KANISA LAPIGA MARUFUKU SHELA KWA WAJAWAZITO WAKATI WA NDOA
KANISA Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, limewapiga marufuku wanawake wajawazito kuvaa shela wakati wa kufunga ndoa kwa madai vazi hilo ni alama ya ubikira kwa mwanamke na sio vinginevyo.
Hayo yamesemwa na Paroko Msaidizi wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Theresa, Padre Festus Mangwangi wakati akiweka mkazo juu ya tamko lililotolewa na Askofu Mkuu wa Jimbo hilo Isaack Amani, wakati akiadhimisha misa ya shukrani iliyofanyika Jumapili iliyopita, baada ya kuteuliwa kwake na Baba Mtakatifu Francis kuwa Askofu Mkuu wa Jimbo hilo.
Kabla ya uteuzi huo uliotangazwa Desemba 27 mwaka 2017, Askofu Mkuu Amani alikuwa Askofu wa Jimbo la Moshi na kusema haitakiwi kwa mwanamke yeyote ambaye anajijua ni mjamzito kuvaa shela kipindi anafunga ndoa kwa kuwa vazi hilo linavaliwa na mwanamke asiyemjua mwanaume (bikra).
Aidha, Padre Festus Mangwangi amewataka wazazi kuwafundisha watoto wao wa kike kutunza miili yao na kuishi maisha ya kimaadili hadi watakapopata wenza wa kufunga nao ndoa na hapo ndipo alama ya shela itakapoonekana umuhimu wake.
“Tamko la Askofu Mkuu linatekelezwa kwa kuwaeleza maharusi watarajiwa wanapokwenda kupata mafundisho ya ndoa kwa katekista na baadaye padre, kuwa kama ni wajawazito basi wasivae shela na hata wale wanaowajua wanaume pia wanashauriwa wasivae”, amesema Padre Festus.
Pamoja na hayo, Padre Festus ameendelea kwa kusema “wanaojitambua kuwa si bikira, hawavai shela, lakini wako wanaojificha na kuvaa shela, hii inakuwa sawa na kudanganya”.
Kwa upande mwingine, Padre Festus amesema endapo atatokea mtu akadanganya na kuvaa shela wakati tayari anamjua mwanaume au kuwa mjamzito basi atakuwa anafanya utovu wa nidhamu.
Nipashe.
No comments: