WALICHOONGEA RAIS MAGUFULI NA KENYATTA BAADA YA KUKUTANA LEO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Kenya Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta wamewaagiza Mawaziri wa Tanzania na Kenya kutatua tofauti ndogondogo zinazojitokeza katika biashara kati ya nchi hizi mbili.
Marais hao wametoa maagizo hayo leo asubuhi tarehe 23 Februari, 2018 walipokutana na kufanya mazungumzo katika hoteli ya Munyonyo mjini Kampala muda mfupi kabla ya kuanza kwa vikao vya mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Mhe. Rais Magufuli na Mhe. Rais Kenyatta wamesema wanataka kuona biashara kati ya Tanzania na Kenya inazidi kukua na bidhaa zinauzwa na kununuliwa baina ya nchi hizo bila vikwazo vyovyote na hivyo kuagiza tofauti zilizojitokeza katika baadhi ya bidhaa zimalizwe.
“Kuna mambo madogomadogo yanakuwa yanajitokeza katika biashara kati ya Kenya na Tanzania, tunataka kwa haya yote Mawaziri wa Kenya na Mawaziri wa Tanzania mkae myatatue, sisi hatuna tatizo, mambo mengine madogomadogo mno, mambo ya viatu, nguo, ngano, gesi ni madogo sana, mnatakiwa myatatue nyinyi yasifike kwetu, sisi huku tuko sawasawa” amesema Mhe. Rais Magufuli na kuungwa mkono na Mhe. Rais Kenyatta.
Wametoa maagizo hayo kwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Dkt. Augustine Mahiga, Waziri wa Katiba na Sheria wa Tanzania Prof. Palamagamba Kabudi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya Balozi Monica Juma na Waziri wa Afrika Mashariki na Maendeleo ya Ushoroba wa Kaskazini wa Kenya Mhe. Peter Munya.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Sudani Kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit katika hoteli ya Munyonyo Mjini Kampala.
Baada ya Mazungumzo hayo Mhe. Rais Magufuli amesema Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine za Afrika Mashariki inaguswa na hali ya Sudani kusini na ametoa wito kwa pande zinazopingana kumaliza tofauti zao ili wananchi wa Sudani Kusini wajikite kujenga nchi yao.
“Nimemhakikishia Mhe. Rais Salva Kiir kuwa Tanzania ipo pamoja na Sudani Kusini na tunapenda tofauti zinazosababisha matatizo nchini mwake ziishe, sisi Tanzania tupo tayari kufanya biashara na Sudani Kusini, hata chakula kama wanahitaji tutawauzia” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Kwa upande wake Mhe. Rais Salva Kiir Mayardit amesema Tanzania na Sudani Kusini zina uhusiano wa kihistoria tangu enzi ya Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius Kambarage Nyerere na kwamba japo kuna vita nchini mwake Mhe. Rais Magufuli amemhakikishia kuwa uhusiano na ushirikiano huo utaendelezwa na kukuzwa zaidi.
Katika hatua nyingine, Mhe. Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Burundi Mhe. Gaston Sindimwo.
Mhe. Gaston Sindimwo amemfikishia ujumbe wa Rais wa Burundi Mhe. Pierre Nkurunziza kuwa hali ya Burundi ni shwari na Mhe. Rais Magufuli amesema anafurahi kuona sasa wakimbizi wa Burundi waliokuwa wamepata hifadhi Tanzania wameanza kurudi nchi kwao.
Mhe. Rais Magufuli pia amefanya mazungumzo na Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Tanzania Mhe. Benjamin William Mkapa ambaye ni mratibu wa mazungumzo ya amani ya mgogoro wa Burundi aliyealikwa kuhudhuria mkutano wa 19 wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki hapa Kampala.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kampala
23 Februari, 2018
No comments: