WANAWAKE WAPEWA ADHABU YA KUCHIMBA KABURI ONYO LA KUUA WANAUME KICHAWI GEITA
Baadhi ya wanawake wa mtaa wa Buyegule wakichimba kaburi la marehemu Mkangiko Vigume aliyedaiwa kufariki katika mazingira ya kutatanisha na kudaiwa wanawake wanahusika kuua wanaume kishirikina katika mtaa huo.
Baadhi ya wanaume wakiwa wamekaa wakisubiri taratibu za mazishi.
***
Wanaume wa mtaa wa Buyegule kata ya Mtakuja Halmashauri ya Mji wa Geita wamewalazimisha wanawake wa mtaa huo kuchimba kaburi la marehemu Mkangiko Vigume kwa madai marehemu alifariki katika mazingira ya kutatanisha na kudaiwa wanawake wanahusika kuua wanaume kishirikina.
Imezoeleka kuwa kwenye jamii zetu wanaume ndiyo wanahusika wakuu wa kufanya shughuli za uchimbaji wa kaburi na kubeba mwili wa marehemu lakini kwenye mtaa huo hali imekuwa tofauti kutokana na madai ya wanaume kulalamika kuwa wameendelea kupoteza maisha kwenye mazingira ya kutatanisha na kujikuta wakiendelea kuisha na kuelezwa kufanya hivyo ni adhabu tosha kwa wanawake ambao wamekuwa na tabia za kishirikina.
Wakizungumza katika familia ya mzee Kangeko Vigume ambaye amefariki kutokana na kuugua ghafla wanaume wamesema kuwa tukio hilo la kufariki mwanaume sio la kwanza na kwamba hadi sasa kuna wanaume 7 wamepoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha yanayohusishwa na ushirikina.
“Kwa kweli sisi tumeumia sana kutokana na matukio haya kuendelea kujirudia mara kwa mara kwenye mtaa wetu, sisi wanaume ndiyo ambao tumekuwa tukifa, jambo la kushangaza wao hawafi wakifa ni kwa magonjwa ila sisi ni ghafla tu”,alisema Mussa John.
“Jambo la kusikitisha watu ambao tunawazika wamekuwa wakirudi na kutungongea hodi na huku sisi tunajua tumewazika hili ndilo linatushtua zaidi sisi kama wanaume wa mtaa huu”,alieleza Mzee Kahema Msabira.
Kwa upande wao wanawake wamesema kuwa kitendo ambacho kimefanywa na wanaume wa mtaa huo sio kitendo kizuri kwani walitishwa na kuambiwa kuwa wasipofanya shughuli ya kuchimba kaburi wataadhibiwa kwa kuchapwa viboko kila mmoja.
“Sikutaka kufanya shughuli hii ya kuchimba kaburi lakini jambo la kusikitisha nimelazimishwa tu, sisi wanawake tunaonewa sana kwani hakuna wanaume wachawi?”,alihoji Frola Nyanda.
Mwenyekiti wa mtaa huo,Andrew Barnabas amesema alishindwa kuzuia wananchi kufanya kitendo hicho kutokana na wengi wao kutokusikiliza hoja yake na kuamua kujichukulia maamuzi wao wenyewe.
Mkuu wa wilaya ya Geita, Herman Kapufi amesema watakwenda kwenye mtaa huo na kukutana na wananchi waweze kuwaelimisha ikiwa ni pamoja na kuwachukulia hatua watu ambao wamehusika kuhamasisha suala hilo.
Pamoja na wanawake kuchimba kaburi huku wanaume wakizika, wanaume wamewataka wanawake hao kujua kuwa hilo ni onyo na kwamba ikitokea mwanaume mwingine kufariki kwenye mazingira ya utata hawatashiriki kwa shughuli yoyote ile ikiwemo kuzika.
No comments: