MAMA AKUTWA AMEKUFA KORIDONI AKIWA MTUPU
MOROGORO: Hiki ni kifo tata! Mama mmoja aliyefahamika kwa jina la Vicky Urambo, mkazi wa Mtaa wa Kiswanya A, Kata ya Uwanja wa Taifa mkoani hapa, amekutwa amekufa katika mlango wa chumbani na sebuleni kwake huku akiwa hana nguo yoyote mwilini.
Tukio hilo lilitokea Jumatatu iliyopita ndani ya nyumba aliyokuwa akiishi mama huyo aliyekuwa akifanya kazi katika Baa ya Moro Night iliyopo Mtaa wa Khahumba katikati ya mji wa Morogoro.
Mashuhuda wa tukio hilo ambao ni wapangaji wenzake marehemu walipohojiwa na Amani walisema siku moja kabla ya kifo cha mwenzao huyo anayeishi peke yake kwenye nyumba hiyo aliwaeleza kuwa hakuwa sawa bila kufafanua.
“Alituambia hayuko sawa, lakini hakufafanua zaidi na ilikuwa jana (Jumapili) kama saa 10 jioni, aliingia chumbani kwake kulala, tukashangaa kuona toka saa 10 mpaka leo (Jumatatu) saa 6 mchana hajatoka nje.
“Tukawa tunasikia simu yake ikiita bila kupokelewa, tulipojaribu kufungua mlango tukagundua kuwa umefungwa kwa ndani, tukaamua kuchungulia dirishani huku tukigonga.
“Tukashuhudia marehemu akiwa amelala chini katikati ya mlango wa chumbani kwake na sebuleni huku akiwa hana nguo yoyote, tukatoa taarifa kwa mwenyekiti wa mtaa naye akawataarifu polisi.
“Polisi walipofika walivunja mlango, wakauchukua mwili na kuupeleka mochwari,” alisema mpangaji aliyejitambulisha kwa jina la Lucy Elius.
Mpangaj huyo alipoulizwa marehemu alikuwa akiishi na nani kwenye nyumba hiyo alijibu kwamba alikuwa akiishi peke yake.
“Hakuwa na mume na katika maisha yake amebahatika kupata mtoto mmoja wa kiume ambaye ni askari polisi jijini Mwanza na tumeshampa taarifa akasema atakuja na mkewe kufanya taratibu za mazishi yatakayofanyika ama hapa au kwao Mbeya,” alisema.
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo, Shamira Salum Tindwa alithibitisha kutokea kwa tukio hilo kwenye mtaa wake.
“Inauma sana, hili ni tukio la kwanza kutokea mtaani kwangu tangu nishike madaraka haya.
“Juzi dada Vicky (marehemu) nilipanda naye daladala moja, cha ajabu muda huu napokea taarifa kutoka kwa mjumbe wangu wa mtaa huu akidai amekufa kifo tata kutokana na kukutwa mtupu,” alisema mwenyekiti huyo wa mtaa.
Mwandishi wetu aliyekuwepo eneo la tukio alishuhudia Kaimu Mkuu wa Upelelezi wa Wilaya ya Morogoro, Beatrice Lyamuya akiwaambia askari wake wa kiume na mwandishi wetu kutoingia ndani kwani marehemu alikuwa mtupu, hivyo akaingia na polisi wa kike tu ambao walikwenda kumsitiri marehemu kwa kanga kwa kushirikiana na wanawake wa mtaani hapo.
Mara baada ya habari za kifo hicho kusambaa, mwandishi wetu aliwashuhudia wafanyakazi wenzake marehemu wakifika eneo hilo na usafiri wa gari dogo maarufu kama ‘Kirikuu’ huku wakiangua vilio na kusababisha eneo hilo kuzizima kwa simanzi.
NA GPL
No comments: