FAMILIA YA WATU 6 KUFARIKI AJALINI, NI ZAIDI YA MSIBA
DAR ES SALAAM: unaweza kusema huu ni zaidi ya msiba kufuatia ile habari ya watu sita wa familia moja wakazi wa Buguruni kwa Mnyamani jijini Dar, kufariki dunia kwa mpigo katika ajali iliyohusisha gari aina lori na basi dogo aina ya Hiace iliyotokea mwishoni mwa wiki iliyopita Mkuranga, Wilaya ya Pwani na kuua watu 26.
BIBI AZUNGUNGUMZA
Akizungumza kwa uchungu kuhusiana na misiba hiyo, bibi aliyefahamika kwa jina la Mwanahamisi Mohammedi ambaye ni mama aliyepoteza mtoto mmoja na wajukuu watatu na watukuu watatu waliokuwa wakienda kwenye sherehe ya Maulid ya watoto iliyokuwa ikifanyika Mwalusembe mkoani humo alisema, alipokea simu saa nne usiku na kuambiwa kuwa mwenye simu hiyo amepata ajali na amefariki dunia na akaelekezwa sehemu ambayo ajali imetokea.
SAA NANE USIKU
Bibi huyo aliendelea kusimulia kuwa, baada ya kupata taarifa hiyo ilibidi awafahamishe ndugu zake wengine ambapo walijipanga na kwenda mpaka eneo hilo la tukio ambapo walifika saa nane usiku na kukuta miili ya wapendwa wao imeshapelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mkuranga.
“Usiku huohuo baada ya kupata taarifa ilibidi tujipange na kwenda mpaka eneo la tukio lakini kwa bahati mbaya tukakuta miili imeshaondolewa na kupelekwa hospitali,” alisema bibi huyo.
Aliongeza kuwa watu wote waliofariki dunia walikuwa wakiishi nyumba moja kama familia hivyo kuna pengo kubwa sana kifamilia ambalo kamwe hawajui litazibwa na kitu gani kwa sababu aliwazoea sana marehemu hao na pia ni damu yake.
“Mimi mpaka sasa sielewi nitaishije jamani, nina huzuni kubwa mno eee Mungu, nimeachwa peke yangu, sielewi mwisho wangu ni nini, fikiria unapoteza watu sita nyumba moja unaweza kupata wapi moyo wa kuvumilia, nitalia siku zote, huu ni zaidi ya msiba,” alisema bibi huyo huku akitokwa na machozi.
WALIOPOTEZA MAISHA
Bibi huyo aliwataja wanafamilia yake waliofariki dunia kuwa ni Mwajuma Ally, Abdallah Athmani, Said Athuman, Nuru Yusuph, Halima Jabir na Yusra Said.
Alisema mwanaye mwingine, Ashura Mohammed amenusurika lakini bado yuko hoi Muhimbili kwa matibabu na mjukuu wake mmoja ambaye amevunjika mkono.
UPASUAJI WA MAJERUHI MOI
Wakati huohuo majeruhi watatu kati ya 10 wa ajali hiyo waliolazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (Moi) wamefanyiwa upasuaji.
Meneja Uhusiano na Ustawi wa Jamii wa Moi, Jumaa Almasi alisema kati ya majeruhi nane, waliowapokea, watatu wamefanyiwa upasuaji wa dharura.
“Kwa ujumla hali ya majeruhi zinaendelea kuimarika, siyo kama walivyoletwa, naweza kusema afya zao zinaendelea vizuri, kwa sasa majeruhi wamebaki saba kwa Moi kwani mmoja ameruhusiwa,” alisema Almasi.
MSEMAJI MUHIMBILI ANENA
Naye Msemaji wa MNH, Neema Mwangomo alisema walimpokea majeruhi mmoja na kumtaja jina la Mariam Msigwa na anaendelea na matibabu.
Alisema majeruhi hao wote walifikishwa hospitalini hapo saa 8.30 usiku siku ya tukio na kuanza kupatiwa matibabu ambapo nane walipelekwa Moi.
POLISI WANASEMAJE?
Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, ACP Fortunatus Muslimu alisema juzi kuwa lori hilo lilikuwa limebeba chumvi tani 32.
“Lori hilo lilikuwa kwenye mwendo kasi na lilipofika Kijiji cha Kitonga wilayani Mkuranga, dereva alishindwa kulimudu,” alisema na kufafanua kuwa dereva huyo anashikiliwa na polisi.
“Kwa vyovyote dereva huyu atafutiwa leseni yake lakini dereva wa Hiace alifariki dunia kwani alikuwa miongoni mwa 26 waliopoteza maisha,” alisema kamanda huyo.
Kamanda Muslimu aliwataka madereva wote nchini kuzingatia sheria za barabarani na kuwa makini kwenye miinuko na kona ili kuepusha ajali kama hiyo iliyotokea.
TUJIKUMBUSHE
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Kibiti, Rufiji na Mkuranga, ACP Mohammed Likwa alisema juzi kuwa gari aina ya Hiace lilikuwa likitokea Dar es Salaam kuelekea Wilaya ya Mkuranga wakati lori lilikuwa likitokea Lindi kuelekea Dar es Salaam.
Lori hilo lina usajili namba T223 CZB aina ya Scania na tela lenye usajili namba T371 CDT na lilikuwa likiendeshwa na Twaha Issa (30), ambaye anashikiliwa na polisi, lilipogongana uso kwa uso na Hiace ‘kipanya’, ambacho usajili wake ni namba T676 CGK lilikuwa likiendeshwa na Seleman Bakari (33) ambaye alifariki dunia.
NA GPL
No comments: