Header Ads

Blogger Tips and TricksLatest Tips And TricksBlogger Tricks

HAWA ‘WA DIAMOND’ ARUDIA UWANJA WA NDEGE AKIENDA INDIA KUTIBIWA

 Msanii Hawa Said maarufu ‘Hawa Nitarejea’ jana alijikuta akirudia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam, baada ya kutotimiza vibali vya kusafiri vya matibabu kwenda nchini India.


Akizungumza na Mwananchi kuhusu kukwama kwa safari ya nyota huyo, meneja wa mwanamuziki Diamond Platinumz ambaye ndiye amechukua jukumu la kugharamia matibabu hayo, Babu Tale alisema hali hiyo iliwakuta wakiwa tayari wameingia ndani ya uwanja wa ndege na kuanza kukaguliwa nyaraka zao.


Babu Tale alisema nyaraka mojawapo iliyowakwamisha kusafiri ni kibali cha daktari kuelezea hali ya mgonjwa ili wahudumu ndani ya ndege wajue namna watakavyomhudumia.


“Kuna mgonjwa anaweza akawa katika hali ya kuzimia, kutapika anatakiwa ahudumiwe tofauti, hivyo Hawa imeshindikana kwa kuwa hakuna hiyo nyaraka inayoonyesha hivyo kutoka kwa daktari na wametuambia turudi itakapokamilika,” alisema.


Hawa na mama yake, Ndagina Hassan pamoja na Babu Tale ilikuwa waondoke jana saa 10:45 jioni kwa ndege ya Shirika la Emirates.


Nyota huyo wa muziki alifika uwanjani hapo akiwa na mama yake saa saba mchana huku Babu Tale akiwasili saa tisa alasiri.


Mwananchi lililokuwa limepiga kambi wakati wote uwanjani hapo lilifanikiwa kuzungumza na Mama Hawa ambaye alielezea furaha yake juu ya mwanaye kupata msaada wa matibabu.


Kwa upande wake Hawa aliwaomba Watanzania kumuombea katika matibabu hayo.


Awali, Babu Tale alisema walitarajia kuwa nchini humo kwa wiki mbili na huenda msanii huyo akapandikizwa ini kama madaktari watashauri hivyo.


Hawa anasumbuliwa na ugonjwa wa kujaa maji tumboni unaoelezwa kuwa unatokana na kuwa na tatizo la ini.


Kutokana na ugonjwa huo ameshalazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) zaidi ya mara nne na kutolewa maji tumboni.


Septemba 29, Diamond ambaye jina lake halisi ni Naseeb Abdul kupitia ukurasa wake wa Twitter alieleza kuwa ameamua kumsaidia ili aweze kupata matibabu zaidi na kuwa yatagharimu wastani wa Sh50 milioni.


MWANANCHI

No comments: