KIAMA WALIOFICHA MAFUTA YA KUPIKIA
Serikali imetangaza msako mkali dhidi ya wafanyabiashara waklioficha shehena ya mafuta ya kupikia na kusababisha upungufu wa bidhaa hiyo nchini.
Utakuwa
mask wa pili wa bidhaa za vyakula tango mwaka 2016 baada ya kampeni ya sukari.
Imesema kamwe haitakubali wananchi
kuchezewa na wafanyabiashara wasio waaminifu, hivyo imetoa siku tatu kwao
kuhakikisha wanasambaza mafuta haraka.
Ili kuhakikisha agizo lake
hilo linatekelezwa kikamilifu, imesema kuanzia Jumapili msako mkali utafanyika
kwenye viwanda na maghala yote kuwabaini walioficha bidhaa hiyo muhimu kwa
wananchi.
Kwa siku tatu mfululizo,
Bunge limekuwa kwenye mjadala mzito kuhusu upungufu wa mafuta ya kupikia huku
baadhi ya wabunge wakikiomba Kiti cha Spika kuitaka serikali kutoa kauli
bungeni kuhusu upungufu huo.
Na kutokana na mjadala huo
mzito, juzi asubuhi Spika wa Bunge, Job Ndugai, aliiagiza serikali kuhakikisha
inatoa majibu ya uhakika bungeni jioni kuhusu uhaba wa mafuta ya kupikia
uliosababisha bidhaa hiyo kupanda bei mara dufu.
Hata hivyo, serikali ilishindwa
kutekeleza agizo hilo la Spika kutokana na kile kilichoelezwa na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Vijana, Kazi na Watu Wenye
Ulemavu, Jenista Mhagama kwamba walihitaji kuwa na majibu kamilifu hivyo
akaomba majibu ya serikali yatolewe Jumatano (jana) saa 11 jioni.
Akitoa kauli hiyo ya
serikali jana bungeni mjini hapa, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema kwa
takwimu zilizopo, nchi haikupaswa kukabiliwa na upungufu wa mafuta ya kupikia.
Alisema wastani wa lita za
mafuta ghafi ya kupikia tani 30,000 zinaingizwa nchini na wafanyabiashara huku
matumizi kwa mwezi yakiwa wastani wa tani 28,900.
"Mafuta yaliyoagizwa
kuanzia Januari hadi Machi mwaka huu yalikuwa na uwezo wa kutosheleza mwezi
Aprili na mafuta ya Mei ambayo yameendelea kupokewa kusingekuwa na upungufu wa
mafuta," Waziri Mkuu alisema na kuongeza:
"Jambo hili hatuwezi
kukubaliana nalo tukaliacha lilivyo kwa sababu upo mpango unaoonekana wa kutaka
kuwayumbisha watanzania katika kipindi hiki ambacho tunajua waislamu wanakaribia
kufunga.
"Natoa maelekezo kwa
wafanyabiashara wanaohusika na mafuta pamoja na sukari, tunatoa siku tatu
kuanzia kesho (leo) Alhamisi, Ijumaa na Jumamosi, mafuta yote yaliyopo
yaondolewe yaendelee kupatikana nchini, ili Watanzania wasihangaike na wasilazimike
kununua kwa bei ya juu."
Kiongozi huyo wa serikali
alisema kuanzia Jumapili, serikali italazimika kuingia viwandani na kwenye
maghala kuhakiki kama mafuta yapo au hayapo.
Majaliwa alieleza hatua hiyo
inafanyika kwa sababu shida wanayokabiliana nayo wananchi, hivyo serikali
haiwezi kuvumilia.
"Jambo hili halipo kwa
bahati mbaya, mafuta yapo wananchi wanaweza kununua tena kwa bei ileile. Kwa
hiyo, nataka wabunge mtambue mafuta tunayo na taratibu za kusambaza zinafanyika
kuhakikisha yanapatikana kwenye maeneo yote kwa bei ileile," alisema.
Awali akiwasilisha taarifa
yake bungeni jana kama alivyotakiwa na Spika, Waziri wa Viwanda, Biashara na
Uwekezaji, Charles Mwijage, alielezea uhalisia wa sakata hilo la uhaba wa
mafuta kama aliyoagizwa na kiongozi huyo wa Bunge.
Mwijage alisema vyanzo vinavyotumika
kuzalishia mafuta nchini vinatosheleza mahitaji kwa asilimia 30, hivyo asilimia
70 huagizwa kutoka nje ya nchi.
Alibainisha kuwa katika
miezi mitatu ya mwanzoni mwa mwaka huu, yaani kuanzia Januari, wastani wa
mafuta yaliyoagizwa ni tani 30,210.71 na jumla ya akiba ya mafuta yaliyopo
nchini ni wastani wa tani 68, 902.
Alizitaja kampuni
zilizoagiza mafuta hayo kuwa ni East Coast, BIDCO, Mulza Oil na G and B
na Mikoani Trades na mafuta yaliyopo kwenye meli ambayo yanasubiriwa kushushwa
bandarini ni wastani wa tani 40,000.
Alisema mafuta yanaposhushwa
bandarini, Shirika la Viwango (TBS) huchukua sampuli kuzipima kisha matokeo
hayo huwasilishwa kwa Mamlaka ya Mapato (TRA).
Waziri huyo alisema kuwa kwa
mujibu wa taratibu, TRA huwataka waagizaji wa mafuta kuwasilisha nyaraka
mbalimbali kutoka kwenye mamlaka zinazotambulika kwenye nchi ambazo mafuta
yametoka.
Alisema kuwa baadhi ya
nyaraka hizo ni vielelezo vinavyoonyesha malipo ya mizigo iliyoingizwa.
Mwijage alisema kumebainika
utata wa viwango kwenye mafuta yaliyopo bandarini tani 68,000.
"Waagizaji pamoja na
kutakiwa kuwasilisha nyaraka muhimu zinazohitajika hawakufanya hivyo. Pamoja na
wastani wa uagizaji mafuta mwaka huu kuonyesha kuwa juu ya wastani wa mwaka
jana, inashangaza kuona kuna uhaba wa mafuta. Ukweli ni kwamba ilitegemewa
mafuta yaliyopo nchini yangeweza kutosheleza nchi," alisema na
kuongeza:
"Naomba Bunge lako
lifahamu kuwa kiwango cha mafuta ghafi yalipo nchini kinatosheleza. Kufuatia
kiasi cha mafuta ghafi yaliyaogizwa kwa miezi mitatu, tunapaswa kuwa na mafuta
yenye kutosheleza kwa sasa.
"Serikali itahakikisha
wananchi wanapata mafuta kama ilivyokuwa kawaida na katika kipindi cha mwezi
Mtukufu wa Ramadhani, serikali haitakubali kuchonganishwa na wananchi kwa watu
wachache kusababisha upungufu wa mafuta na bidhaa nyingine."
Baada ya maelezo hayo ya
Mwijage, ndipo Waziri Mkuu aliposimama na kutoa kauli bungeni kuhusu msako
dhidi ya wafanyabiashara walioficha mafuta ya kupikia.
NIPASHE
No comments: