HOFU UPYA VIFO VYA WASANII
UPEPO siyo mzuri! Unaweza kutamka maneno hayo kutokana na hali inayoendelea kwa mastaa Bongo baada ya wenzao wanne kufariki dunia ndani ya wiki moja na kuzua hofu upya kwa wasanii mbalimbali, Risasi Mchanganyiko linakupa habari kamili.
Mastaa mbalimbali wana hofu ya kifo kwa sababu ya wenzao hao kuondoka mfululizo na kufananisha na vifo vilivyowahi kutokea mwaka 2012 mpaka 2014 ambapo mastaa wengi walifariki akiwemo Steven Kanumba, Hussein Ramadhan ‘Sharo Milionea’, John Maganga, Albert Mangwea, Rachel Haule, Adam Kuambiana na wengine wengi.
“Jamani Mungu tu atusamehe maana hivi vifo vya mfululizo namna hii vinatupa hofu kubwa sana maana vinatukumbusha miaka iliyopita ambayo tuliwapoteza wenzetu wengi ambao pengo lao halizibiki mpaka sasa,” alisema msemaji wa Chama cha Waigizaji Kinondoni, Masoud Kaftany.
MISIBA YA WANNE
Ndani ya wiki moja kulitokea misiba ya wasanii wanne wakiwemo wa muziki na filamu ambapo alianza msanii wa maigizo wa zamani kutoka kundi la Kaole, Zena Dirp maarufu kwa jina la Bi.Sauda au Mama Cheni ambaye alifariki Aprili 17, mwaka huu.
Baada ya msiba huo wa pili aliyefuatia ni aliyekuwa video queen na msanii wa filamu Bongo, Agness Gerald ‘Masogange’ ambaye kifo chake kilimshtua kila mtu kwani aliugua kwa siku nne tu na kufariki dunia Aprili 20, mwaka huu. Kifo kilichofuata ni cha msanii wa filamu aliyeshiriki kwenye tamthiliya ya Jumba la Dhahabu, Dalila aliyefariki dunia katika Hospitali ya Temeke, Aprili 21, mwaka huu.
Msiba wa nne ni wa msanii wa Bongo Fleva, Jebby ambaye alifariki dunia Aprili 22, mwaka huu huko nyumbani kwao Dodoma. Kutokana na vifo hivyo vingi vikiwa ni vya ghafla na ambavyo havikutarajiwa kwani hakuna aliyekuwa akitarajiwa kwa kuwa hakuna aliyekuwa ameugua kwa muda mrefu na kusababisha watu labda wamkatie tamaa bali ni muda mfupi tu.
Wasanii wengi kutokana na misiba mfululizo wamejikuta wakikosa amani na wengine kusema kuwa inabidi wabadili mfumo wao wa maisha huku wakiwataka na wengine kubadilika kwani kifo hakina taarifa. “Kiukweli vifo hivi vimetushtua sana nawasihi wasanii wenzangu tubadili maisha yetu, tusiishi kwa mazoea, vifo vya wenzetu view funzo kwetu tuliobaki,” alisema Davina ambaye ni msanii wa filamu.
No comments: