WANAFUNZI DARASA LA AWALI HADI LA SITA WANASOMA KATIKA CHUMBA KIMOJA MTWARA
Wanafunzi wa darasa awali hadi la sita katika Shule ya Msingi Raha Leo Elimu Maalumu (viziwi) Manispaa ya Mtwara Mikindani wanasoma katika darasa moja, kutokana na kukosekana kwa vyumba vya madarasa.
Pia, darasa hilo linalotegemewa na wanafunzi 25 linatumika kama ofisi ya walimu, stoo na bwalo.
Hayo yameelezwa leo Ijumaa Machi 9 , 2018 na kiongozi wa wanafunzi hao, Twaha Salum wakati wa kupokea zawadi kutoka kwa wanawake wafanyakazi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Tawi la Mtwara, kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani iliyoadhimishwa jana.
Twaha amedai kila wanapotembelewa na wageni wamekuwa wakiwaeleza changamoto zinazowakabili ili kuwatafutia utatuzi lakini inashindikana.
“Darasa hili linatumika na wanafunzi wote wa elimu maalumu, ndiyo stoo, ofisi ya walimu wetu na tunalitumia kama. Changamoto ni nyingi kila wakija wageni tunawaambia lakini hakuna kinachofanyika,”amesema Twaha.
Mwalimu wa kitengo hicho, Caroline Chitunda amesema mbali na changamoto zilizotajwa na mwanafunzi huyo, wanakabiliwa na ukosefu wa bweni na chumba maalumu kwa ajili ya kupimia usikivu wa wanafunzi licha ya kupatiwa vifaa vyote.
“Kama mnavyoona meza moja wanasomea madarasa mawili mawili. Pia tuna uhaba wa vyumba vya madarasa na chumba cha upimaji wa masikio kwa sababu wanaofika kuanza kusoma hapa lazima apimwe usikivu, ni chumba maalumu hakitoi sauti na hakiingizi sauti lakini vifaa vyote tunapatiwa na Serikali,” amesema Chitunda.
Mwalimu mkuu msaidizi, Ally Matola amesema wanafunzi wa madarasa mawili wanatumia mbao moja kwa ajili ya kusoma.
“Mbao moja inatumika wa madarasa mawili,hawa watoto wasio na usikivu kipindi kimoja kinachukua muda mrefu tofauti na wale wenye usikivu kamilifu, walimu wanapokezana kufundisha unakuta vipindi kwa siku havikamiliki,” amesema Mwalimu Matola.
Ofisa Habari wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Jamadi Omari amesema wanatambua changamoto zinazoikabili shule hiyo na kwa sasa wameanza kutafuta ufumbuzi wa vyoo kwanza.
“Tunalifahamu lakini manispaa tuna changamoto nyingi na katika Shule ya Raha Leo tumeanza na vyoo kwanza kwa sababu ni tatizo na tunafanya kwa awamu kutatua changamoto zilizopo,”amesema Omari.
Wakina mama wa BoT Tawi la Mtwara wamekabidhi sukari, unga, mafuta ya kula, majani ya chai, biskuti, shuka, maharagwe, mchele na juisi ambazo fedha zimetokana na kujichanga kwa wafanyakazi wakiwamo wanaume.
Mwenyekiti wa kamati ya kina mama, BoT Tawi la Mtwara, Zakia Juma ameiomba jamii kujitokeza na kuwatembelea watoto wenye uhitaji maalumu kwani na wao wanahitaji upendo.
No comments: