BI HARUSI ATOWEKA NA MICHANGO!
ARUSHA: Mrembo aliyejulikana kwa jina la Doreen Aloyce, anadaiwa kutoweka na michango ya harusi, hali iliyosababisha wachangiaji kucharuka.
Chanzo makini kililiambia Ijumaa Wikienda kuwa mwanadada huyo alichangisha michango kwa watu mbalimbali kwa ajili ya harusi yake, lakini baada ya kupatiwa haikujulikana harusi iliyeyukia wapi.
Wakizungumza baadhi ya wachangiaji hao walimlalamikia Doreen kuwa wanaona tu picha za harusi huku wakiwa hawajaalikwa siku ya tukio wakati walichangia pesa zao. “Yaani kwa jumla sisi watoa michango tunashangaa tumechangishwa michango na kwa kuwa sisi ni shoga yetu na alituomba tumchangie michango kwa ajili ya ndoa na kwa kuwa ni jambo la heri tukachanga, lakini siku zilivyozidi kwenda tukaona kimya.
“Kilichotushtua na kutushangaza zaidi ni baada ya kuona anatuma tu picha za harusi kwenye ukurasa wake wa Instagram akionesha picha kwamba ameshafunga ndoa. “Kutokana na hilo ikabidi tuanze kuulizana kama kuna mtu kati yetu ambaye amehudhuria, lakini kila mmoja alikataa, tukabaki tunajiuliza kwa nini ametufanyia hivi?“Michango ametuchangisha na picha zenyewe bwana harusi sura yake haionekani, kitu ambacho kimetutia shaka pia kuwa hii ndoa huenda amechukua michango yetu na kupiga picha tu akiwa amevaa shela ili tuone kuwa ameshafunga ndoa.
“Tunachotaka sisi ni michango yetu airudishe na siyo vinginevyo,” alisema mmoja wa wachangiaji wa harusi hiyo kwenye kundi la WhatsApp. Ili kuujua ukweli wa madai hayo, Ijumaa Wikienda lilimtafuta bi harusi huyo ambaye alisema yupo Zanzibar kwenye mapumziko baada ya kufunga ndoa.
Alieleza kuwa kuna sababu iliyomfanya kufunga ndoa hiyo, lakini alipotakiwa kutaja jina la mumewe alikataa. “Ni kweli nilifanya michakato ya harusi yangu, kwa hiyo nilifanya harakaharaka kwa kuwa mume wangu alikuwa nchini Sweden, niliwachangisha watu kweli, lakini ulitokea msiba kwenye familia yangu na ikabidi tusogeze mbele kila kitu wanajua.
“Kwa hiyo mume wangu alikuja huku ikabidi tufunge ndoa harakaharaka kwa sababu ya msiba.“Wachangiaji walianza kunipigia simu na kusema mbona situmi picha na wao walitaka waje wale na kunywa, kwa nini nimefungia ndoa mbali yaani Zanzibar, lakini niliwapa taarifa kuhusu kusogeza mbele tarehe ya harusi.
“Sasa wakaanza kusema kwamba mimi nimeposti picha, lakini sura ya mume wangu nimeificha. “Ni kweli nilificha sura ya mume wangu kwa sababu kwa mila zetu na pia najua mimi ni mwandishi wa habari nilishaelekezwa na wakongwe wa tasnia ya uandishi kuwa nisimuanike mume wangu kwa kuwa itakuja kuwa shida waandishi watamfuatafuata mpaka nyumbani.
“Baada ya kupata simu zao wakinilalamikia nilimweleza mume wangu akaniambia niwaambie waandike majina yao ili tuweze kuwarudishia pesa zao kwa sababu mtu anapoanzisha jambo kubwa kama hilo, lazima awe amejiandaa, michango ni ya ziada tu hivyo ninawarudishia michango yao,” alisema Doreen ni mwandishi wa habari mkoani Arusha.
NA GPL
No comments: