Header Ads

Blogger Tips and TricksLatest Tips And TricksBlogger Tricks

SUGU MOTO CHINI :: Asema aliyemshataki amempa tiketi muhiu

Mbunge wa Mbeya Mjini  (Chadema), Joseph Mbilinyi ' sugu'  jana aliachiwa huru kutoka greza za Ruanda la mjini hapo kwa msamaha wa Rais Magufuli, baada ya kutuikia kifungo jela kwa siku 73.

Sugu, msanii wa muziki wa kizazi kipya, aliachiwa pamoja na Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga, ambaye kwa pamoja Februari 26 walihukumiwa kifungo cha miezi mitano jela na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, baada ya kukutwa na hatia ya kutoa lugha ya fedheha dhidi ya Rais.

Sugu na Masonga waliachiwa huru jana asubuhi na kupokelewa kwa shangwe nyumbani kwake na wanachama wa Chadema, akiwamo Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe na baadhi ya wabunge wake.

Akiwa nyumbani kwake eneo la Ituha mjini hapa, Sugu alisema taarifa za kutoka gerezani walipewa juzi na ilipofika asubuhi jana walitolewa na kupelekwa nyumbani hapo kwa gari la Mkuu wa Gereza la Ruanda.

“Nawapa pole Wanambeya wenzangu (maana) nayajua machungu mliokuwa nayo (kwa kipindi chote)," alisema Sugu. "Mliumizwa mioyo na saikolojia, lakini nawasihi msilipe kisasi."

"Kisasi mtalipa (kwenye uchaguzi mkuu) 2020.

"Niliingia gerezani kwa utata na nimetoka kwa utata.”

Alieleza mazingira ya gerezani yamempa nguvu mpya kisiasa ya kuendelea kupambana bila kuogopa, ili kuona haki inatendeka kwa vyama vya upinzani.

Akizungumzia kuachiwa huko, Mkuu wa Magereza Mkoa wa Mbeya, Paul Kijida, alisema viongozi hao wametoka kwa msamaha wa Rais Magufuli alioutoa Aprili 26 kuadhimisha miaka 54 ya Muungano wa Tanzania, jijini Dodoma.

Katika kuadhimisha siku hiyo, Rais Magufuli aliamuru kupunguzwa kwa robo ya adhabu za wafungwa 3,319 ambapo 585 walitoka siku hiyo hiyo.

Kijida alisema kulingana na hesabu zilizopigwa kulinganisha na muda waliokaa gerezani, Sugu na Masonga walistahili kuachiwa jana.

“Katika hesabu zetu siku zao za kukaa gerezani zimekoma leo (jana), hivyo kuachiwa kwao ni sahihi kabisa kwa mujibu wa sheria.”Akifafanua zaidi, Kijida alisema kuwa hilo sio jambo jipya kwani wapo wafungwa wanaofungwa miaka mingi wanaweza kupewa msamaha wa sehemu ya muda wa kifungo chao na unapofika hata kama ni baada ya miaka miwili au mitatu tangu msamaha utolewe, huachiwa huru.

“Wapo wanaofungwa hata miaka 30, Rais anaweza kuwapunguzia kifungo chao kwa miaka miwili hivyo muda wa kifungo chao pamoja na ule wa msamaha unapofika tunawaachia hata kama itakuwa ni baada ya miaka kadhaa kupita,” alisema Kijida.

Kwa upande wake, Katibu Masonga alisema wanamshukuru Mungu kutoka gerezani wakiwa salama na kwamba kifungo hicho kimewafundisha mambo mengi ikiwamo ukandamizwaji na namna haki inavyominywa.

Alisema gerezani walikuwa wakiishi maisha magumu ukilinganisha na vile Serikali inavyodai kuwa imeboresha mazingira ya wafungwa.

“Kupitia kifungo hiki ambacho naamini kimenipa ushujaa zaidi, nitaendelea kupigania haki hata kama nikirudishwa tena sijali,” alisema Masonga.

Mwenyekiti wa Chadema Mbowe alisema chama chake kitaendelea na rufani ambayo walishaikata ili kuhakikisha haki inatendeka.

KUFUTA DOAMbowe alisema wameamua kuendelea na rufani, ili kufuta doa la wao kubambikiziwa kesi.

"Tumekata rufani kwa ajili ya kufuta doa dhidi ya viongozi wetu ambao walihukumiwa kwenda jela, tunafanya hivyo, ili kuondoa doa ambalo linaweza kuchafua historia yao katika vizazi vijavyo," alisema Mbowe.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Mbeya kupitia Chadema, Sophia Mwakagenda, alisema kuachiwa kwa Sugu kunawaongezea nguvu ya kuwatetea Watanzania bungeni.

Febrauri 26, Hakimu Mkazi Mfawidhi Michael Mteite alitaja maswali matatu yaliyomfanya afikie uamuzi wa kuwatia hatiani 'Sugu' na mwenzake.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mteite alisema Mahakama imejiridhisha kuwa ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri ulikuwa ni wa kweli kwani waliona na kusikiliza maneno yaliyotolewa.

Hakimu Mteite alisema kabla ya kufikia uamuzi wake, hata hivyo, Mahakama imeona viini vitatu ambavyo vilitengeneza maswali katika kesi hiyo.

Aliyataja maswali hayo kuwa ni je, maneno yaliyotolewa na washtakiwa kweli yalikuwa ni ya fedheha dhidi ya Rais? Mlengwa katika shauri hilo ni Rais John Magufuli kweli? Na je, washtakiwa walitoa maneno hayo?

Katika dhana hiyo, Hakimu Mteite alisema kutokana na ushahidi uliotolewa na upande wa Jamhuri ni kweli washtakiwa walitoa maneno hayo, na kwamba waliyekuwa wanamsema ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Haya maneno ya washtakiwa kuwa huwezi kupendwa kwa 'kumshuti' Lissu, kumteka Ben Saanane, watu kuuawa mchana kweupe na kufungwa kwenye viroba, Rais anatubadilishia aina ya kututawala... ni ya kitaifa na yanamhusu Rais Magufuli ambaye ndiye mtawala,” alisema Hakimu Mteite.

Akitoa utetezi ili kina Sugu wapunguziwe adhabu, Wakili Peter Kibatala alisema hakuna kumbukumbu ya washtakiwa kufanya kosa hilo awali na kwamba “Rais ni mwanasiasa kama ilivyo kwa washtakiwa.

"Hivyo maneno yaliyotolewa ni ya kisiasa na yachukiliwe hivyo hivyo.

"Ni kweli Mlengwa alikuwa ni Rais Magufuli (lakini) hakuna ushahidi unaoonyesha hadhi ya Rais imeshuka.”

Awali wakati wa usikilizaji shauri hilo, washtakiwa hao walikana kutumia lugha ya fedheha dhidi ya Rais Magufuli na kwamba sauti zilizokuwa zimetolewa kortini kama kielelezo si zao.

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya ilianza kusiliza kesi hiyo Januari 16, mwaka huu.

Ilidaiwa mahakamani hapo kuwa Sugu na mwenzake walitumia lugha za fedheha dhidi ya Rais John Magufuli Desemba 30, mwaka jana katika viwanja vya Shule ya Msingi Mwenge.

NIPASHE

No comments: