HIVI NDIYO ULINZI NYUMBANI KWA MO DWEWJI ULIVYOIMARISHWA!
GUMZO kubwa kwa sasa ni tukio la kutekwa kwa bilionea mkubwa Tanzania, Mohammed Dewji ‘Mo’ ambapo utekaji huo umesababisha ulinzi mkubwa kuwekwa nyumbani kwake, Masaki jijini Dar es Salaam, Risasi limejionea.
Mo alitekwa juzi, Alhamisi ya Oktoba 11, 2018 alfajiri na wazungu wasiojulikana akiwa katika eneo la Hoteli ya Colloseum iliyopo Oysterbay jijini Dar ambapo alifika kwa ajili ya kufanya mazoezi.
Baada ya tukio hilo lililotikisa nchi, waandishi wetu walifika nyumbani kwa tajiri huyo ili kuzungumza na ndugu, jamaa na marafiki akiwemo mkewe lakini walikutana na mazingira magumu kufuatia walinzi wa Kampuni ya KK Security kutanda kila kona.
“Kama siyo ndugu huruhusiwi kupita hapa, mnajua hali siyo shwari kwa hiyo kama unajijua huhusiki eneo hilo, chapa lapa,” alichimba mkwara mmoja kati ya askari hao. Wakati waandishi hao wakiangalia ustaarabu wa kuondoka eneo hilo ili kuepusha shari, mmoja wa walinzi alisikika akimwambia mwenzake kuwa, inabidi wawasiliane na ofisi kuu ya kampuni yao ili kuimarisha zaidi ulinzi kutokana kile kilichotokea.
Akizungumza na Risasi, jirani wa Mo aliyejitambulisha kwa jina la Fred, alisema tangu bilionea huyo kijana atekwe, nyumbani hapo ulinzi umeongezeka. “Leo walinzi wameongezwa, tena wenye silaha na ndiyo maana huoni mtu akirandaranda pale, kama siyo ndugu kuingia mle ndani sasa hivi ni shughuli pevu, utakaguliwa mpaka basi,” alisema jirani huyo na kuongeza:
“Unajua waliomteka hawajajulikana ni akina nani na walikuwa na nia gani, kwa hiyo hata mkewe na ndugu zake wengine wamewekewa ulinzi mkali maana isije ikatokea na wao wakatekwa.” Jinsi alivyotekwa Taarifa zilieleza kuwa, Mo ambaye ni mwekezaji wa Klabu ya Soka ya Simba ya jijini Dar, alitekwa alipokuwa akiingia ‘gym’ katika Hoteli ya Colloseum na kwamba waliomteka walifika mapema kisha alipofika walimchukua na kupiga risasi juu na kuondoka naye.
“Mara tu baada ya kushuka kwenye gari lake alilofika nalo aina ya Range Rover lenye rangi nyeusi ndipo wakatokea watu hao wasiojulikana kisha wakamchukua, wakapiga risasi juu na kuondoka naye kuelekea kusikojulikana,” alisema mmoja wa mashuhuda bila kutaja jina.
DEREVA ASIMULIA
Dereva wa usafiri wa kukodi wa Uber wa jijini Dar aliyeshuhudia utekaji huo, naye alisema kuwa alikuwa akiingia kwenye hoteli hiyo kumshusha abiria wake na ilikuwa majira ya saa 11:00 alfajiri ndipo alipokutana na tukio hilo. Tulikuwa tunakaribia pale hotelini, mara mbele yetu tukaona watu wanne wameshuka kwenye gari ndogo.
“Watu hao walikuwa wamejifunika vitambaa usoni, wakapiga risasi moja juu. “Baada ya kupiga risasi hewani, wale askari wa hotelini walikimbia. “Ndipo wale watu wanne wakaingia hotelini na kutoka na mtu ambaye tulimtambua kuwa ni Mo,” alisimulia dereva huyo aliyeomba jina lake lisitajwe gazetini.
TAMKO LA POLISI
Wakati gazeti hili likienda mtamboni, Jeshi la Polisi kupitia kwa Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa lilieleza kuwa, jitihada za kuhakikisha Mo anapatikana zinaendelea.
“Kuna baadhi ya watu tunawashikilia kuhusiana na tukio hilo kwa ajili ya mahojiano lakini kwa sasa siwezi kutaja idadi yao lakini tumejipanga vilivyo katika mikoa yetu yote mitatu. Ukaguzi unaendelea kufanyika katika vizuizi vyote vya barabarani ili kuhakikisha hakuna mhusika yeyote wa tukio hilo ambaye atapata nafasi ya kukimbia,” alisema Mambosasa na kuwaomba wananchi kuwa watulivu na kuendelea kushirikiana na polisi kwa karibu na kwamba taarifa rasmi za tukio hilo watazipata kutoka jeshi la polisi na siyo kwingine.
MO NI NANI?
Mo ni Mkurugenzi wa Makampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Lmited (MeTL), ni mwekezaji wa Klabu ya Simba akiwa na hisa ya asilimia 49 na amekuwa akiingia kwenye chati ya juu ya Jarida la Forbes kama miongoni mwa matajiri vijana barani Afrika.
KUHUSU UTEKAJI NCHINI
Matukio ya utekaji nchini yanayowakuta raia wasio na hatia yameanza kuonekana miaka mingi iliyopita, lakini sasa yanataka kushamiri nchini. Hata hivyo, kwa mwaka huu yanaonekana kushamiri kwa watu mbalimbali hadi kufikia hatua ya kujadiliwa ndani ya vikao vya Bunge, lakini bado yanaendelea.
Wakati tukio la Mo likiendelea kutikisa baadhi ya watu wamewashauri matajiri kuwa makini na maisha yao kutokana na ukweli kwamba wako hatarini kufanyiwa matendo ya kihalifu likiwemo suala la kutekwa. Hatari ya matajiri kutekwa imeelezwa kuwa inatokana na uwepo wa makundi ya maharamia kuwawinda ili wajipatie fedha kupitia njia haramu ya utekaji nyara.
“Matajiri wanatakiwa kuwa makini kwasababu matukio kama haya yamekuwa yakitokea sehemu mbalimbali duniani kwa matajiri, watoto wao kutekwa na wahalifu na baadaye kuomba wapatiwe fedha ili wawaachie huru mateka,” Alisema Alfred Massawe alipozungumza na gazeti hili jana kuhusiana na sakata la bilionea Mo kutekwa.
NA GPL
No comments: