RAIS MAGUFULI AWATAJA VIONGOZI ‘VILAZA’
RAIS John Magufuli amefunguka na kuwaambia viongozi wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kuwa ni vilaza baada ya kugundua Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imekuwa kikwazo kwa Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
Rais Magufuli amesema hayo jijini Dar, leo Machi 26, 2018 wakati akizindua magari 181 ya Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ambayo yanategemewa kuanza kusafirisha dawa mijini na vijinini, baada ya kupokea malalamiko kuwa zipo baadhi ya taasisi za serikali zimekuwa zikichangia kukwamisha kwa kuchelewesha dawa ambazo zinazoingizwa nchini na Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
“Nimesikia saa zingine kunakuwa na ucheleweshwaji kati ya taasisi fulani ndani ya serikali. Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), mnaleta madawa halafu mnashindwa kupata kibali bandarini. Madawa yanacheleweshwa inawezekana ‘expiry date’ yake inafika, bado yamezuiliwa pale bandarini. Atakayezuia madawa haya niambieni ili nijueni chombo gani cha serikali kinachohusika ili na mimi nimzuie moja kwa moja,” alisema Magufuli.
Magufuli aliendelea kuweka wazi kuwa watu ambao wanakwamisha dawa huzo wanatoka katika wizara hiyohiyo wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.
“Hata aliyempa nguvu ya kuzuia dawa yupo chini ya wizara yenu, yaani ni nyinyi wenyewe, basi nyinyi vilaza, mtu anayezuia yupo kwako, anayezuiliwa yupo kwako, bado mnakaa mnaimba nini? Nataka haya niyashughulikie.
“Mambo mengine mnakwamishana nyinyi wenyewe, kama ni TRA mwambie Katibu Mkuu, mwambie Waziri wa Afya, mwambie Waziri wa Fedha tufike mahali tusikwamishane, kwa sababu anaweza akawa amekwamisha madawa yenu lakini madawa ya mtu binafsi anayaruhusu siku hiyohiyo, sasa hili ni lenu wala halihitaji kufika kwangu,” alisema Magufuli.
No comments: