LEMA AFUNGUKA MO DEWJI KUTEKWA, A-Z KILICHOTOKEA! – VIDEO
MBUNGE wa Arusha Mjini wa (CHADEMA) na Waziri Kivuli wa Mambo ya Ndani, Godbless Lema, amesema serikali inao wajibu mkubwa wa kuleta wachunguzi wa kimataifa kwa ajili ya kufanya upelelezi wa tukio la kutekwa kwa mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewj (Mo) na watu wasiojulikana Alhamisi iliyopita, Oktoba 11, 2018 katika eneo la Hoteli ya Colosseum eneo la Oyster Bay jijini Dar es Salaam.
Lema ameyasema hayo leo Oktoba 16, makao makuu ya ofisi za Chadema jijini Dar es Salaam na kubainisha kwamba eneo alilotekwa Mo ni jirani na nyumba za viongozi wakubwa wa serikali na lina ulinzi mkubwa, hivyo polisi wana uwezo wa kuwapata watekaji hao kwa kutumia footage za camera.
Mbunge huyo amesema suala la utekaji na mashambulizi kwa nchi hii limekuwa kama suala la kawaida na waziri anazo takwimu. Ben Saanane alipotea Novemba 2016, Azory akapotea Novemba 2017, Tundu Lissu akashambuliwa kwa risasi, Septemba 2017, mapaka leo yupo Ubelgiji akipatiwa matibabu.
“Tukio la Tundu Lissu kupigwa risasi, wachunguzi kutoka nje walizuiliwa; tukio hili la kutekwa kwa Mohammed Dewji, Waziri Lugola amesema hakuna haja ya wachunguzi wa nje. Sisi tunataka wachunguzi wa nje ili kubaini nani anahusika na matukio haya ya utekaji nchini.
“Leo tunaambiwa wapelelezi wa kimataifa hawahitajiki, naamini familia ya Mohammed Dewji ina uwezo hata wa kulipia gharama yoyote kulipia private investigators (wapelezi binafsi) wa kimataifa kusaidiana na wa hapa kuchunguza tukio hili, lakini Serikali haikubali.
“Ni utamaduni duniani kote linapotokea tukio kama hili na kama eneo la tukio kuna kumbukumbu za kamera, huwa wanatoa footage za kamera kupeleka kwenye vyombo mbalimbali vya habari ili iwe rahisi kwa wananchi kuwatambua wautuhumiwa,” alisema Lema.
Akizungumzia kuhusu waziri kuzuia mijadala ya matukio ya utekaji wakati jeshi la polisi likiendelea na uchunguzi kuwasaka watuhumiwa, Lema amesema jambo hilo ni sawa na kuzuia watu kulia kwenye msiba, na kwamba huu ni ‘msiba’ wa nchi. Mtu mmoja hata kama ni kichaa anaokota makopo, thamani yake ni kubwa sana haijalishi uwezo wake wa fedha.
“Kukaa kimya wakati watu wanapotea siyo jambo la la busara, ushauri wangu ni kwamba, mtu yeyote anapoonewa wakati wowote ni lazima kupiga kelele. Tulipata wakati mgumu Chadema, leo mambo yamegeuka hadi kwa wafanyabiashara. Wito wangu kwa viongozi wote wa dini na taasisi za kiraia watoke wapige kelele kwa sauti ili Mohammed Dewji apatikane. Akina Mzee Reginald Mengi watoke, wafanyabiashara wote na nyie wanahabari mtoke mpige kelele.
“Kama tukio la Mohammed Dewji halitapatiwa majibu, kuna uwezekano wa wafanyabiashara wengine wakubwa kuogopa na kukimbia nchini wakihamisha mitaji ya biashara zao, matokeo yake tunaweza kudidimiza uchumi wetu kama ilivyokuwa kwa Zimbabwe,” amesema Lema.
No comments: