WANANCHI WAMKATAA MKUU WA WILAYA MBELE YA WAZIRI MKUU
WANANCHI wa wilaya ya Kwimba wamemuomba Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aondoke na mkuu wa wilaya hiyo Bw. Mtemi Msafiri baada ya kutoridhishwa na utendaji wake.
Wametoa ombi hilo jana (Ijumaa, Februari 16, 2018) walipozuia msafara wa Waziri Mkuu alipowasili katika Ofisi za Halmashauri ya wilaya Kwimba zilizopo Ngudu kwa ajili ya kuzungumza na watumishi akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza.
Wananchi hao walimkataa mkuu wao wa wilaya Bw. Msafiri kupitia ujumbe wa mabango 17, ambapo Waziri Mkuu amewataka wananchi hao wawe watulivu wakati Serikali inafanyia kazi malalamiko yao.
Wananchi hao wanadai kwamba Mkuu huyo wa Wilaya anatabia ya kuamrisha polisi wawakamate kwa kisingizio cha uzururaji na kisha wanawekwa mahabusu, ambapo baada ya muda wanatolewa na kwenda kulima kwenye shamba lake.
Waziri Mkuu amesema Serikali inahitaji kila mtumishi atambue majukumu yake na ayatekeleze. “Hakuna atakayeonewa, haki zenu zote tunazitekeleza nanyi mnatakiwa kutenda haki kwa kuwatumikia wananchi.”
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka Mkuu huyo wa wilaya Bw. Msafiri, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Kwimba Bibi Pendo Malebeja na wakuu wote wa Idara wajitathmini kama kweli wanatekeleza majukumu yao ipasavyo na kuwatumikia wananchi.
“Mkurugenzi katika kipindi chako chote cha utendaji kuanzia mwaka 2013 hadi leo, fedha nyingi za Serikali zilizoletwa Kwimba zimepotea na hazijulikani zilipo huku miradi mingi bado haijakamilika na muda wote huo Halmashauri imekuwa inapata hati chafu.”
Pia Waziri Mkuu amewataka watumishi wote wa Halmashauri ya wilaya ya Kwimba wabadilishe mienendo yao na wawatumikie vizuri wananchi pamoja na kuishi nao vizuri.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU
IJUMAA, FEBRUARI 16, 2018.
No comments: