Header Ads

Blogger Tips and TricksLatest Tips And TricksBlogger Tricks

PROFESSOR JAY: ‘MADINGI’ WAPUNGUE BASATA


LEGENDARI, Joseph Haule ‘Professor Jay’ au Mgodi Unaotembea, kama ambavyo anapenda kujiita ni Mbunge wa Jimbo la Mikumi, mkoani Morogoro na yeye binafsi anasema ni mbunge wa binadamu na wanyama.

Anaongoza binadamu na wanyama kwa maana kwamba katika jimbo lake kunapatikana Mbuga ya Mikumi ambapo hata twiga na tembo huwa wanaandamana mbugani hapo.
Wiki hii katika muziki alikovunia umaarufu wake, ameibuka na ujio mpya wa ngoma iitwayo Pagamisa akiwa amemshirikisha Prodyuza T- Touch, huku mkali wa michano Young Dee akitia vionjo pia.

Kuhusu ujio wake mpya Professor Jay ana mengi ya kuzungumzia, lakini pia muziki wake kwa jumla, nini mtazamo wake kuhusu ushirikiano wa wasanii na serikali, mambo aliyofanya jimboni kwake na mengi, teremka naye kwenye makala hii ambayo inapatikana pia Global TV Online!

Showbiz Xtra: Kwanza kabisa nini maana ya neno Pagamisa?
Professor: Pagamisa ni neno la Kizulu linalomaanisha mapambano yanaendelea. Yaani Aluta Continua! Unajua mara kwa mara nimekuwa nikipenda kuwaambia vijana wapambane ili waweze kufika kule wanakotaka. Kwa hiyo ni wimbo mwingine ambao unawahamasisha.

Showbiz Xtra: Kwenye kiitikio amekaa T-Touch, kwa nini yeye na si mtu mwingine? Lakini pia kuna kionjo cha Young Dee kinasikika pia, unaweza kuzungumzia uwepo wake?
Professor: T-Touch ni mtu mwenye heshima sana ninapokuwa ninafanya naye kazi. Wakati ninataka kurekodi nilimsikia akiimba na nikagundua kuna kitu anaweza kukifanya. Sasa sio jambo geni duniani prodyuza kufanya muziki. Tumeona kina Dre na wengi wakifanya hivyo. Kwa hiyo niliona nimpe nafasi aweke kipaji chake nje.

Kuhusu Young Dee ni mtu ambaye anafuatilia kazi zangu na kuniheshimu pia. Mimi pia ninaheshimu kazi za wadogo zangu na vipaji vyao. Kwa hiyo katika kuheshimu ni lazima wapate nafasi kama hivi.
Showbiz Xtra: Wanamuziki wamekuwa ‘busy’ wakitoa albamu, kwako hili limekaa vipi?
Professor: Mimi pia ninampango wa kuachia albamu. Vikao vya bunge vikiisha kwenye mwezi Agosti, kitakachofuata itakuwa albamu yangu iitwayo The Icon.

Showbiz Xtra: Kwenye albamu hiyo tutegemee kuwaona wanamuziki gani wa ndani na nje ya Bongo?
Professor: Ni ‘surprise’, lakini kubwa ni watu wenye ‘talent’ kubwa kwa sababu ni albamu kutoka kwa legendary kwa hiyo inabidi kukaa kiligendari pia.
Showbiz Xtra: Vipi kuhusu shoo, bado unafanya kweli?
Professor: Nilikuwa sifanyi sana kwa maana nilipopata ubunge kuna mambo mengi nilitakiwa kufanya kwa ajili ya wananchi wangu. Lakini kwa sasa mambo mengi nimekwisha yaweka sawa na yanajiendesha, kwa hiyo mapromota waje tu. Wala wasihofie kwa sababu ni mbunge ninapokea mkwanja mrefu wakahofia bei yangu. Tutaelewana tu maana bado ninahitaji kuruka na wanangu majukwaani.

Showbiz Xtra: Hivi Professor ushawahi kufikiri kufanya kazi ya pamoja na wanamuziki wenzio wa ndani na nje ya nchi ambao wanawakilisha wananchi?
Professor Xtra: Ndiyo. Hilo suala lipo. Tuliwahi kukaa mimi, Sugu, Vick Kamata, Jaguar na Bobi Wine na kujadili kufanya kazi ya pamoja ikiwemo kufanya ziara. Lakini bado hatujafanikiwa kwa sababu mabunge yetu yapo tofauti. Tukisubiri Kenya bajeti ipite, Bongo ndiyo inakuwa wakati wake au Uganda. Kwa hiyo tutaangalia namna ya kulifanya hili mpaka liwezekane.
Showbiz Xtra: Hivi karibuni pia kulikuwa kuna majibizano kati ya Diamond na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza, kama sakata hili ulilifuatilia una maoni gani?

Professor: Sitazungumzia sana kuhusu mvutano wao lakini nitatoa maoni yangu kuhusu kinachosababisha haya yote. Mimi ninaona tatizo lipo Basata. Wapo watendaji ambao wamepitwa na wakati. Ndiyo wanaosababisha kazi za wasanii kufungiwa mara kwa mara. Sasa kuna haja kwenye baraza hilo wawekwe vijana ambao wanafahamu nini kinafanyika katika dunia ya leo, hili litasaidia na hakutakuwepo kwa malalamiko kama hayo ya Diamond.      
Showbiz Xtra: Tukihama kwenye muziki, unazungumziaje hali ya kisiasa nchini na kwa viongozi wa wapinzani mmekuwa mkilalamika kutokuwepo kwa uhuru wa kuzungumza?

Professor: Hali ya kisiasa ndiyo kama hivyo kila mmoja anavyoiona. Hakuna uhuru wa kuzungumza kila kona nchini. Kuanzia kwenye vyombo vya habari, viongozi wa kisiasa na hata wananchi. Bila shaka wote tunaona hali anayopitia Mbunge Joseph Mbilinyi. Ni mlengo uleule wa kukosekana kwa haki.
Showbiz Xtra: Ninakushukuru sana Professor kwa time yako.
Professor: Asante pia kwa Gazeti la Amani na Global TV Online kunipa nafasi na kusapoti kazi zangu. Amani sana!

 NA GPL

No comments: