BINTI AUWA AKITOKA KANISANI, ALIENDA KUMWOMBEA MAMA YAKE KIPOFU! – VIDEO
DAR ES SALAAM: Inauma sana! Ndio unavyoweza kusema baada ya binti, Toto Aloyce (20), mkazi wa Buza kwa Lulenge, jijini Dar kuuawa kinyama na watu wasiojulikana akiwa anatoka kanisani kumuombea mama yake ambaye ni kipofu.
Akisimulia tukio zima, mama wa binti huyo, Tamasha Juma aliliambia Amani kuwa Jumatatu iliyopita jioni, binti yake alimuomba shilingi 1000, kwa ajili ya kwenda kununua chipsi.
Alieleza kuwa baada ya kumpa fedha hiyo, binti huyo alichukua shuka ili akitoka kununua chipsi aende kanisani kwa ajili ya mkesha wa maombi ambapo pamoja na maombi yake binafsi, alikuwa akimuombea yeye aweze kupona macho.
“Sikujua kama fedha zile zilikuwa za mwisho kwa binti yangu kwani baada ya kumpa tu hatukuonana tena mpaka nilipopata taarifa za kifo chake,” alisema mama huyo.
Aidha, mama huyo alieleza kuwa alipata taarifa ya kifo cha mwanaye huyo siku iliyofuata alfajiri baada ya kuitwa nje na wasamaria wema.
“Nilipotoka nje nilipewa taarifa kuwa mwanangu amekutwa amefariki dunia wakati akiwa anarudi nyumbani huku akiwa na jeraha kubwa kichwani,” alisema mama huyo.
Aliendelea kusimulia kuwa, majirani waliokuwa karibu na sehemu ulikokutwa mwili wa binti yake walimuambia kuwa marehemu alipiga kelele muda mrefu huku akiomba msaada lakini watu waliogopa kutoka.
“Yaani mwanangu ameuwawa kinyama sana jamani kwa sababu waliomsikia wanasema alipiga sana kelele ya kuomba msaada lakini watu waliogopa kutoka wakihofia na wao kufanyiwa kitu kibaya,” alisema mama huyo.
Mama wa msichana huyo aliongeza kuwa mtoto wake alikuwa ni msichana aliyetulia asiyependa makundi na alikuwa na tabia njema na wala hakuwa na tabia ya kutokatoka hovyo nyumbani.
Wananchi wa eneo hilo walipokuwa msibani hapo waliliambia Amani kuwa, matukio kama hayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara lakini polisi wameshindwa kuwasaidia kwani malalamiko yao wameshayapeleka mara kwa mara lakini wahusika hawachukuliwi hatua.
Alipotafutwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Temeke, ACP Andrew Satta alikiri kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa wanaendelea na uchunguzi kwani matukio kama hayo yamekuwa yakitokea maeneo hayo mara kwa mara.
Stori: NA GPL
No comments: