SAKATA LA KUFUNGIWA, ISHU YA DIAMOND KUHAMA NCHI YAZUA MJADALA
HAPATOSHI! Ndivyo unavyoweza kusema. Siku chache baada ya serikali kufungia nyimbo zake mbili, mkali wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ ameibuka na kujibu mapigo hali ambayo imesababisha gumzo la aina yake mitandaoni.
Februari mwaka huu, Mamlaka ya Mawasiliano nchini TCRA ilitangaza kuzifungia nyimbo 15 za wasanii mbalimbali zikiwemo mbili za Diamond, Hallelujah na Waka Waka.
TCRA ilizifungia nyimbo hizo baada ya kupokea orodha yake kutoka Baraza la Sanaa (Basata) waliosema hazina maadili.
Baada ya kufungiwa, Diamond alisafiri kwenda nchini Kenya na kuzindua albamu yake ya A Boy From Tandale ambayo ndani yake ina nyimbo hizo mbili zilizofungiwa.
Hata hivyo, akiwa nchini humo, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza alinukuliwa na Redio Clouds FM, akisema hairuhusiwi msanii yeyote aliyefungiwa, kuimba zile nyimbo zilizofungiwa ndani na hata nje ya nchi.
Akijibu mapigo juzi kupitia Redio Times FM, Diamond alianza kwa kusema kuwa anashindwa kuelewa baadhi ya viongozi wa serikali wanaokurupuka na kufungia nyimbo bila kukaa na kuzungumza nao.
“Mtu anakurupuka tu anafungia wimbo. Hajui changamoto zetu, sijui anatafuta sifa tu anafungia,” alinukuliwa Diamond.
Kama hiyo haitoshi, katika mahojiano hayo yaliyofanyika wakati akiitambulisha albamu yake hiyo ya A Boy From Tandale kwa mara ya kwanza nchini, Diamond alisema anawaheshimu viongozi wengi wa serikali wanaofanya kazi kwa uchunguzi na data za kutosha lakini si aliyefungia nyimbo zake.
“Mbona kuna viongozi wengi tu tunawaheshimu kama Waziri Mwakyembe (Harrison), au mtu kama Makonda (Paul) yaani unaona yale wanayoyafanya hawakurupuki, wanafanya utafiti, siyo mtu unakurupuka hujui mimi nimetumia fedha kiasi gani au nimewekeza kiasi gani.
“Unajua hawa viongozi wanapaswa kukaa na sisi. Kuzungumza na sisi wajue changamoto zetu. Kiongozi anaibuka tu anafungia. Na mimi niseme tu, kiongozi anaweza kuwa kweli amesoma, amenizidi elimu au umri lakini katika suala la muziki nikawa naufahamu zaidi. Aite wasanii wakubwa kama kina Kiba, kina Joh Makini tuzungumze asitafute kiki tu,” alisema Diamond.
Akizidi kutiririka, Diamond alisema alisikitika kumuona kiongozi huyo hata baada ya yeye kufungiwa, akiwa nchini Kenya akasikia anachonga redioni (hakumtaja jina).
“Mimi niko zangu kule namsikia mtu tena huku sijui anachonga chonga tu. Unanifungia mimi muziki ili iweje? Unajua mimi nina familia, unamfungia Roma miezi sita unajua changamoto anazopitia? Anakula nini anaishi vipi?
“Unanifungia mimi umewahi kusaidia kitu gani kwenye muziki wangu? Utamnunulia Tiffah (bintiye) pampas? Mimi simuogopi, niko tayari hata kufungwa jela lakini nitaupigania huu muziki. Simuogopi, atakuja hapa sisi atatuacha,” alisema Diamond.
Kwenye mahojiano hayo Diamond alisema haoni tatizo kufungiwa kwani anaweza kwenda kufanya muziki wake nje ya nchi na akaishi.
“Mimi naweza nikaenda hata nje ya nchi nikaishi nikafanya muziki sasa nani ataathirika?”
Baada ya kusema hayo, mitandao mbalimbali ya kijamii ‘ilichafuka’ ambapo watu mbalimbali waliweka picha yake na Waziri Shonza huku kila mmoja akionesha hisia zake.
Kuna ambao walikuwa wanampongeza Diamond kwa kitendo chake cha kutetea muziki, kuna wengine walikuwa wakiikosoa serikali kwa kitendo cha kumfungia Diamond pamoja na wasanii wengine.
Zaidi, watu wengi walionekana pia kuijadili ishu ya Diamond kuhama nchi na kwenda kufanya muziki wake nje ya nchi. Wapo waliosema si jambo zuri, wengine walisema ni sawa tu hata akienda huku wengine wakisema hata akienda nje ya nchi sheria itamfata huko huko.
Risasi Mchanganyiko lilimtafuta Waziri Shonza lakini simu yake ya mkononi iliita bila kupokelewa.
NA GPL
No comments: