UPASUAJI WA KWANZA DUNIANI WAFANYIKA BILA DAKTARI
Dunia inakwenda kasi sana, sayansi na teknolojia vinazidi kufanya miujiza mingi ambayo miaka michache iliyopita ilikuwa haiwezekani, sasa inafanyika kwa ufanisi wa hali ya juu.
Hebu vuta picha, mgonjwa anayesumbuliwa na matatizo ya moyo, aingizwe chumba cha upasuaji katika Hospitali ya Rufaa Mbeya tayari kwa oparesheni lakini daktari anayetakiwa kumfanyia upasuaji yupo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na anataka kufanya kazi hiyo bila kufika Mbeya! Bila shaka utaona ni jambo lisilowezekana si ndiyo?
Basi kwa taarifa yako, kwa mara ya kwanza katika historia ya utabibu duniani, upasuaji wa kwanza wa aina hiyo, umefanyika kwa ufanisi mkubwa, yaani daktari yupo mji mwingine na mgonjwa yupo mji mwingine lakini daktari anamfanyia upasuaji wa moyo mgonjwa wake kwa kutumia teknolojia tu.
Teknolojia hiyo iliyopewa jina la Corpath katika upasuaji uliopewa jina la Telerobotic Coronary Intervention imefanyika nchini India, na kuweka rekodi ya aina yake.
Daktari Tejas Patel ambaye pia ni mwenyekiti na mkuu wa kitengo cha upasuaji wa kisasa wa moyo katika Taasisi ya Apex Heart Institute iliyopo Ahmedabad nchini India ndiye aliyekuwa ‘stering’ katika upasuaji huo uliofanyika Desemba, mwaka huu.
Aliyefanyiwa upasuaji huo ni kiongozi wa kidini wa madhehebu ya Kihindu ya Swaminarayan Akshardham, Pramukh Swami Maharaj aliyekuwa katika hekalu la dhehebu hilo lililopo umbali wa kilometa 32 kutoka Apex Heart Institute, Ahmedabad, alipokuwa daktari huyo.
Kwa sababu upasuaji huo ni wa kwanza duniani, ililazimu timu ya madaktari wa dharura wawepo kando ya mgonjwa ili endapo teknolojia itashindwa kufanya kazi yake, wawe tayari kutoa msaada wa kuokoa maisha ya mgonjwa, hasa ukizingatia kwamba kiungo kilichokuwa kinafanyiwa upasuaji ni moyo, ambao hitilafu ndogo tu inaweza kusababisha kifo.
Hata hivyo, kwa kutumia vifaa maalum vilivyokuwa vikifanya kazi zote zinazotakiwa kufanywa na jopo la madaktari na manesi (robots), daktari huyo aliyekuwa amekaa nyuma ya kompyuta yake akiyaongoza marobots kufanya kile alichotaka kifanyike, upasuaji ulifanyika kwa mafanikio makubwa na kuingia katika rekodi za dunia.
Kufanikiwa kwa upasuaji huo kunafungua ukurasa mpya katika fani ya utabibu ambapo sasa, hakutakuwa tena na ulazima wa mgonjwa aliyepatwa na matatizo ya moyo, kama kupanda au kushuka ghafla kwa shinikizo la damu, kusafirishwa umbali mrefu na kwa muda mrefu kwenda kutafuta huduma kwa madaktari wenye uzoefu na magonjwa ya moyo.
Uzuri ni kwamba, kwa kutumia teknolojia hiyo iitwayo Corpath Technology daktari atakuwa na uwezo wa kuwahudumia wagonjwa wengi zaidi kwa wakati mmoja, akiwa amekaa tu nyuma ya kompyuta yake. Hata wagonjwa waliopo vijijini wataweza kupatiwa huduma za dharura za magonjwa ya moyo, kwa kukimbizwa kwenye vituo vya afya vilivyofungwa telerobotics system kisha daktari popote alipo akamhudumia mgonjwa kwa ufanisi wa asilimia 100.
Mark Toland, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Corindus ambao ndiyo wagunduzi wa teknolojia ya Corpath, amenukuliwa akisema malengo yao ni kuhakikisha teknolojia hiyo inasambaa dunia nzima na kuokoa maisha ya mamilioni ya watu wanaopoteza maisha yao kwa sababu ya kukosa huduma za dharura za magonjwa ya moyo.
No comments: