KIZUNGUMKUTI CHA ELIMU YA MSINGI KUISHIA DARASA LA SITA
Wakati wadau wa elimu wakionyesha hofu ya utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, Serikali imesema muundo mpya wa wanafunzi wa shule za msingi kumaliza wakiwa darasa la sita, hautaanza kutumika sasa na hautawahusu wanaoendelea na masomo.
Kauli hiyo imekuja kukiwa na taarifa kuwa baadhi ya walimu wamewatangazia wanafunzi wa darasa la nne kwamba wataishia darasa la sita hivyo watahitimu mwaka 2020.
Imedokezwa kwamba wanafunzi hao, wataungana na wale walioko darasa la tano mwaka huu kufanya mtihani wa mwisho kwa pamoja, jambo lililoibua hofu kwa wadau kuhusu utekelezaji wake.
Sera hiyo iliyozinduliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete Februari 13, 2014 iliweka mabadiliko makubwa kwenye mfumo wa elimu ya awali, msingi na sekondari unaotakiwa kuwa wa muundo wa 1+6+4+2+3 kutoka 2+7+4+2+3.
Kwa mujibu wa sera hiyo, elimumsingi itaanzia chekechea hadi kidato cha nne na itakuwa ya lazima na ya bure. Sera hiyo inabainisha kuwa umri wa kuanza shule utabadilika, sambamba na wa elimumsingi ya lazima kuwa miaka 10.
Utekelezaji wa sera hiyo umewekewa msisitizo katika Ilani ya CCM ya mwaka (2015-2020) iliyonadiwa kwa wananchi na Rais John Magufuli wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka 2015.
Kifungu cha 52 cha ilani hiyo kinasema: Elimu ya kisasa na hasa yenye mwelekeo wa sayansi na teknolojia ina nafasi ya pekee katika kufanikisha ujenzi wa msingi wa uchumi wa kisasa wa Taifa linalojitegemea.
Pia inasema katika kipindi cha miaka mitano ijayo (2015-2020), CCM itahakikisha Serikali inasimamia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 kwa kutekeleza mambo kadhaa ikiwamo kuandaa mfumo, muundo na taratibu nyumbufu za kutoa elimu ya awali na elimumsingi (1+6+4) bila malipo.
Miaka miwili na zaidi imepita tangu Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani Novemba 5, 2015, huku suala lililotekelezwa likiwa la elimu bila malipo pekee.
Majibu ya Serikali
Alipoulizwa kuhusu lini muundo huo mpya wa elimu utaanza kutekelezwa, Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Leonard Akwilapo alisema hakuna mwanafunzi anayesoma sasa elimu ya msingi atakayekumbwa na utekelezaji na muundo huo mpya.
Alisema wanafunzi wote walioko shuleni wataendelea kutumia utaratibu wa kawaida wa miaka saba, huku akisema Serikali bado haijakamilisha baadhi ya mambo muhimu ikiwamo yale yanayohusu miundombinu na walimu.
“Suala hili halitatekelezwa sasa na wanafunzi wote walioko shuleni watamaliza shule kwa kipindi cha miaka saba. Wakati ukifika tutatoa taarifa kupitia taratibu zilizopo,” alisema Dk Akwilipo.
Hofu ya wadau
Pamoja na kwamba mpango huo haujaanza, Chama cha Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania (Tamongsco), kimeupinga kikisema unachelewesha watoto kuanza kujifunza na badala yake kutaka Serikali ijikite katika kuboresha miundombinu.
Katibu Mkuu wa Tamongsco, Kanda ya Kaskazini, Leonard Mao alisema katika maoni yao waliyoyatoa walipendekeza mfumo wa 2+7+4.
“Mwanafunzi anapaswa kuanza darasa la kwanza akiwa na miaka saba na chekechea asome miaka miwili,” alisema.
Mao aliyeshiriki kuandaa sera hiyo alisema: “Bado utekelezaji wake ni mgumu, kwa sababu pale mtoto anapomaliza miaka sita shule ya msingi, anaanza kidato cha kwanza hadi cha sita. Je, madarasa yote yatakuwa na maabara, walimu wapo wa kutosha, wanafunzi wameandaliwa?”
Mhadhiri mwandamizi wa Shule Kuu ya Elimu ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Duce), Dk George Kahangwa alisema pamoja na Serikali kuamua kujikita katika sera hiyo, inapaswa kuwa makini vinginevyo hali inaweza kujirudia ya miaka yote.
Alisema kwanza ilipaswa kuweka mifumo yenye kueleweka itakayobainisha namna sera hiyo itakavyotekelezwa, wakati wa kutekelezwa na wahusika wake.
Alisema kabla ya kuchukua hatua hiyo, Serikali ihakikishe imewaandaa vya kutosha walimu waliopo na ikiwezekana kuongeza wengine wapya.
“Tunapofanya mabadiliko ya kimfumo, lazima pia hawa walimu waliopo wapatiwe mafunzo waweze kuendana na mabadiliko hayo. Lakini pia lazima Serikali ihakikishe imeandaa vitabu vya kutosha na kubadilisha mitalaa iliyopo, vinginevyo tutaishia kuwa na sera za kwenye majukwaa lakini katika vitendo hatufiki mbali,” alisema.
Dk Kahangwa aliungwa mkono na waziri kivuli wa elimu, Suzan Lyimo ambaye alisema bado haamini kama Serikali itafanikiwa kutekeleza sera hiyo kutokana na upungufu mkubwa uliopo.
“Binafsi nadhani kama Serikali itatekeleza sera hii, basi ni mpaka pale itakapotenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya ili kutosheleza mahitaji ya wanafunzi,” alisema mbunge huyo wa Viti Maalumu (Chadema).
Meneja wa Uraghibishi wa Twaweza, Anastazia Lugaba alionyesha wasiwasi wake kuhusu nafasi ya Serikali kutekeleza sera hiyo akiitaka kuweka mikakati itakayotekelezeka na kuifanyia mageuzi sekta ya elimu, “Hii sera ya elimu bure haijafanikiwa na tangu ilipoanza kutekelezwa imekuwa ikikumbana na vikwazo vingi hali ambayo pia imewavunja moyo walimu wengi,” alisema.
No comments: