe makini Tanzania iwe na upendo na mshikamano kati yetu.
“Kila anayekuja kubusu msalaba huu tulioulaza hapo mbele amueleze Yesu nataka Tanzania yenye upendo,” amesema Mhashamu Askofu Chengula.
No comments: