WARAKA WA KKKT WANG'OA KIGOGO
Msajili wa vyama katika Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Maryline Komba, amesimamishwa kazi ili kupisha uchunguzi wa barua anayodaiwa kuwaandikia maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)
Uchunguzi huo unakuja baada ya barua hiyo kusambaa kwenye mitandao ya kijamii ikiwa na saini yake na serikali imesema inataka kujiridhisha kama iliandikwa kweli na ofisi hiyo ya msajili huyo au la.
Barua hiyo imesambaa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na kuwa maarufu, ilitoa siku 10 zinazoisha kesho kwa maaskofu wa kanisa hilo ambalo ni la pili kwa kuwa na waumini wengi nchini, kufuta waraka wake wa Pasaka uliotolewa Machi 24, mwaka huu.
Akizungumzia barua hiyo jana jijini Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba, alisema kama barua hiyo imeandikwa na msajili huyo, basi haikuwa na baraka za wizara wala serikali.
Mwigulu alisema moja ya barua zinazosambaa mitandaoni ina saini ya msajili huyo ingawa suala hilo halikupewa baraka za wizara, serikali wala si maelekezo ya serikali, hivyo ni batili.
“Kwa sababu nyaraka zimetoka nyingi, tunaendelea kufanya uchunguzi kujua lengo lake ni nini. Wakati uchunguzi ukifanyika ili kujua nyaraka ipi ni ipi, namsimamisha kazi msajili aliyeandika barua hiyo,” alisema Mwigulu.
“Ikithibitika kama nyaraka hizi zimeandikwa na Wizara, lazima tujue undani wake kwa nini mambo yanayoleta uchochezi yanaandikwa tena kwa barua isiyo na nakala kwa Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu, Waziri, Naibu Waziri wala si msimamo au maelekezo ya serikali,” alisema.
Katika mkutano huo ulioitishwa wizarani hapo, Dk. Mwigulu aliwaeleza waandishi wa habari kuwa ziko nyaraka zinazozunguka kwenye mitandao ya kijamii zilizo halali na zisizo halali zilizotumia teknolojia zinazotengeza taharuki kwa faida ya watengenezaji wenyewe. Alisema amejitokeza kujibu kwa kuwa wizara yake ndiyo inayohusika na usimamizi na uendeshaji wa masuala ya kiimani yakiwamo yale yote yanayohusu dini.
“Mambo haya ya nyaraka au matamko yalitolewa miezi miwili iliyopita ni jambo lililopita. kama serikali hilo jambo halijawahi kuwa tatizo kwa maana kwamba waliotoa waraka walitoa maoni yao,”alisema na kuongeza:
“Jambo hili limesababisha taharuki na hizi taarifa ni batili na ombi langu kwa viongozi wa dini waendelee na kazi zao wasiingie katika taharuki kwa taarifa hii batili,” alisema.
Dk. Mwigulu alisema ziko taratibu za kikatiba za kuendesha masuala ya kiimani na wala Tanzania haijawahi kutokuaminiana na taasisi hizo katika shughuli za kila siku za kimaendeleo.
“Jambo hili lililoleta taharuki ni batili si maelekezo ya serikali wala wizara. Kwa kuwa teknolojia ni nyingi, ziko nyaraka zimewekwa vichwa vya habari kwa maslahi yao binafsi, viongozi wetu wa dini na waumini walioguswa na waliopata mshtuko watambue taarifa hii ni batili waendelee na kazi zao, wafanyie kazi vitu ambavyo vina uhalali,” alisema.
“Mara zote tumekuwa tukielekeza na kutoa rai kuwa serikali inaheshimu katiba na uhuru wa kuabudu na wizara inasimamia masuala ya Amani. Mtu yeyote anayetengeneza mgawanyiko katika jamii kwa namna yoyote kwa faida yake au kwa kutumika atambue kwamba serikali haiwezi kuvumilia,” alisema.
“Mambo yanayoleta mgawanyiko kwa taifa tusiyashabikie. Ni vyema tutangulize uzalendo. Amani ikivunjika ni vigumu kuirejesha. Kwa mamlaka niliyopewa ya kusimamia Amani, nitoe rai kwa watu wanaopenda kushabikia vitu vinavyoleta uchochezi au mgawanyiko kwa sababu vikitokea ni vigumu kurejesha zaidi ya kuacha makovu,”alisema.
Aliwataka waandishi wafikishe taarifa kwa umma kuwa waache kushabikia taarifa ambazo hawana uhakika nazo au zinazoleta mgawanyiko katika jamii au zinaleta mgawanyiko kwa manufaa ya makundi yanayolenga kupata faida binafsi za kisiasa au wanazojua wenyewe,” alisema. “Kuna wengine walikuwa wananipigia na wengine wanabeba suala hili kiajenda zaidi na wengine nilishawaambia hili jambo ni batili halina ukweli wala baraka za serikali wala wizara lakini kwa sababu linatengeneza mgawanyiko kwa waumini wanaona ni ajenda, Watanzania tukatae vitu vinavyotugawa na kutuletea matatizo yasiyo na ulazima,” alisema.
Alitoa rai kwa viongozi wa kiroho watambue serikali inaendelea kulinda katiba kama ilivyo kwenye viapo kuhakikisha uhuru wa kuabudu na maoni na kila mmoja anafanya kazi kwa kutimiza masharti ya kazi.
Kuhusu taarifa kuwa KKKT wameeleza wako tayari kukutana na serikali ndani ya siku 30 badala ya 10 kama ilivyotakiwa, Mwigulu alisema hilo ni jambo la kawaida kwa serikali kukutana na taasisi na kwamba ziko zilizoomba kuonana na wizara na zingine wamepanga kukutana nazo. Alisema serikali haijawahi kutokuwa na imani na taasisi hizo na kwamba inashirikiana nazo na wanakwenda vizuri.
“Kwa nini paonekane pana msuguano kwenye nchi yetu kati ya serikali na taasisi hizi? Serikali hatujawahi kutokuwa na imani wala kutokuaminiana na taasisi hizi wala kutokuaminiana na viongozi wa taasisi hizi. Tunashirikiana, tunakwenda vizuri na wote tumekubaliana kuiishi katiba,” alisema.
NIPASHE
No comments: