MAMBOSASA ASEMA HAWAJABAINI SILAHA ILIYOTUMIKA KUMUUA AKWILINA
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema uchunguzi kuhusu tukio la kuuawa kwa risasi mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini bado unaendelea na mpaka sasa haijabainika ni silaha gani ilitumika kusababisha kifo chake.
Mambosasa ametoa kauli hiyo leo Machi 30, 2018 baada ya waandishi wa habari kumuuliza ulipofikia uchunguzi wa tukio hilo.
Februari 18, 2018 Mambosasa alisema polisi inawashikilia askari wake sita na silaha zao kwa ajili ya uchunguzi.
Polisi iliunda timu ya upelelezi kuchunguza chanzo cha kifo cha mwanafunzi huyo kilichotokea Februari 16, 2018 wakati polisi wakiwatawanya wanachama wa Chadema waliokuwa wanakwenda ofisi za mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni kushinikiza mawakala wao kupatiwa barua za viapo vyao.
VIDEO-Familia ya Akwilina yatoa ombi kwa Serikali, Ndalichako
"Bado tunaendelea na upelelezi wa tukio hili. Hatujajua ile silaha moja iliyotumika hadi kumpata Akwilina kwa sababu askari walikuwa wengi siku ile na hakukuwa na ushahidi ni yupi aliyetenda kosa hilo,” amesema Mambosasa.
Amesema upelelezi bado haujakamilika na ukiwa tayari umma utaarifiwa.
No comments: