ABAKA MTOTO KWA AHADI YA KUMPA ANDAZI
Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linamshikilia Amos Meshack (36), mfanyabiashara wa udongo wa pemba, kwa tuhuma za kubaka mtoto wa umri wa miaka tisa, mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Ndala A Manispaa ya Shinyanga.
Tukio hilo lilitokea juzi mchana nyumbani kwa mtuhumiwa huyo, Kata ya Ndala.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Simon Haule alisema chanzo cha tukio hilo ni tamaa za mwili.
Alisema mbinu iliyotumika ni mtuhumiwa kumwita mtoto kwa ahadi ya kumpatia Sh 200 kwa ajili ya kununulia maandazi.
“Kutokana na ahadi hiyo, mtoto aliingia katika nyumba au kibanda ambacho mtuhumiwa hukitumia kufanyia biashara ndogo ndogo za kufinyanga na kutengeneza udongo wa pemba, alimkamata na kumbaka akimsisitiza asieleze chochote kwa mtu yeyote.
“Hata hivyo, mama mzazi wa mtoto aligundua tukio la kubakwa kwa mwanaye baada ya kumuona akiwa hana furaha na kuamua kumdadisi,” alisema.
Alisema aligundua mwanae amebakwa baada ya kuona nguo zake za ndani zikiwa zimefichwa nyuma ya kitanda, huku akionekana mnyonge.
Alisema baada ya kumhoji mwanae alidai alibakwa na baba Amani ambaye ni Meshack, na kuwa huo ndiyo mchezo wake wa kila siku.
Alisema wakati akianza uchafu huo, alikuwa akimpatia pipi na safari hii alimnunulia maandazi kisha kumvutia ofisini kwake na kumbaka tena.
“Alipelekwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga kupimwa na majibu ya daktari yalivyotoka ilibainika amebakwa…mchezo huo amekuwa akifanyiwa kila mara na siyo mara moja,”alisema.
Kamanda Haule alisema wanamshikilia mtuhumiwa na baada ya uchunguzi kukamilishwa atafikishwa mahakamani.
No comments: